Wagonjwa wanaozunguka mitaani kuomba msaada wa matibabu sasa kutibiwa bure

Mwanza. Wagonjwa waliokuwa wakilazimika kuzurura mitaani kuomba msaada wa matibabu sasa wanatarajiwa kupata huduma hizo moja kwa moja bila ya kuombaomba, kufuatia mpango mpya ulioanzishwa na shirika lisilo la kiserikali la Pearable Good Samaritan Tanzania Organization (PGS).

Mpango huo unalenga kuwafikia na kuwahudumia watu wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya, hasa wale wasio na uwezo wa kifedha.

Akizungumza leo, Julai 18, 2025, katika ofisi za shirika hilo zilizopo Nundu, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Mkurugenzi wa Operesheni wa shirika hilo, Josephat Swai, amsema kuwa kwa muda mrefu baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakilazimika kuzunguka mitaani kuomba msaada wa kifedha ili kugharamia matibabu yao, jambo linaloonesha hitaji la haraka la msaada wa kiafya kwa watu hao.

“Ni hali ya kusikitisha kuona wagonjwa wakilazimika kuombaomba ili wapate matibabu. Kupitia mpango huu, tunalenga kuwafikia moja kwa moja na kuwasaidia kupata huduma muhimu za afya bila kuhangaika mitaani,” alisema Swai.

Alibainisha kuwa shirika hilo limejipanga kushirikiana na vituo vya afya pamoja na wadau wa sekta ya afya kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi.

“Tupo kwa ajili ya kutoa usaidizi wa gharama za mahitaji za kimatibabu, tumefanya utafiti wa kina tumeona Watanzania wengi wenye changamoto hiyo lakini hawajui watapata vipi usaidizi, mfano kuna watu wanaugua wanapata maradhi jambo linalopelekea kukata tamaa ya maisha na kutelekezwa na ndugu zao,” amesema.

Katika hatua hiyo, Swai amesema PGS imekuja na suluhisho kwa kuwasaka mtaani wagonjwa wenye uhitaji ili kusaidia katika kugharamia matibabu yao.

“Mfano kuna wale wenye uhitaji wameshindwa kumudu gharama za mahitaji kukabili changamoto za kiafya, pili wapo wenye uhitaji wa vifaa bandia na miguu, tupo kuwezesha kwa kuungana na Watanzania wenzetu kwa ajili ya kusaidiana,” amesema.

Amesema katika kufanikisha msaada huo, jamii inahitajika kuungana na shirika hilo ili kufanikisha malengo ya kuwasaidia watu wanaoteseka na magonjwa yanayohitaji gharama kubwa.

“Nia na dhamira yetu ni njema sababu wapo watu wanarudisha ndoto zao nyuma, maradhi yanawafanya wakate tamaa ya maisha na kusababisha familia zao ziparanganyike wakihofia kufiliskika, tunaomba Watanzania mtupokee ili tuweze kushikana pale penye shida na uhitaji,” amesema.

Aidha, Swai ameonya juu ya tabia ya baadhi ya wagonjwa wanaotumia ugonjwa wao kama fursa ya kujipatia kipato na kuacha kushughulikia matibabu yao.

“Jambo hilo pia limekuwa likileta fursa kwa baadhi ya Watanzania wenye maradhi kuchukua kama sehemu ya wao kujipatia kipato, unakuta mtu ana fomu anachangisha, akipatiwa kiasi cha fedha anakosa uaminifu wa kufika katika vituo vya afya na kuweza kutatua changamoto hiyo,” ameongeza.

Kwa upande wake, John Francisco ambaye ni mlemavu wa macho amesema licha ya misaada inayotolewa bado wanapitia michakato mirefu kupata misaada hali inayopelekea kukimbilia mtaani hasa wakiambiwa na madaktari ukweli wa ugonjwa huo kuwa hautibiki.

“Kutokana na hiyo hali mtu akishaambiwa na daktari hakuna suluhisho na bahati mbaya mtu huyo hakusoma sasa anashindwa afanye nini badala yake inamlazimu afanye mchakato wa kutafuta mradi wa kuzunguka mtaani mbali na makazi ya watu wanaomfahamu kwa sababu ya aibu ili apate mtaji, sasa nifanye nini nile pumba,” amesema.

Hata hivyo, mkazi mwingine wa jiji hilo, Shirima Daudi amesimulia jinsi alivyompoteza ndugu yake aliyepata ajali na kuanza kuzunguka mtaani kutafuta msaada lakini hakufanikiwa.

“Hakuna mtu anaweza kukusaidia bure lazima uwe na asilimia ili uweze kusaidiwa ilishatokea mimi ndugu yangu alipata ajali tukawa tunafanya michango, cheti  cha madeni kilikuja milioni tatu lakini mungu si athumani mungu akasema msihangaike huyu mtu tumpumzishe lakini bado deni tulilipa,” ameelezea Shirima.

Ameongeza kuwa mgojwa huyo alikaa hospital takriban miezi tisa bila msaada wowote hadi wakaamua kutoka na kwenda mtaani kutafuta msaada.

“ilifikia hatua haponi kabisa mpaka alikatwa nyama za makalio kuongezewa kwenye magoti maana alisagikasagika mpaka sasa ikafikia hatua tukaingia mtaani kutafuta elfu mbili,mia mbili miatatu na tulizoea,” ameongezea.