Dar es Salaam. Kupanda kwa gharama za maisha kumeathiri wanafunzi vyuoni nchini Tanzania, baadhi wakilazimika kuahirisha masomo.
Wanaoathiriwa zaidi ni wanafunzi wanaotegemea msaada wa familia, ambao kunapotokea changamoto ya hali ngumu za kiuchumi huathirika.
Kutokana na changamoto hizo, baadhi huahirisha masomo kwa muda ili kufanya kazi za muda mfupi au biashara ndogondogo ili kujikimu, hivyo huathiri si tu maendeleo yao ya kitaaluma bali pia ustawi wa kisaikolojia, kwani hushindwa kuzingatia masomo kutokana na msongo wa mawazo.
Katika hilo, wadau wa elimu wanashauri kuwe na mfumo imara wa mikopo ya dharura kwa wanafunzi wanaokumbwa na changamoto za kiuchumi ili kuhakikisha hali hiyo haiwi kikwazo kwa haki ya kupata elimu ya juu.
Takwimu zinaonyesha kuwapo ongezeko la asilimia zaidi ya 100 la wanafunzi wanaolazimika kuahirisha masomo kutokana na kukwama kiuchumi.
Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iliyotolewa Mei mwaka huu inaonyesha wanafunzi 761 waliahirisha masomo kutokana na mkwamo wa kiuchumi mwaka 2023/2024 ikiwa ni ongezeko kutoka wanafunzi 267 mwaka uliotangulia.
Kundi hilo lilibeba asilimia 39.1 ya wanafunzi 1,943 walioahirisha masomo katika mwaka husika huku wengine 721 wakiahirisha mwaka kutokana na sababu za kimasomo, 257 sababu za kijamii, 144 sababu za kikazi na 60 kwa changamotomza afya.
Akizungumzia suala hilo, mdau wa elimu Dk Luka Mkonongwa amesema licha ya Serikali kutoa mikopo, wapo baadhi ambao asilimia ya mkopo wanaopata hawawezi kumudu maisha ya chuo.
Baadhi ya wanafunzi hupata mkopo wa asilimia 20, 40, 80, 60 na 100 kulingana na tathimini iliyofanyika.
“Kwenye mazingira ya chuo wanapambana na changamoto nyingi, kama anapata asilimia 20 na mahitaji yake chuoni ni mengi atafikiria kuacha chuo akajipange kwenda kutafuta maisha na akirudi awe imara,” amesema.
Dk Mkonongwa amesema wapo wanaokwenda kujipanga na kurudi, lakini wengine huacha na kwenda kuangalia mambo mengine.
“Hii ya kuacha chuo kabisa huchochewa pia na hali ya upatikanaji wa ajira, mtu akikwama kiuchumi akaangalia waliomaliza vyuo na hawana ajira anaona bora ajikite kutafuta hela kabisa au akipata sehemu nyingine ya kazi anaamua kuacha chuo ili apate hela,” amesema.
Katika mwaka wa masomo 2025/26 ili kuwawezesha kupata urahisi na kumudu mahitaji yao Sh916.7 bilioni zimetengwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu 99,620 wa mwaka wa kwanza katika ngazi za diploma, shahada ya kwanza na shahada za uzamili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la uombaji mikopo alisema wanafunzi 88,000 wa shahada ya kwanza watapangiwa mikopo hiyo.
Amesema idadi hiyo ni ongezeko la wanufaika 8,000 ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2024/25 ambao wanufaika 80,000 walipangiwa mikopo.
Kwa wanafunzi wa diploma amesema mwaka huo wa masomo wanufaika 10,000 watapata mikopo ikiwa ni ongezeko la wanufaika 3,000 ikilinganishwa na ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita.
Amesema fedha hizo zitatumika pia kwa wanafunzi 173,783 wanaoendelea na masomo.
“Tunazidi kuongeza wigo wa wanafunzi wanaopata mikopo, mwaka huu hata wanafunzi wa diploma idadi yao imeongezeka hapa lengo ni kuhakikisha wanapata elimu bila kujali hali zao,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi waliowahi kuahirisha masomo, Yasri Juma amesema alikwenda kufanya kazi ili kurudi shuleni.
“Lakini nilirudi chuo kwa shinikizo, haikuwa ridhaa yangu maana niliona kama nimeshatengeneza fedha, basi sina haja ya kumalizia mwaka uliobakia. Nilipata sehemu ya uhakika ambayo ilinihitaji nirudi chuo hivyo nilirudi,” amesema.
Amesema aliacha masomo kutokana na hali ngumu ya maisha nyumbani kwao. Kabla ya kuingia mwaka wa pili baba yake aliyekuwa akimlipia ada alifariki dunia, hivyo alibeba jukumu la kulea familia.
“Ni kama nilikuwa na bahati, vipi wengine ambao hawakupata nafasi ya kufanikiwa huko nje walipokwenda na kurudi chuo, ndoto zao zimezima. Ni vyema mfumo wa uwezeshaji wanafunzi uwe imara,” amesema.
Dk Mkonongwa amependekeza kuangalia upya tathmini zinazofanywa na bodi katika utoaji mikopo na isiangalie mtu amesoma wapi sekondari ya awali na upili, hatua itakayowasaidia waliopata ufadhili katika ngazi hizo za masomo na waliowafadhili hawapo tena.
“Hii ya kuendelea kuhisi kuwa aliyekuwa anamsomesha bado yupo kumbe mzazi, ndugu aliyekuwa anajitolea au shirika hayupo tena hii tathmini si sahihi,” amesema.
Amependekeza mkopo uombwe kulingana na uhitaji, kwani wapo ambao wangeweza kuamua kuwa hawahitaji na watalipa asilimia zote wenyewe.
Amesema kukosekana ushauri ni moja ya sababu inayofanya watu wachukue uamuzi ambao baadaye huujutia.
Ameshauri ni vyema wanapoanza vyuo wapewe ushauri, wawe wavumilivu katika mapito ya kiuchumi na kijamii wanapokuwa vyuoni kwani baadhi ya sababu zinazotolewa zinaweza kutatuliwa kwa ushauri.