Ukaguzi wabaini maabara binafsi kufanya tohara, kulaza na kutibu wagonjwa, TMDA yatoa kauli

Mwanza. Tathmini ya uendeshaji wa maabara binafsi za afya, iliyofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, imebaini kasoro kadhaa pamoja na vitendo vinavyohatarisha afya ya jamii vinavyofanywa na baadhi ya maabara hizo.

Miongoni mwa dosari zilizogundulika ni pamoja na maabara hizo kutoa huduma za tiba bila kibali halali, kujigeuza kuwa zahanati, na hata kulaza wagonjwa, hatua ambazo ni kinyume na sheria na taratibu zinazosimamia utoaji wa huduma za maabara ya afya nchini.

‎Nyingine ni kutoa majibu ya vipimo yasiyo sahihi, kuchoma wagonjwa sindano, kufanya tohara, kutokuwa na usajili (maabara bubu), kuhifadhi vitendanishi vya Serikali, baadhi ya maabara hizo kukosa wataalamu wenye sifa kutokana na wamiliki kukwepa gharama, na kuwa na vifaa vya kufanyia uchunguzi visivyo na sifa.

‎Mapungufu yaliyobainishwa yametajwa kuhatarisha afya ya jamii kwa kusababisha usugu wa dawa kutokana na wataalam wa maabara kutoa dawa na tiba, kuelekeza dawa zisizo sahihi na kuathiri figo huku ikiifanya Tanzania kuonekana ni taifa la wababaishaji.

‎‎Hayo yameelezwa leo Ijumaa Julai 18, 2025 na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RMO), Silas Wambura wakati akizungumza katika kikao kazi na wamiliki wa maabara binafsi katika wilaya za Ilemela na Nyamagana, kilichoandaliwa na TMDA ili kuwajengea uwezo na kutambua majukumu yao.

‎‎”Maabara hizi haziruhusiwi kutoa huduma za tiba kazi yenu ni kupima, lakini mmegejiuza zahanati mpaka mnachoma wagonjwa sindano, yawezekana mnawatumia wataalam lakini pale hapajasajiliwa kufanya hiyo kazi.

“Tuna tatizo la usugu wa dawa na wataalam wa maabara wanachangia kwa kutoa dawa na tiba. Huu usugu wakati mwingine unasababishwa na wao kwa kutoa dozi za dawa wakati hawaruhusiwi kisa tu wanataka kuonyesha wao ni mabingwa na wataalam,” amesema.

‎‎Wambura amewataka wamiliki hao kuacha kuangalia faida pekee wakati wanaangamiza maisha ya watu, bali wafanye kazi kwa kufuata taratibu, kanuni, na miongozo iliyowekwa na Serikali ili kulinda afya za watu.

‎‎”Timu za afya ngazi ya mkoa na halmashauri zinafanya ufuatiliaji na kaguzi, pia wizara na TMDA nao wanachukua hatua mbalimbali, na tunapogundua tatizo mojawapo ya hatua ndiyo kama hizi kuwajengea uwezo na kuona namna gani wanaweza kutoa huduma saama,” amesema Wambura.

‎‎Naye, Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mziray amesema tathmini hiyo ni kuanzia mwaka 2020/2021 – 2024/2025, ambapo wameitisha kikao hicho ili kuwakumbusha wamiliki hao majukumu, wajibu, na sheria katika shughuli wanazozifanya.

‎‎”Tunaamini kabisa kikao hiki kitasaidia kuweka uelewa wa pamoja baina yetu na hawa wadau wetu kwa sababu matibabu sahihi yanapatikana endapo kukiwa na uchunguzi sahihi. Kwa mujibu wa sheria ya TMDA sura ya 219 wanaofanya makosa haya wanaweza kupigwa faini au kufunguliwa kesi,” amesema Mziray.

‎‎Mwenyekiti wa wamiliki wa maabara binafsi mkoani Mwanza, Natus Magori ‎amesema baadhi ya changamoto zinazotokea ni bahati mbaya ama hitilafu hususan kwenye utoaji wa majibu ya vipimo kwa wagonjwa, na siyo makosa ya wamiliki.

‎‎Amekiri kwamba mwanzo kumekuwa na kutoelewa dhidi ya wakaguzi kutoka TMDA, lakini baada ya kikao hicho watawekana sawa na kuweka makubaliano ya namna ya kufanya kazi na kuendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu.

‎‎Mmoja ya washiriki wa kikao hicho, Justina Malima amesema ukiukwaji huo unasababiswa na wamiliki kupuuza kwa makusudui na kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa kutosha kutoka kwenye mamlaka zinazohusika.

“Tuhuma kama hizi zimeleta athari kwetu wamiliki kwa sababu inaonekana watu wote wa maabara hawako manini, na wenye maabara bubu wanatukosesha mapato sisi tuliosajiliwa,” amesema Justina.