Wananchi wasisitizwa kuwatumia wasaidizi wa kisheria kupata haki zao

Unguja. Wananchi kisiwani hapa wametakiwa kutumia misaada wa kisheria inayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuzijua haki zao na kutatua migogoro kwa njia ya amani inapojitokeza.

Hayo yameelezwa leo Alhamis Julai 17, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Amour Yussuf Mmanga katika Bonanza la mbio za Ngalawa lililofanyika Fumba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema, wananchi wengi wanakumbwa na changamoto za kisheria lakini hawatambui watumie nji ipi katika kutafuta haki zao jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi zao na kupoteza haki zao za msingi.

“Uwepo wa msaada wa kisheria utawezesha wananchi kuelewa haki zao na kutatua migogoro yao kwa njia ya amani hivyo natoa wito kwa wananchi waliokumbwa na changamoto za kisheria kuwatumia wasaidizi wa kisheria waliopo katika maeneo yao kupata msaada,” amesema Mmanga. 

Mmanga ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali za mitaa ili huduma za msaada wa kisheria ziwafikie wananchi kwa haraka zaidi. 

Amesema atahakikisha kuwa anawakutanisha wadau hao na wananchi wake ili kila mmoja afurahie matunda ya uwepo wao katika jamii.

 Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Hanifa Ramadhan Said amesema kuwa lengo la Wiki hiyo ni kuwaunganisha watoa huduma wa kisheria na wananchi ili kupata nafasi ya kueleza changamoto zao na kusaidiwa kwa njia ya kisheria.

“Wasaidizi wa sheria wako karibu na jamii na wanasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika ngazi ya jamii, hata kwa wale wasioweza kumudu gharama za huduma za kisheria tunawasaidia kupata haki zao,” amesema Hanifa

Bakari Omar Hamad kutoka kituo cha huduma za kisheria (LSF), amesema uwepo wa wasaidizi wa sheria ni nguzo muhimu ya maendeleo kwa kuwa unasaidia wananchi kudai haki zao kwa misingi ya amani na usawa.

Amesisitiza kuwa, dhamira ya LSF kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kupatikana kwa wote. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema kupitia elimu ya sheria, wananchi wanajengewa uwezo wa kutatua migogoro yao kwa njia ya amani na kuepuka michafuko.

“Watoa msaada wa kisheria ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanajua haki zao, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, na wanatatua migogoro kwa njia ya sheria badala ya vurugu,” amesema Haroun. 

Amesema katika wiki hiyo shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika zikilenga kuwafikia watu walio katika mazingira magumu wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu. 

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inahakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wote bila ubaguzi na hadi kufikia watoa msaada 283 wamewafikia wananchi zaidi ya 422,000 na kusikiliza malalamiko ya wananchi zaidi ya 400, yakiwemo masuala ya mirathi, stahiki za kazi, ardhi na ndoa.