Polisi yachunguza mtoto aliyepotea mazingira ya utata Tabora

Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linachunguza tukio la kupotea kwa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu anayeishi na wazazi wake Kata ya Mpela, Manispaa ya Tabora.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Julai 19, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema mtoto huyo amepotea Julai 18, 2025 maeneo ya nyumbani kwao wakati wazazi wake wakihamisha vitu kuhamia katika nyumba nyingine.

Amesema kwa mujibu wa familia mtoto huyo alikimbilia bajaji ya mizigo iliyokuwa ikihamisha vitu na baada ya hapo hakuonekana mpaka hivi sasa.

“Tunaendelea na uchunguzi kubaini mtoto huyu alipo na pia wananchi watupe ushirikiano kwa taarifa au kumuona mtoto huyu ili aweze kupatikana na kuungana na familia yake,” amesema Kamanda Abwao.

Ameongeza kuwa wazazi wake wamehama nyumba huyo wakiwa na katika hali mhemko kwani hawakutarajia kuhama kwa muda huo, hivyo ilikuwa ni kitendo cha ghafla kwao huku wakiwa na hasira kutokana na tofauti za kifamilia.

“Kuhama kwao kwa mujibu wa maelezo yao kumetokana na kuhitilafiana na ndugu yao kwa kuwa nyumba waliyokuwa wakiishi ilikua ya kwake hivyo amewarushia maneno makali ambayo yamewaudhi na kuamua kuhama haraka na hii huenda ndio sababu ya kupoteza umakini,”ameongeza.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Afrah Yusuph alipozungumza na mwandishi jioni ya leo, amesema bado juhudi za kumtafuta zinaendelea kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Amesema taarifa za tukio hilo wametoa katika kituo cha polisi Tabora Mjini hivyo yoyote anaweza kuwasiliana nao kwa njia hiyo au mawasiliano ya simu yanayopatikana mitandaoni.