Dar es Salaam. Siku moja nilikwenda benki kuchukua mshiko. Nilikuwa katika hekaheka za kulipa madeni na kutimiza miradi yangu ya maendeleo. Nilidamka nikimwacha Bi. Mlevi kitandani, nikatinga mavazi ya mazoezi na kutoka.
Huyu mama ana mipango mingi sana, hivyo angeijua safari yangu angenijaza mapendekezo yake ambayo yangevuruga dira na sera zangu. Nikasema moyoni: “Aliyelala usimwamshe”. Potelea mbali kama alinichungulia kwa jicho moja, kwa mavazi haya ataelewa kuwa nimo mbioni kuepukana na maradhi yasiyoambukiza.
Muda niliofika benki ulikuwa rafiki sana. Sikukuta msururu, hivyo nilirudi nyumbani mapema nikiwa na kitita kinono. Nikakichimbia kwenye kabrasha la mafaili yangu kwa nia ya kumficha, kisha nikaendelea na harakati zingine. Nilitengeneza mpangokazi wangu kwa siku mbili, siku ya tatu nikafanya ukaguzi wa ghafla kwenye kabrasha kabla ya kuanza utekelezaji. Hapo ndipo nilipopigwa na butwaa.
Nilikuta mfuko umechanwa vipande vipande na kitita changu kimevurugwa katika kila kona. Uchunguzi wangu wa awali ulibainisha bila shaka yoyote kuwa panya alihusika na uhaini huo. Mzigo ulikuwa umesiginwa kwa vitu vyenye ncha kali kwenye kona zake, na aliacha ushahidi wa kinyesi chake kwenye eneo la tukio. Nilimlaani sana mdudu huyo kwani alikula namba za pande zote mbili. Hakufikiria hata kuniachia nusu hasara.
Niliwahi kuzungumzia panya katika siku zilizopita. Huyu mdudu (nikimwita mnyama nitakuwa namheshimu) ana akili sana, na anajua anachokifanya. Kuna bwana mmoja aliyeitwa kwenye usaili alikuta cheti chake kimesiginwa. Msiginaji alijua kumkomoa maana alilenga pale kwenye sahihi na muhuri. Jamaa alitangaza vita kuu dhidi ya panya hata akaua wadudu wengine wasio na hatia.
Mwingine alilazimika kufunga ndoa kanisani akiwa amevalia suti iliyompwaya, halafu njiwa. Wakati wa maandalizi alijibana hadi akaweza kununua suti iliyomkaa vema. Akaikunja vizuri kabatini kusubiri tukio hilo muhimu. Siku ya tukio alipokwenda kuikunjua, alikuta mtaalamu panya keshafanya yake. Alilitoboa koti kifuani na suruali magotini, sehemu zisizofichika machoni mwa wadaku.
Kwa kuwa tukio mubashara halina marudio, jamaa alilazimika kupiga simu kwa rafiki zake kuomba msaada. Lakini siku ya kufa nyani miti yote huteleza, wale aliolingana nao kwa wajihi hawakuwa hewani. Mwisho wakati akielekea kuchelewa alimpata binamu yake aliyeoa siku zile zile. Tofauti yao ni kwamba mfadhili alikuwa mfupi na mnene, wakati mhanga ni mwembamba na mrefu. Ilikuwa komedi tosha.
Pamoja na ukorofi wake, panya anabaki kuwa mwalimu mzuri katika ulaji. Wakati binadamu anakoboa mahindi kupata unga wa sembe, hajui kwamba anaondoa kiini cha hindi ambacho ndicho chenye virutubisho vyote. Panya anapoingia ghalani anakula viini vyote na kukuachia makapi yasiyo na faida. Hata mezani, panya hali chipsi wala ubwabwa, yeye anachagua dona la kauzu ama samaki.
Ameona nini hadi akaacha chipsi yai na kuangukia kwenye dona kauzu? Panya hasikilizii ladha kama tunavyofanya sisi wanadamu. Yeye hujua ubora wa chakula kutokana na harufu yake asilia. Wakati watoto wetu wanahangaika na harufu za ziada zinazouzwa madukani, yeye huzingatia uhalisia. Pale utakapotayarisha chakula bora na halisi ndipo utakapomwona panya akihangaika.
Kwenye akili ya chakula namfananisha panya na mwanasiasa. Huyu anajua kunusa mafanikio zaidi yetu. Hivi majuzi nimeshangaa kuona wanachama 4,000 wa chama tawala wakitia nia ya kuwa wabunge wetu. Lakini kama ninavyosema, wanasiasa wanajua kunusa. Sisi wengine tunaona matatizo yetu yametushinda ya watu hatuyawezi, lakini wanasiasa wanaomba kushughulika na matatizo yetu. Ama kweli usimwamshe aliyelala!
Kugombea ubunge ni haki ya kila anayekidhi vigezo. Lakini sanjari na hilo, kuzijadili siasa vilevile ni haki ya kila mtu. Lakini kuna mtazamo kuwa watiania wanakimbilia chama tawala kwa sababu ya kutegemea mteremko. Hoja hii inaakisi kile kilichotokea 2020 ambapo chama hicho kilipata ushindi mkubwa wenye utata katika ngazi zote za udiwani, ubunge na uwakilishi.
Lakini pia inaakisi unene wa mafao ya wabunge. Mishahara ukijumlisha posho za vikao, za nyumba na usafiri zinavutia sana machoni na masikioni. Hata mafao ya kustaafu yana rangi inayomvutia mtu yeyote. Ukizingatia hali halisi ya huku mtaani, unaweza kuchukua uamuzi bila ya kufikiria mara mbili. Acha wanaomwaga machozi, sitashangaa mgombea anayetetea jimbo akijinyonga pale atakapoliwa kichwa na wajumbe.
We huogopi mtu anavyojing’atua kwenye nafasi ya Mkuu wa Mkoa kwenda kubahatisha ubunge! Kwa uhalisia Mkuu wa Mkoa hawezi kufananishwa na Mbunge, kwani yeye ndiye Rais wa wananchi wote mkoani mwake. Mbunge ni mwakilishi tu wa wananchi hao. Lakini mwanasiasa analitazama hilo kwenye ‘engo’ ingine, kama panya anavyolitazama dona la kutowezwa na kauzu chukuchuku.
Hivi tunavyoongea uchumi wa Dodoma umeporomoka mara baada ya Bunge kuvunjwa. Biashara haiendi kwani walishazoea kuuza mabanda kwa mabanda ya kuku wa kuchoma kila siku, sasa hawana wa kumuuzia. Mjasiriamali wa Dodoma anafanana na mbunge, kwani kama hela anazo. Bunge likizinduliwa na yeye yupo Dodoma, likivunjwa yupo Dar es Salaam. Ukikaa na muuza uzuri utanukia marashi. Sio mnakaa na “wasukuma chemba”.