Kocha mpya Yanga anataka bao tano!

VIONGOZI wa Yanga wamepanga Jumapili hii kuanza msimu mpya kwa kutambulisha benchi jipya la ufundi kisha kutangaza mastaa waliopewa ‘thank you’ na kumalizia wapya waliosajiliwa kabla ya timu kuanza kambi.

Lakini Kocha mpya anayetajwa kumalizana na timu hiyo, Romain Folz amezungumza kitu cha kushtua kwa aina ya soka analofundisha.

Ingawa Yanga wanafanya siri jina lake, lakini Mwanaspoti limepenyezewa kuwa aliyekuwa kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns, Folz, ndiye atakayetangazwa rasmi kama kocha mkuu wa kikosi hicho wikiendi hii.

Folz mwenye umri wa miaka 35 anarudi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia uhamisho huu wa kuelekea kwa vigogo wa Afrika Mashariki waliomaliza msimu wa 2024/25 kwa kutwaa mataji yote ya ndani.

Romain Folz, akiwa msaidizi ndani ya Mamelodi Sundowns alinukuliwa na Gazeti moja la Afrika Kusini akisema; “Kocha Mkuu alinipa jukumu kubwa, hasa upande wa mashambulizi kujaribu kutengeneza mfumo mpya wa kushambulia kwa namna tofauti.”

“Tulijaribu kuwa na mbinu mbalimbali za kupata matokeo. Tulikuwa na matokeo mazuri tuliifunga Arrows 5-0 kwenye Carling Knockout na tukaifunga Chiefs 4-0 kwa hiyo nafikiri tulitumia mbinu sahihi.”

“Lakini naamini ingawa tulifunga mabao mengi, bado tungeweza kufunga zaidi. Tulifanya vizuri lakini bado tulikuwa na nafasi ya kuboresha,” alisisitiza Folz ambaye mwaka jana mwanzoni mwa msimu walitimuliwa yeye na bosi wake licha ya kuwa timu ilikuwa ikipata ushindi.

Mtindo wa uchezaji wa Folz haukudumu. Yeye pamoja na Folz walifutwa kazi baada ya miezi sita tu klabuni hapo.

Sundowns walifika nusu fainali ya MTN8 lakini wakatolewa na Stellenbosch, kisha wakashindwa fainali ya Carling Knockout dhidi ya Magesi FC.

Inaaminika kuwa Rais wa Yanga, Hersi Said, alipata mapendekezo mazuri kuhusu Folz kutoka kwa Mkuu wa Maendeleo ya Soka Duniani wa FIFA, Arsene Wenger, walipokutana kwenye Kombe la Dunia la Klabu la FIFA hivi karibuni.

Vyanzo vya ndani ya klabu vimebainisha, wanatarajia Folz kutambulishwa Jangwani wikiendi hii, ili achukue rasmi mikoba ya Miloud Hamdi ambaye amehamia klabu ya Ismaily inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Folz amemaliza hivi karibuni kazi yake nchini Algeria na klabu ya Olympique Akbou, ambapo aliisaidia timu hiyo inayopambana kutoshuka daraja kubaki salama katika ligi kwa michezo minane ya mwisho wa msimu.

Ameshawahi pia kuzinoa klabu za Township Rollers (Botswana), Marumo Gallants, AmaZulu (Afrika Kusini) na Horoya AC (Guinea). Uhamisho wake kwenda Yanga ni hatua mpya ya kuvutia katika maisha yake ya ukocha.

Folz aliwahi kusema: “Nimefanya kazi na FIFA, ambayo ilikuwa ndoto yangu mara tu nilipoondoka Afrika Kusini. Walikuwa wakinitafuta kwa muda mrefu,” aliiambia iDiski Times.

“Najivunia kuwa sehemu ya taasisi kubwa kama hii. Hii si nafasi yangu ya kwanza; sasa nafanya kazi na mashirikisho ya soka na timu za taifa kusaidia kukuza na kuboresha mchezo wa soka duniani.

“Ninaheshimu sana fursa waliyonipa, na naithamini. Nilikuwa namheshimu Arsene Wenger na nilitamani kuwa sehemu ya mradi wake katika kitengo cha Fifa cha High-Performance.”