HATIMILIKI 15,597 ZA KIMILA ZATOLEWA MKOANI KIGOM

……………

Na Ester Maile Dodoma 

Utoaji hatimiliki za ardhi katika mkoa wa Kigoma  umeongezeka kutoka 4,432 mwaka 2020 hadi 13,886 mwaka 2025, utoaji  hati miliki za kimila pia  umeongezeka kutoka 1370 hadi 15,597. 

Hayo yamebainishwa na mkuu wa Mkoa huo IGP Mstaafu Balozi Saimon Nyakoro  Sirro hii leo 19 Julai 2025  jijini Dodoma, wakati wa  mkutano wake na waandishi wa habari akizungumzia mafanikio ya mkoa huo kwa  kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita. 

Aidha vijiji vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi vimeongezeka kutoka vijiji 95 hadi vijiji 170 na migogoro ya ardhi 167 na mingine ikiendelea kutatuliwa kuendana na taratibu zilizowekwa kiserikali.

 Hata hivyo Utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na Watu Wenye Ulemavu umeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.96 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 6.40 mwaka 2025. Aidha, kaya masikini (walengwa wa TASAF)  imepungua kutoka kaya 112,887 hadi kaya 108,609.

Ameeleza kuwa Mkoa unaendelea na ukamilishaji wa ukarabati wa Meli ya MT SANGARA ambayo inatumika kubeba shehena ya mafuta kiasi cha lita 410,000 katika ziwa Tanganyika ambao umefikia asilimia 99, pia utekelezaji wa ukarabati wa meli kongwe ya MV Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo ambao umefikia asilimia 15 unaendelea. 

 Vile vile amesema Mkoa unaendelea na ujenzi wa stendi ya mabasi ya Kakonko ambao umefikia asilimia 85 kwa gharama ya shilingi milioni 351.44 , unaendelea na ujenzi wa vibanda 15 vya nyongeza soko la Mpakani Muhange wenye gharama ya shilingi milioni 81.45 na ujenzi wa vibanda 34 vya biashara katika Soko Kuu la Kakonko Mjini ambao umefikia asilimia 93 kwa gharama ya shilingi milioni 368.34 .