Mwili wa msichana aliyeuawa na kutelekezwa barabarani watambuliwa

Arusha. Mwili wa msichana aliyepatikana akiwa ameuawa na kutupwa kando ya barabara ya Kambi ya Fisi, jijini Arusha, umetambuliwa na ndugu zake.

Mwili huo ulikutwa ukiwa uchi, na kulingana na taarifa za awali, marehemu alionekana kuwa ametendewa unyama mkubwa ikiwemo kung’olewa macho, kuvunjwa shingo, na kufanyiwa ukatili wa kingono.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa tukio hili la kikatili na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.

Kwa mujibu wa taarifa mwili huo umetambuliwa kwa jina la Neema Ibrahim (22), mkazi wa Mtaa wa Lolovono, Sokoni One jijini Arusha.

Mwili wa Neema ulikutwa Julai 15, 2025, katika Mtaa wa Kambi ya Fisi, ukiwa umetupwa kando ya barabara na ukiwa hauna nguo.

Taarifa za awali kutoka kwa vyombo vya usalama zinaeleza kuwa alifanyiwa unyanyasaji wa kingono kabla ya kuuawa, ambapo alijeruhiwa sehemu zake za siri, kuvunjwa shingo na kutobolewa macho yote mawili na watu wasiojulikana.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambi ya Fisi, Emanuel Olevaroya, amesema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa uchi, na ulikuwa umewekwa kifudifudi kando ya barabara.

Kwa mujibu wa Olevaroya, dalili za awali zilionyesha kuwa marehemu alifanyiwa ukatili kabla ya kutupwa eneo hilo.

Alitoa wito kwa wakazi wa mtaa huo kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo la kusikitisha.

 “Baada ya Tukio hilo mwili wa binti huyo ulichukuliwa na Jeshi la Polisi kabla ya jana Julai 18, 2025 ndugu waliokuwa wanamtafuta na kuukuta mwili  umehifadhiwa katika chumba cha  kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru,” amesema.

Mama mzazi wa Neema amesema kuwa alipata taarifa ya kutokuwepo kwa binti yake nyumbani kwa siku tatu mfululizo, hali iliyowalazimu kuanza msako kwa kumtafuta kwa ndugu, jamaa na majirani, bila mafanikio, hadi walipopata taarifa za kupatikana kwa mwili wake.

“Huyu msichana huwa anaishi na mtoto wake wa miaka mitano na mdogo wake anayesoma kidato cha kwanza ambaye ndiye aliyetupigia simu kuwa dada yake hajarudi siku ya pili nyumbani.

“Baada ya kupata taarifa hizo tulianza msako bila mafanikio kabla ya majirani kushauri kwenda mochwari kunakodaiwa kuna msichana amefariki na mwili kutupwa barabarani.

“Awali, tulikataa kwenda tukidai mtoto wetu hajafa, lakini baada ya mabishano marefu siku ya pili yake (Jana) tuliamua kwenda mochwari na bahati mbaya tukamtambua ni kweli Neema ”amesema mama huyo na kuanza kulia.

Amesema kuwa mara ya mwisho alionekana Jumapili usiku maeneo ya Makao Mapya.

Katika tukio lingine la msichana, Aisha Charles Urio (17) mkazi wa ‘Sokon One’aliyeuawa Julai kisha mwili wake kutelekezwa kwenye nyumba bovu Kata ya Daraja Mbili, umezikwa nyumbani kwao mkoani Singida leo Julai 19, 2025.

Mwili wa Aisha ulikutwa umetupwa katika moja ya nyumba chakavu zilizopo katika Kata ya Daraja Mbili, ukiwa na majeraha ya kuvunjika shingo na mkono.

Aidha, uchunguzi wa awali umeonesha kuwepo kwa michubuko sehemu zake za siri, dalili za kuingiliwa kingono kabla ya kuuawa.

Zuwena Shabani, jirani wa marehemu, alisema kuwa Aisha alikuwa katika harakati za kusafiri kwenda kwa mama yake mzazi baada ya kufukuzwa nyumbani na mke mdogo wa baba yake (mama wa kambo), hali iliyomlazimu kutafuta msaada na makazi mbadala. Ndipo akakumbwa na mkasa huo wa kusikitisha.

 “Tangu juzi Aisha alikuwa anaaga majirani anasema ananyanyasika sana na ametakiwa kuondoka hivyo amewasiliana na mama yake ambaye anaishi Singida na ataondoka kesho yake siku ya Jumatatu.

“Jumatatu asubuhi saa 12 watu wanasema walimuona Aisha na begi kubwa akisafiri, lakini bahati mbaya ndio jana Jumatano tunapata taarifa kuna mwili wa msichana umeokotwa huko Daraja Mbili kwenye moja ya nyumba bovu na walivyoenda kuthibitisha walikuta ni yeye,” amedai.

Amesema kuwa msichana huyo inadaiwa alionekana Jumatatu mchana wakipata chakula na kuzunguka huku na huko na kijana mmoja jirani yao ambaye huwa anapiga debe katika stendi kubwa ya mabasi ya mikoani.

“Baada ya kutokea tukio hilo, kijana anaedaiwa alikuwa naye hakuonekana tena hapa mtaani, wala stendi anakofanya kazi,” amedai.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Long’dong katika Kata ya Sokon One, Amosi Mndolwa amesema mwili wa msichana huyo ulikutwa katika jumba hilo ukiwa na majeraha mbalimbali ikiwemo ya kipigo na kuvunjwa shingo na mkono wake wa kulia.

“Tulipigiwa simu kuna mwili wa mtu anayesadikiwa ni wa mtaani kwangu, tulifika eneo  la tukio na baadhi ya watu kweli walimtambua ni binti wa mtaani kwetu,” amesema.