Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi nchini wametoa maoni wakipendekeza namna ya kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ili kuhakikisha Taifa linatimiza malengo yaliyokusudiwa katika ukuaji uchumi.
Dira ya Taifa 2050 iliyozinduliwa jana Alhamisi Julai 17, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma imeweka malengo ya ukuzaji wa pato la Taifa, uwezeshaji wa sekta binafsi, ukuzaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani ili kutimiza lengo la nchi kujitegemea kiuchumi.
Hatua hii imetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi nchini kama mpango madhubuti unaohitaji kuwekewa mazingira rafiki ya utekelezaji na utatuzi wa vikwazo katika utekelezaji wake.
Kwa kufanya hivyo wanasema kutahakikisha yaliyoainishwa ndani ya dira yanatimia, kwani ndiyo ukombozi wa Taifa.
Akizungumzia na Mwananchi leo Ijumaa Julai 18, 2025 mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema Dira 2050 ni nzuri iliyogusa nyanja muhimu katika ukuzaji uchumi wa Taifa.
Hata hivyo, ametahadharisha kuwa uzuri wake pekee hautoshi, bali utekelezaji ndiyo muhimu zaidi.
“Dira hii imegusa maeneo muhimu, kuweka lengo kuwa kila mtu awe na uchumi mkubwa ifikapo 2050 ni kitu kizuri lakini lazima tujue kuwa na dira nzuri ni kitu kimoja lakini utekelezaji wake ni kitu kingine,” amesema.
Mtaalamu huyo wa uchumi anasema uzuri wa dira utakuwa na umhimu ikiwa tu yale yaliyoainishwa ndani yake yatashuka kwa jamii yakatekelezwa, huku akitahadharisha kuwa zipo changamoto ambazo lazima zitatuliwe kuwezesha utekelezaji.
“Ili dira hii iweze kutekelezeka na Taifa linufaike na mazuri yake, mambo mawili muhimu ni lazima yafanyike. Kwanza, ni lazima yawekwe mambo yatakayochochea utekelezaji na pili, ni lazima yawepo mambo yatakayoondoa vikwazo vya utekelezaji wake,” amesema.
Profesa Kinyondo amesema miongoni mwa mambo yanayohitajika ili kuchochea utekelezaji ni kuboresha rasilimaliwatu.
Vilevile, amesisitiza ni muhimu jamii nzima kuyajua na kuyaishi maudhui yaliyoainishwa katika dira ili kila mtu awe sehemu ya utekelezaji katika eneo lake.
Amesema lazima jamii ihusike, pia bidhaa za ndani zitumike kwenye miradi ya ili kuwezesha mzungumko wa fedha nchini.
“Tunapotaka kujenga uchumi wa kujitegemea lazima tujue watu wa ndani na malighafi za ndani zinatumika kwa kiwango gani katika uwekezaji wa miradi, ikilinganishwa na watu na bidhaa kutoka nje. Tusiangalie watu pekee,” amesema.
Kuhusu mambo yatakayoondoa vikwazo vya utekelezaji wa dira, Profesa Kinyondo amesema kunahitajika misingi ya utawala bora na wa sheria, unaojali haki za watu katika kumiliki mali ili wafanye kazi na kunufaika na rasilimali zao bila kuingiliwa wala kuporwa na wenye nguvu.
“Hakuna nchi iliyowahi kuendelea bila kuzingatia haki za watu katika kumiliki mali bila kuporwa na wakawa na nafasi ya kushtaki na kushinda kesi mahakamani, watu wakiwa na haki ya kumiliki ardhi na mamlaka zikathaminisha ardhi yao na mali zao, hata kama wapo vijijini wanaweza kunufaika na mali hiyo katika huduna nyingi, ikiwemo kupata mikopo katika taasisi za fedha na kuboresha uwekezaji wao,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Kinyondo, misingi ya kisheria inapaswa ibadilike ili kuendana na matakwa ya Tanzania ambayo imetajwa katika Dira 2050, akizungumzia mabadiliko ya Katiba, sera na miongozo mbalimbali kama mahitaji katika kuwezesha utekelezaji wa dira hiyo.
Kwa upande wake, mtaalamu wa uchumi kutoka Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tobias
Swai, amesema ubora wa dira hii ni kuwa imejengwa katika misingi ya kujaza upungufu uliopo katika dira iliyopita ya mwaka 2000 – 2025.
Mhadhiri huyo anaona kuwa taasisi za fedha nchini ni wadau muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa dira ikiwa msingi wake mkubwa ni ukuzaji wa uchumi ambao ni takribani mara 12 kutoka uchumi sasa.
Amesema hilo linawezekana ikiwa taasisi za fedha zitaweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mitaji, hasa kwa wajasiriamali wadogo na kuweka uhusiano mzuri na wadau mbalimbali.
“Kuna haja kila mdau katika sekta ya fedha kuweka uhusiano chanya na wadau ili kuhakikisha mitaji, hasa midogo inapatikiana kwa urahisi kwani kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja takribani mara 12 kwa miaka 25 lazima juhudi ziwepo,” amesema.
Dk Swai amesema Dira 2050 imejitofautisha na ililiyopita ya 2025 katika eneo la ushirikishaji jamii, kwani imeandaliwa kwa kutumia wadau mbalimbali katika sekta za umma, binafsi na wataalamu. Vilevile, imepitia bungeni jambo ambalo halikufanyika siku za nyuma.
“Dira hii ni yetu sisi na tumejiwekea malengo wenyewe, hivyo ili kutimiza malengo yake ni lazima tufanye kazi ya ziada kwa kutumia fursa zilizopo kama vile madini, mbuga za wanyama, sekta ya utalii na usafirishaji hasa kupitia fursa za SGR (reli ya kisasa) ambayo tunaweza kuipanua zaidi,” amesema.
Hata hivyo, Dk Swai ametahadharisha juu ya changamoto za teknojia duni, uhaba wa mitaji na ujuzi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, huku akiweka wazi kuwa uhamasishaji jamii, ubunifu, kufanya kazi kwa bidii na uandaaji makongamano ya kuchochea fikra kuntu kunaweza kusaidia kuepuka changamoto hizo na kufikia malengo ya dira.
Mchumi na mwanasiasa mkongwe nchini, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X muda mfupi baada ya dira kuzinduliwa jana Julai 17, alisisitiza umuhimu wa kujenga umoja, mshikamano na kuondoa ubaguzi katika Taifa ili kutekeleza malengo yalioyomo.
“Leo (Julai 17) inazinduliwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Shabaha ya dira ni kuwa na Pato la Taifa la Dola trilioni moja za Marekani ambapo pato la mtu mmoja liwe wastani wa Dola 7,000 (Sh18.2 milioni) kwa mwaka kutoka Dola 1,200 (Sh3.1 milioni) za sasa. Hii maana yake ni kuwa uchumi wetu (GDP) unapaswa kukua mara 13,’’ amendika Zitto.
Katika kujenga umoja na mshikamano Zitto amesema: “Inawezekana, lakini katika Taifa lililo na mshikamano, lisilo na ubaguzi na lenye demokrasia. Msingi wa hayo ni haki.”
Amesema kazi kubwa inapaswa kufanywa kwa nidhamu ya hali ya juu kufikia shabaha hiyo, akionya kuwa Taifa lenye jamii ya “uchawa” haliwezi kuwa na nidhamu ya kufikia malengo tajwa.
Dira 2050 ilizunduliwa jana Julai 17 baada ya kupitia hatua mbalimbali za uandaaji wake ambao tofauti na zilizopita iliandaliwa kwa ushirikishaji wadau katika makundi mbalimbali. Baadaye ilifikishwa bungeni ambako wabunge walipitisha azimio kuipitisha.