CCM yaahirisha vikao vya kitaifa, yaeleza sababu

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuahirisha vikao vyake vya kitaifa vilivyopaswa kufanyika tarehe 18 hadi 19 Julai 2025 kutokana na sababu za kiufundi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, Julai 18, 2025, kufuatia barua ya awali iliyotumwa Julai 11, 2025, ikielekeza maandalizi ya vikao hivyo ambavyo vilihusisha Kamati ya Usalama na Maadili pamoja na Kamati Kuu ya chama hicho tawala.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tarehe mpya ya kufanyika kwa vikao hivyo itatangazwa baadaye. Chama pia kimeomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na mabadiliko hayo ya ratiba.

“Vikao vya CCM vya kitaifa vilivyopangwa kufanyika tarehe 18–19 Julai 2025 sasa vimeahirishwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza kutokana na hatua hiyo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kuahirishwa kwa vikao hivyo kunakuja wakati ambapo chama hicho kipo katika kipindi muhimu cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za kisiasa na kiutawala kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.