Lindi. Jumla ya wavuvi 427, wakiwemo askari kutoka Jeshi la Magereza, wamekabidhiwa boti kumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Boti hizo, ambazo ni mikopo kutoka halmashauri, zimetolewa kwa watu binafsi, vikundi vya wavuvi pamoja na taasisi za Serikali na za binafsi.
Jumla ya wanufaika 427 wamepata boti hizo zenye thamani ya Sh1.3 bilioni 1.3.
Ukopeshaji wa boti hizo umelenga kuwawezesha kuachana na uvuvi haramu, kuongeza uzalishaji wa samaki na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi boti hizo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi Wilaya ya Kilwa, Juma Omari, amesema kuwa vifaa hivyo vipya vitasaidia kupunguza changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli za uvuvi.
“Awali tulikuwa tunatumia boti zisizo na uwezo wa kwenda baharini mbali (maji marefu), jambo ambalo lilitulazimu kuvua kwenye maeneo ya karibu ambayo mara nyingi samaki wake hawajakomaa,” amesema Omari.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa boti hizo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni hatua kubwa ya maendeleo kwa sekta ya uvuvi katika mikoa hiyo, na kwamba zitachangia kuongeza tija, kulinda mazingira ya bahari na kuimarisha maisha ya wavuvi.
“Tumekuwa tukifukuzwa sana baharini wakati tukiwa tunavua, kwani tulikuwa tunatumia uvuvi ambao hautakiwi na Serikali kutokana na vifaa duni tunavyotumia na huwezi kwenda kuvua kwenye maji makubwa, tunaishukuru Wizara kwa kuweza kutupatia boti kwa mkopo wa bei nafuu,” amesema.
Aidha wavuvi hao waliweza kushirikishwa katika uombaji wa mikopo hiyo ya boti kwa kuona matangazo kupitia katika halmshauri zao na kwenye tovuti za Wizara.
Katika hatua nyingine Katibu mkuu Wizara ya mifugo na uvuvi, Agness Meena amewataka wakurugenzi na watendaji kwenda kuwasimamia wavuvi waliokabidhiwa boti hizo kuzitumia vizuri na kurejesha marejesho kwa wakati, kwani itasaidia kuongeza chachu ya maendeleo katika sekta ya uvuvi.
Pia amewataka wavuvi kuacha mara moja kutumia uvuvi haramu, kwani unasababisha kupotea kwa samaki na hauwezi kuleta tija kwa Taifa.
“Niwaombe wakurugenzi na watendaji wa halmshauri kwenda kusimamia urejeshwaji wa mikopo kwa usahihi ilikuweza kuwapatia na wengine wanaohitaji boti za kisasa katika uvuvi.
“Serikali inatumia fedha nyingi katika kulinda rasilimali za bahari na mazao yake, ili kuweza kudhibiti uvuvi haramu Wizara imeanza kutumia teknolojia na vifaa vya kuthibiti uvuvi haramu, ikiwemo ndege nyuki kwa upande wa maziwa makuu napia ndege nyuki hizo zitatumika kwenye ukanda wa bahari,” amesema.
Amesema pia boti za kisasa zimekuwa zikichangia ongezeko la samaki kutoka tani 387,542 zenye thamani ya Sh1.74 trilioni mwaka 2017/2018 hadi tani 529,668.1 zenye thamani ya Sh4.5 trilioni mwaka 2024/2025.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mradi wa boti, Profesa Mohamed Shehe amesema kuwa boti hizo zimetolewa kwa watu binafsi, vikundi pamoja na taasisi za Serikali na binafsi ambapo jumla ya wanufaika 427 wamepata boti hizo zenye thamani ya Sh.1.3 bilioni.
“Boti hizi ni za kisasa na zimekamilika kila kitu tumezitoa kwa wanufaika 427, wakiwemo Jeshi la Magereza ambapo boti hizo zote zinathamani ya Sh1.3 bilioni,” amesema Profesa Shehe.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Lindi, Vitalis Linuma amesema kuwa mkoa huo una jumla ya wavuvi 11,639 na leseni za uvuvi 4,810 ambapo amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni mkoa kutokuwa na boti imara ya kufanya doria ili kuweza kukabiliana na uvuvi haramu
Pia, amesema kuwa ukame wa mabadiliko ya hali ya hewa na gharama za ukubwa wa upatikanaji wa chakula cha samaki, unarudisha nyuma ukuaji wa samaki na pia changamoto nyingine ni kutopatikana kwa mbegu bora za viranga vya samaki imekuwa ikisababisha kutozalisha samaki kwa wingi.
“Changamoto zinazotukabili kama Mkoa wa Lindi zimekuwa zikisababisha kutozalishwa samaki wengi, tunaiomba Wizara kutusaidia upatikanaji wa chakula cha ruzuku kwa bei nafuu, kutusaidia kutupatia boti yenye uhakika katika kukabiliana na uvuvi haramu,” amesema Linuma.
Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza, Ahmed Mwendadi ameahidi kwenda kuzitumia boti hizo ipasavyo na kurejesha mikopo kwa wakati.
“Nina imani kuwa boti hizi zitakwenda kutumiwa ipasavyo kwani wafungwa ndio watakwenda kuzifanyia kazi na pindi watakapomaliza vifungo vyao, wataweza kupata ajira katika Jeshi la Magereza,” amesema Naibu Kamishna wa Magereza Mwendadi.