TANZANIA Prisons imeamua kuvunja benki kumpata kocha mkuu atakayeinoa timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, huku ikisisitiza kuwa presha iliyokutana nayo, haitarajii ijitokeze tena kwa misimu ijayo, huku jina la kocha wa zamani wa timu hiyo, Ahmad Ally aliyekuwa JKT Tanzania akitajwa.
Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja kupitia mechi za ‘playoffs’ ilizoshinda kwa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Fountain Gate, kwa sasa imeanza kusuka upya kikosi kwa kutema na kuongeza wapya.
Hadi sasa makocha waliopo mezani kwa ajili mazungumzo ni Ahamd Ally (JKT Tanzania), Mohamed Abdallah ‘Baresi’ aliyekuwa Mashujaa na Mkenya, Patrick Odhiambo aliyewahi kufundisha hapo misimu miwili nyuma.
Hata hivyo, Mwanaspoti imehakikishiwa kuwa pamoja na majina hayo, lakini maafande hao katika kuonyesha wapo siriazi kutaka mafanikio msimu ujao ni kununua mkataba wa kocha Ally aliyepo JKT Tanzania ili arejee kikosini.
Ally aliyewahi kuinoa Prisons kwa mafanikio msimu wa 2023/24 kabla ya kubebwa na JKT na kuiongoza imalize katika nafasi ya sita msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Bara, sasa Wajelajela hao wameamua kumrejesha kikosini.
Mtendaji Mkuu wa Prisons, John Matei alisema baada ya kuwa na presha kubwa msimu uliopita, wanahitaji mabadiliko makubwa kikosini na kwamba hadi sasa wameunda kamati ya usajili ambayo kwa miaka ya nyuma haikuwapo.
Alisema katika usajili wao, wataachana na wachezaji kadhaa wakiwamo waliomaliza mkataba na ambao ni majeruhi wa muda mrefu.
Pia wataachana na nyota watatu kati ya sita waliokuwapo kwa mkopo.
“Kwanza tunahitaji kocha ambaye ataweza kuendana na falasafa ya timu, tumekuwa na kikao kizuri na viongozi makao makuu na tumeazimia kuwa na kikosi bora cha ushindani,” alisema Matei na kuongeza;
“Ili kuondokana na presha za mara kwa mara, tumeamua kuweka mikakati ikiwamo usajili imara na kufanya maandalizi mapema, yapo majina matatu ya makocha ambao tukifikia mwisho, tutamalizana na mmojawapo.’
Matei aliongeza katika mchakato wa kuisuka timu, kamati ya usajili imewashirikisha makocha wa timu za vijana pamoja viongozi ambao watakuwa pamoja katika kutengeneza Prisons mpya ya 2025/2026.
“Tunatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi huu Julai, au mapema Agosti, lengo ni kumpa nafasi kocha mpya kuweza kutengeneza timu, kimsingi tumejipanga kwa msimu ujao,” alisema Matei.