KIUNGO mshambuliaji Najim Mussa aliyekuwa anaichezea Namungo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, anakaribia kujiunga na Pamba Jiji, baada ya nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kuonekana finyu kwa msimu ujao.
Staa huyo aliyejiunga na Namungo dirisha dogo la Januari 2025, amemaliza mkataba wake wa mkopo na timu hiyo na sasa mabosi wa Pamba wanampigia hesabu kwa ajili ya kumsajili tena, ingawa dili lake pia ni la mkopo wa msimu mzima.
Najim aliyesajiliwa na Singida msimu wa 2024-25, akitokea Tabora United, amekosa nafasi kwa viungo, Emmanuel Keyekeh aliyetoka Samartex ya Ghana, Josaphat Arthur Bada (ASEC Mimosas) na Mohamed Damaro aliyetokea Hafia ya Guinea.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata, zinaeleza mabosi wa Pamba wamewasiliana na uongozi wa Singida kwa ajili ya kuipata saini ya nyota huyo, japo kilichobakia kwa sasa ni chaguo la mchezaji mwenyewe la timu atakayopenda kuchezea msimu ujao. “Uongozi umetupa ruhusa ya kuzungumza naye, lakini kwa sharti la mchezaji mwenyewe kuridhia kwa sababu Singida kwa sasa haina mpango tena wa kumrudisha, inahitaji aendelee kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema kiongozi wa Pamba.
Nyota huyo akiwa na Singida aliichezea mechi mbili tu za Ligi Kuu Bara, jambo lililomfanya kutolewa kwa mkopo Januari 2025, ili kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, ambapo kwa Namungo alicheza na kuonyesha pia makali yake.
Akiwa na Namungo, nyota huyo alichangia bao moja la Ligi Kuu Bara, katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-1, dhidi ya timu ya Fountain Gate, Desemba 25, 2024, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite kwaraa uliopo mjini Babati, Manyara.