Bangi ilivyo fupa gumu Tanzania

Dar es Salaam. Ripoti ya Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2024 imeonyesha bangi bado inaongoza kutumika zaidi duniani, takribani watu milioni 228 waliitumia mwaka 2022.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia nne ya watu wote duniani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 28 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Amerika ya Kaskazini imeendelea kuwa kinara wa matumizi ya bangi, huku asilimia 19.8 ya watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 waligundulika kuitumia mwaka 2022.

Ripoti hiyo pia imebainisha matumizi ya bangi miongoni mwa vijana, yameendelea kuwa changamoto duniani, likiwepo Bara la Afrika.

Ripoti inaeleza matumizi na biashara haramu ya bangi vimeendelea kushamiri barani Afrika, huku waathirika wengi wakiwa vijana walio chini ya umri wa miaka 35.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini Tanzania mwaka 2024, tani 2,303.2 za bangi sawa na kilo 2,303,195.86 zilikamatwa zikihusisha watuhumiwa 7,981. Kati ya hao wanaume ni 7,475 na wanawake 506.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) inaonyesha kiwango hicho ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo linalochangiwa na kuimarika kwa operesheni za ukamataji na ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa.

Kwa upande wa dawa za kulevya za mashambani, bangi imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa kukamatwa zaidi, ikifuatiwa na mirungi.

Mamlaka imeripoti kukamata shehena ya bangi tani 2,307.37, kati ya hizo tani 2,303.2 ni bangi ya ndani, huku tani 4.17 zikiwa ni skanka, bangi yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC, iliyoingizwa kutoka baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika.

Taarifa inaonyesha kiwango cha skanka kilichokamatwa mwaka 2024 kimeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali inayoonyesha mafanikio ya juhudi za Serikali kudhibiti biashara hiyo haramu.

Mwaka 2023 zilikamatwa kilo 423.54, wakati mwaka 2024 zilikamatwa kilo 4,168.89 za skanka sawa na tani 4.17 zikihusisha watuhumiwa 48. Kati ya hao wanaume ni 38 na wanawake 10.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema bangi ni tatizo kubwa kutokana na kushamiri kwa mashamba ya zao hilo nchini.

Amesema kwa muda mrefu nguvu kubwa iliwekwa katika kukamata bangi iliyosindikwa na kuvutwa vijiweni, ilhali nyingine bado inaendelea kulimwa na sasa mikoa yote ina mashamba ya bangi.

“Tumebaini karibu mikoa yote ina mashamba ya bangi, ndiyo maana tumeweka nguvu kuhakikisha tunayafikia mashamba yote. Awali bangi ilikuwa inalimwa zaidi Arusha na Mara, lakini katika uchunguzi wetu tumebaini mikoa mingine yenye mashamba ya bangi na tunayatekeza,” amesema na kuongeza:

“Mikoa kama Ruvuma haikuwa na historia hiyo lakini tulifanya operesheni tukakuta kuna mashamba makubwa ya bangi, hivi karibuni tumeteketeza ekari 90. Hata Dar es Salaam inaweza isiwe na mashamba ila watu wanaotesha miche ya bangi. Tunaendelea na jitihada hizi ili kumaliza kabisa kilimo cha bangi na si kusubiri hadi ifike mtaani.”

Amesema biashara ya bangi kama ilivyo kwa aina nyingine za dawa za kulevya inaambatana na rushwa ndiyo sababu inaendelea kuwepo.

“Tunajua bangi haiwezi kutoka shambani hadi ikasafirishwa bila kuwapo mtandao unaofanikisha hilo, tumeungana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashughulikia watumishi na watendaji wote watakaoruhusu bangi kupita kwenye maeneo yao,” amesema.

Amesema wapo waliochukuliwa hatua kuanzia wakulima, wafanyabiashara na hata watumishi wa mamlaka za Serikali.

“Iko wazi, ukikutwa na bangi kuanzia kilo 20 ni kosa la uhujumu uchumi ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 au kifungo cha maisha jela,” amesema.

Mkurugenzi wa Shirika la New Vision of Life Society linalotoa elimu ya kupambana na dawa za kulevya kwa vijana, Khamis Shuweri amesema upatikanaji wa bangi ni rahisi kuliko ilivyo kwa dawa nyingine za kulevya, ndiyo maana inaendelea kuwa kikwazo kwenye vita dhidi ya dawa hizo haramu.

Amesema licha ya jitihada zinazofanywa na mamlaka mbalimbali kukabiliana na matumizi ya bangi, dawa hizo bado zinalimwa nchini na wanaojihusisha na kilimo hicho wanapata fedha nyingi ndiyo maana imekuwa ngumu kukikomesha.

“Umaskini unawafanya wakimbilie porini wakalime bangi, hawajali wanachokifanya kinaweza kuleta athari gani kwa jamii kwa wakati huo wanafikiria masilahi yao tu. Kuna namna kilimo cha bangi kinaonekana kuwa rahisi ikilinganishwa na mazao mengine,” amesema.

Amesema suala hilo linapaswa kuliangalia kwa umakini na Serikali na isichoke kufanya doria kwenye mapori ili kuondoa uwezekano wa watu kwenda kujificha huko na kulima bangi.

Vilevile iondoe vikwazo kwenye mazao mengine ikiwemo tozo, ushuru ili watu wahamasike kufanya kilimo kingine.

Kauli hiyo inashabihiana na kilichoelezwa na DCEA baada ya operesheni katika vijiji vinane vya Wilaya ya Tarime iliyobaini kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani, ambao huwapa mitaji wakulima wa Tarime kisha bangi ikishakomaa huvunwa na kusafirishwa kwenda kuuzwa huko.

Operesheni hiyo iliwezesha kukamatwa kilo 7,832.5 za bangi kavu, kilo 452 za mbegu za bangi na ekari 3,007.5 za mashamba ya bangi kuteketezwa, huku wakulima 17 wakikamatwa.

Watuhumiwa baada ya kuhojiwa walieleza namna wanavyofadhiliwa kuendeleza kilimo hicho kisha kusafirisha mavuno kuuzwa nchi jirani.

Kamishna Jenerali Lyimo alieleza raia hao wa nchi jirani wanafadhili gharama za kilimo ikiwamo fedha za mbegu, kupalilia, kuvuna na vibarua ambao kwa siku hulipwa ujira wa Sh10,000.

“Kinachofanyika ni kwamba hawa wakulima wamevamia eneo la hifadhi ya bonde la Mto Mara na wamejimilikisha, hivyo wanaingia makubaliano na hao raia wa nchi jirani wanawapa fedha za kugharamia kilimo halafu wakishavuna wanaweka bangi kwenye magunia ikiwa mbichi na nyingine inachakatwa,” amesema.

Kwa upande wake, Shuweri aliyewahi kuathiriwa na bangi amesema vijana wengi wanaingia kwenye matumizi kwa kufuata mkumbo, huku akidai baadi ya wasanii wanachangia jambo hilo.

“Siku hizi bangi imekuwa haigopwi, vijana wanaitumia kwa kufuata mkumbo, tunakutana na vijana unamuuliza aliingiaje anakwambia aliona mwenzake anavuta na yeye akaanza kuvuta. Wasanii pia wanachangia hili kwa kiasi kikubwa wanavyoonyesha picha zinazoashiria matumizi ya bangi na utajiri wao, kuna namna watoto wanawaiga bila kujali wala kujua athari zake,” amesema.

Daktari wa magonjwa ya akili, Firmina Scarion amesema bangi ikitumiwa kupita kiasi huamsha mfumo wa ubongo, hali inayosababisha kubadilika kwa tabia na kumbukumbu, hivyo mtumiaji kuhisi raha iliyopitiliza.

“Matatizo yanayowakuta vijana wa namna hii ni pamoja na kujihusisha kwenye vitendo vya kamari, wizi na vingine vya kujipatia pesa ili waendelee kununua na kutumia bangi. Wanaweza pia kusababisha magonjwa mengine ya akilii kama vile kuwa na wasiwasi uliopitiliza,” amesema.

Katika mahojiano aliyowahi kufanya na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga, Wallace Karata pia alizungumzia hali hiyo, akisema matumizi ya bangi hubadilisha utendaji kazi wa ubongo na kumfanya mtumiaji awe tofauti.

“Kuna magonjwa ya akili ambayo yamejificha, inawezekana mtoto kwenye familia yake kuna ugonjwa wa akili wa kurithi, sasa akitumia bangi anaenda kuyaamsha… hiyo skanka madhara yake ni makubwa na yanatokea kwa haraka zaidi

“Mtu anaweza kuona maruweruwe, kusikia sauti zinazomhamasisha kufanya chochote, kama ni mtoto anajiona mkubwa na mwenye nguvu. Uwezekano wa akili ya mtumiaji kuchanganyikiwa ni mkubwa.”

Dk Karata alibainisha kuwa bangi inapotumiwa na mtoto au kijana inaathiri uwezo wake wa kufikiri na kuharibu mfumo wa kumbukumbu.