Chaumma yatoa fomu kwa wagombea ubunge Kilimanjaro

Moshi. Chama cha ukombozi wa umma (Chaumma), Mkoa wa Kilimanjaro kimezindua shughuli ya uchukuaji wa fomu wa nafasi za ubunge na madiwani katika mkoa huo, huku watiania katika majimbo saba kati ya tisa wakichukua fomu hizo za ubunge.

Waliochukua fomu za  ubunge ni Gervas Mgonja, Jimbo la Same Magharibi, Grace Kiwelu (Vunjo),  Michael Kilawila (Moshi Vijijini), Patric Assenga (Moshi Mjini), Hendry Kileo (Mwanga), Allan Mmanyi (Same Mashariki) na Andrea Oisso (Rombo).

Zoezi hilo pia limetanguliwa na ufunguzi wa ofisi mpya katika eneo la Majengo, lililopo Manispaa ya Moshi, Mkoani hapa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uchukuaji wa fomu za ubunge na madiwani, Mwenyekiti wa Chaumma Mkoa wa Kilimanjaro, Gervas Mgonja amesema chama hicho kinakwena historia mpya ya matumaini kwa wananchi wa mkoa huo na kuwa sehemu ya mapambano ya kisiasa kupitia chama hicho makini.

“Chaumma si chama cha siasa tu, ni harakati ya kweli ya ukombozi wa siasa na kiuchumi kwa wananachi wa kawaida, uzinduzi wa zoezi hili la kugawa fomu kwa wagombea ni hatua muhimu ya kuandaa viongozi wa kesho, wanaojali utu, haki, uwazi na Maendeleo ya wananchi,” amesema Mgonja.

“Hamkuja kutafuta madaraka, mmeitwa kutumika, mmeamua kusimama kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania waliokata tamaa, msiwe sehemu ya siasa za matusi, chuki au rushwa, kuweni mfano wa siasa safi, siasa ya kujenga sio ya kubomoa,”amasema Mgonja

Amesema “Leo nimesimama mbele yenu sio kwa sababu ya siasa za kawaida bali kwa sababu ya maumivu ya wananchi wa Kilimanjaro, vijana waliomaliza shule na kukosa ajira, wakulima waliopoteza matumaini na wazazi walioshuhudia watoto wao wakikosa huduma bora za afya na elimu.”Mgonja

 Watia nia wa ubunge Chaumma wafunguka

Akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Vunjo, Grace Kiwelu amesema anaamini bado wanavunjo wanamuhitaji na  anaamini uchaguzi ukiwa huru na wa haki atakuwa mwakilishi sahihi wa ubunge katika jimbo hilo atakayeweza kuwasemea changamoto zao.

“Imefika leo 2025 nimebadilisha tu gari kutoka Chadema na kuingia Chaumma naamini haki inadaiwa haiombwi, gari inapoharibika unapanda gari jingine kwa hiyo nimeingia kwenye gari ya Chaumma kuendelea kulipigania Jimbo la Vunjo, Vunjo wananijua nimefanya nao kazi miaka ya nyuma sio Mgeni kwao,” amasema Kiwelu.

Ameongeza”Naamini bado wananihitaji kuwa mwakilishi wao ndani ya Bunge ndio maana leo nimechukua fomu na nina hakika uchaguzi huu ukiwa huru na haki wanavunjo watapata mwakilishi sahihi ambaye ndiye Mimi.”

Mtia nia Jimbo la Mwanga, Hendry Kileo, amasema Jimbo hilo lina rasilimali nyingi za kiuchumi na kwamba bado hazijafanyiwa kazi vya kutosha.

“Jimbo la Mwanga lipo nyuma kiuchumi, ukiangalia linaziwa jipe, bwawa la nyumba ya Mungu lakini ardhi yenyewe haijawahi kutumiwa vizuri, nitahakikisha naisimamia serikali vizuri na kuhakikisha huduma zote zinazopaswa kuwepo kama kwenye maeneo mengine zinakuwepo,”amasema Kileo.

“Kitu ambacho pekee amekiacha Mzee Msuya ni Wilaya ya Mwanga kuwa ya kwanza kuwa na umeme, lakini nitahakikisha naibadilisha Mwanga iwe Wilaya ambayo kila mmoja anatamani kuishi,”amasema Kileo.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu amesema, “Mtu akipiga kura hakuna kwenda nyumbani inategemea hayo maeneo wananchi watakuwa na utayari kiasi gani, lakini wananchi hawarudi nyumbani wakipiga kura lazima kura zilindwe.”

Naye, mtia nia Jimbo la Moshi mjini, Patrick Assenga amasema wananchi wanahitaji mabadiliko katika nchi hii na kwamba kwenye uchaguzi wa mwaka huu hawataingia kinyonge.

“Nchi yetu wananchi wanahitaji mabadiliko, Jimbo Moshi mjini ni la upinzani kwa miaka mingi sana mwaka 2020 Jimbo hili liliporwa na CCM, nataka kurejesha Halmashauri mikononi mwa upinzani tena, na safari hii itakuwa chini ya Chaumma, hatuendi bungeni kugonga meza, naenda kwasababu tuna changamoto nyingi za wananchi,”amesema Assenga.

“Naamini wananachi wa Moshi mjini watatuachagua maana naamini ndio chama pekee cha upinzani kilichobakia kama matumaini yao, hatutaingia kwenye uchaguzi huu kinyonge wala kizembe, hatutapoteza uchaguzi huu kama tulivyofanyiwa huko nyuma,”amasema Assenga.

Amasema, “Tukishapiga kura hatutaondoka kama tulivyofanya miaka minne, tutabaki vituoni kulinda kura, wanaume kwa vijana wote tutabaki kuhakikisha Mbunge na madiwani wanatangazwa na hatutanii katika hili.”

Mtia nia wa ubunge Jimbo la Rombo, Andrea Oisso amasema katika Jimbo hilo lenye rasilimali nyingi wananchi hawakupaswa kuishi maisha ya kimaskini kutokana na utajiri uliopo wilayani humo.

“Rombo ni jimbo ambalo wananchi wake walitakiwa kuwa na maisha bora kutoka na uhalisia wa jimbo lenyewe, rasilimali ardhi na watu wake, naamini kwamba naweza kuwa mtu sahihi kupigania maslahi ya watu wa Rombo,” amasema Oisso.