Unguja. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema maonyesho ya elimu ya juu yanapunguza urasimu kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na elimu ya juu kwani wanapata taarifa sahihi kupitia maonyesho hayo.
Amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakishindwa kujiunga na vyuo vikuu sio tu kwa sababu ya changamoto za kifedha, bali kutopata taarifa sahihi na kuchoshwa na mizunguko ya kufuatilia taratibu za kujiunga.
Lela ametoa kauli hiyo leo Julai 18, 2025 wakati akifungua maonyesho ya sita ya elimu ya juu yaliyofanyika Unguja, Zanzibar ambapo amewataka wazazi na wanafunzi kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi kupata taarifa mbalimbali za kujiunga na vyuo.
Amesema taasisi zote zinazohusika na vyuo vikuu zinapatikana katika maonyesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja, Zanzibar.
“Uzuri wa maonyesho haya tunakutana wote ambao tunahusika na kuwaunga wanafunzi vyuo vikuu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa vyuo vikuu na mamlaka zote ambazo zinasajili programu za masomo, huu ndio muda mwafaka wa kukutana na kutatua changamoto ambazo zinakuwapo na kuwakwamisha wanafunzi,” amesema.
Mbali ya kuwasajili wanafunzi, lakini amewasihi watendaji wakuu kwamba huu ndiyo muda wa kuzungumza zile changamoto zinazokuwa zinawakabili na hilo litasaidia kupunguza gharama za mizunguko.
Waziri Lela amesema ni vema wakuu wa taasisi na vyuo hivyo, na wenye dhamana ya elimu katika wizara kuhakikisha miongozo na taratibu za kielimu ambazo zipo kwa sasa zinatekelezwa asilimia 100 hususani wakati huu wa udahili.
Amesema katika kipindi hiki ambacho wazazi na wanafunzi wanatafuta fursa ya kujiunga na vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, ni wakati mwafaka kuwawezesha vijana kufahamu fursa za masomo zinazotolewa na nchi mbalimbali na kupata uelewa, kujua vigezo wanavyotakiwa kuwa navyo wanapotaka kujiunga na elimu ya juu.
“Wazazi, walezi, muda ndio huu, waje hapa kuonana na mamlaka ambazo zitawapa taarifa za ukweli na uhakika kuhusiana na mustakabali wa elimu na wanafunzi watapata ushauri wa fani gani ambazo kwa sasa ni vipaumbele kwa Serikali, taifa na dunia kwa ujumla,” amesema.
Hatua hiyo inarahisisha na kupunguza muda kusafiri kwenda mikoa mbalimbali kuuliza vyuo programu zake na mawakala ambao wamesajiliwa kutoa huduma nje wapo, kwa hiyo mambo yote yanafanyika katika eneo moja.
Meneja wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactivet) Zanzibar, Elitha Mbedule amesema wanatoa huduma zote za taasisi zinapatikana hapo na wanapokea wadau ambao wengi ni wa vyuo vya kati vinavyotoa astashahada na stashahada.
“Wengi wanaokuja ni wale wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu ambapo kwa utaratibu wetu, mhitimu lazima apate namba ya utambuzi wa tuzo (AVN), tunawaelekeza kwa kutumia simu zao wanaomba kwa kupitia mfumo, tunawaelekeza na kuingia kwenye mfumo na vyuo vikuu vipo hapa, wanakwenda kwenye chuo wanachokitaka,” amesema Mbedule.
Amesema wamejikita kutoa huduma kupitia teknolojia, hivyo wanataka huduma nyingi wadau wazipate wenyewe kupitia mifumo anatakiwa atambue kuwa yupo kwenye chuo halali.
Amesema elimu wanayoisimamia ni ile inampa mhitimu ujuzi wa kufanya kazi, kwa hiyo tunasisitiza sana hata katika kuandaa mitaala ijikite kuhakikisha wanapatikana watu wenye ujuzi wa kufanya kazi.
Kaimu Meneja wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, Philbert Temba amesema wanawasaidia wanafunzi ambao hawana uwezo wa kujilipia na kwa sasa wameshuka hadi ngazi ya stashahada.
“Pia, katika maonyesho haya tupo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi ambao tayari wameanza kuomba mikopo ila wanashindwa, pia, tupo na mtu wa anwani (Napa), changamoto kubwa ilikuwa ni kupata anwani za makazi ili kuwarahisishia anawasaidia wanafunzi kupata anwani zao,” amesema.