Coastal yashtuka, yasimamisha usajili | Mwanaspoti

WAKATI klabu nyingine zikiendelea kuchangamkia mchakato wa usajili, Coastal Union imeshtukia kitu, imeamua kwanza kuanza na msako wa kocha kabla ya kuanza kushusha mastaa wapya.

Wagosi hao walimaliza msimu katika nafasi ya nane kwa kukusanya pointi 35, wakishinda mechi nane, sare 11 na kupoteza 11.

Taarifa za ndani ya klabu hiyo zililiambia Mwanaspoti kuwa, bado viongozi wa kikosi hicho wanapambana kuafikiana na kocha kwanza ili atakapofika amalizie usajili uliosalia.

“Tunamalizia makubaliano na kocha kwanza, hatuoni ni sawa kufanya usajili wakati kocha hayupo, anaweza kuja akawa na mapendekezo tofauti na kile tulichofanya, tutakuwa tumejitengenezea msingi wa anguko,” alisema kigogo huyo na kuongeza; “Kocha akifika ndio tutashirikiana naye kufanya usajili na ukimalizika tutaanza maandalizi ya msimu mpya, hivyo tunaamini tutakuwa na timu bora itakayokuwa tofauti na msimu uliopita.”

Awali, Mwanaspoti liliandika mipango ya klabu hiyo ni kutaka kumchukua kocha Anicet Kiazayidi Makiadi kutokana na uwezo wake aliouonyesha alipokuwa Tabora United.

Huku wakati huo huo, Dodoma Jiji pia imeingia sokoni kuwania saini yake baada ya kocha wa kikosi hicho Mecky Mexime kumalizana na mabosi hao. Timu hiyo ilimaliza msimu na kocha Joseph Lazaro anayedaiwa kubanwa na kanuni kwa leseni aliyonayo kuwa kocha mkuu, hivyo kushindwa kumbakisha.

“Ni wazi kuwa kocha Lazaro, anaijua timu hiyo kuanzia msimu uliopita na hata mpaka sasa, ila leseni yake ndio hairuhusu kuongoza kikosi kinachoshiriki Ligi Kuu, nje na hapo yuko vizuri,” kilisema chanzo hicho.