Yanga yatumia mbinu za kimafia, yamshusha Conte

ILE vita ya kuwania kiungo Moussa Bala Conte kutoka Guinea, imeisha baada ya Yanga kumtambulisha rasmi leo mchana ikiizidi kete Simba iliyoanza mapema kumtamani mchezaji huyo.

Iko hivi. Simba ndio walikuwa wa kwanza kumshawishi kiungo huyo wa CS Sfaxien ya Tunisia, kisha wakazungumza na kukubaliana mambo ya msingi bila kumsainisha.

Yanga ikaingilia kati dili kwa kufanya mazungumzo na kukubaliana lakini baadaye wakaenda pia kwa klabu anayoichezea yaani Sfaxien.

Klabu hizo mbili zikagongana kwa uongozi wa timu hiyo, kisha kuanza kuvutana kununua mkataba wa mwaka mmoja ambao Conte aliubakiza na klabu yake hiyo.

Hata hivyo, habari zilisema Yanga ilishamalizana na Sfaxien kwa kulipa dau ambalo lilikubalika na Waarabu hao kisha ikapewa ruhusa ya kumalizana na mchezaji.

Akili ambayo Yanga iliitumia ikatuma mkataba wa awali ambao Conte alikubaliana nao na Sfaxien hawakuchelewa wakatuma hadi hati ya uhamisho wa mchezaji wa kimataifa (ITC) ambayo tayari ipo ndani ya majengo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pale Karume.

Wakati huo Simba ilikuwa inaendelea kumtumia kipa anayeitumikia timu hiyo, Moussa Camara kumshawishi kiungo huyo asikubali kumalizana na Yanga kwa kuwa kwao ndiyo sehemu salama.

Kama haitoshi Simba kupitia kocha Fadlu Davids akafanikiwa kuzungumza na kiungo huyo akimwambia kwamba yeye ndio anamtaka na anajua wapi anakwenda kucheza.

Simu hiyo ya Fadlu zikadaiwa zilizidi kumtia ugumu Conte kukubaliana na Yanga akionyesha kukerwa na Sfaxien hatua ya wao kumalizana na mabingwa wa Tanzania wakati hawakuwa wamekubaliana naye.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Conte alishawishika na mazungumzo yake na Fadlu akiona uhakika wa nafasi yake hatua ambayo Yanga ilikuwa inakwama kufanikisha hilo kwa kuwa hawakuwa na kocha bado zaidi ya kiungo huyo kuzungumza na mabosi wa juu wa timu hiyo.

Yanga kuona utata huo, ikamsafirisha Rais wa klabu hiyo, Injini Hersi Said na kwena bosi mmoja kwenda Guinea aliko Conte na kumalizana naye  na kukubali kusaini mkataba wa miaka mitatu na jana ikamtambulisha mchana.

Kutua kwa Conte kunafungua milango ya Khalid Aucho kuondoka klabu kama tulivyoripoti jana kwamba ameomba kwenda Israel aliko ‘swahiba’ wake, Kennedy Musonda.

Lakini kunazidi kumweka pabaya Clatous Chama kuendelea kubaki kikosini kwa kanuni ya nyota wa kigeni, kwani tayari Yanga imeshasajili nyota wengine wawili wa kigeni, akiwamo mshambuliaji Celestin Ecua na kiungo mshambuliaji Mohamed Doumbia. Kanuni inaruhusu kila timu kuwa wageni wasiozidi 12.