Mbunge aliyepata ajali wakati wa usahili wa watiania aruhusiwa

Dar es Salaam. Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane, ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupata ajali iliyosababisha avunjike mguu wakati wa shughuli ya usaili wa wanachama waliotangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.

Ajali hiyo ilitokea Julai 5, baada ya Mbunge huyo kutumbukia kwenye shimo la gereji lililopo katika karakana ya Chuo cha Maendeleo Kilwa Masoko, ambako usaili wa wagombea ubunge na udiwani ulikuwa ukiendelea.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 19, 2025 na Mwananchi Digital, kwa njia ya simu  kuhusu maendeleo yake, Mbunge huyo  amesema anaendelea vizuri na amesharuhusiwa kutoka hospitali.

“Niliruhusiwa kutoka hospitali tangu Julai 15, 2025 na ninashukuru Mungu ninaendelea vizuri kwani kwa sasa kinachoendelea ni kufanya mazoezi na kusafishwa kidonda ambapo madaktari waliniruhusu nifanye hivyo katika hospitali ya karibu na nyumbani,” amesema.

Ndulane ameongeza kuwa kwa hali aliyonayo kwa sasa hata kama itatokea leo wakamtangaza kuwa ni miongoni mwa wagombea watatu walipitishwa anao uwezo wa kwenda jimboni kwenye kupigiwa kura.

Upigaji kura huo ni hatua hiyo ya mwisho za mchakato wa kumpata mgombea wa CCM atakayewakilisha Chama katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.