MSHAMBULIAJI huru Anuary Jabir, imeziingiza vitani timu tatu kuwania saini yake kwa ajili ya msimu ujao ambazo ni Namungo, Dodoma Jiji na Mbeya City kati ya hizo itakayokuwa na ofa nono itafanikiwa kupata huduma yake.
Jabir msimu uliyoisha alikuwa na Mtibwa Sugar iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu 2025/26, kiwango alichokionyesha kimezivutia timu hizo kuhitaji huduma yake.
Chanzo kutoka Dodoma Jiji kilisema: “Tupo katika mazungumzo na Jabir endapo kama tutamsainisha atakuwa amerejea nyumbani, ila kwa sasa hatuwezi kusema kila kitu kipo tayari kabla ya kusaini mkataba.”
Kwa upande wa kiongozi mmoja wa City ambaye hakutaka kutaja jina lake alikri kuendelea kwa mazungumzo baina yao na Jabir: “Tumempa ofa yetu katuambia tumpe muda kuitafakari, hivyo mambo yakienda sawa huenda akawa sehemu ya kikosi chetu.”
Alipotafutwa Jabir kuthibitisha hilo alisema: “Nazungumza na timu tofauti, kwa sababu sijasaini bado siwezi kusema ni ipi na ipi.”