Kongwa. Ni kipaji, ubunifu na ndoto iliyochomoza katikati ya akili kubwa. Ndiyo, hakuna neno lingine unaloweza kulitumia unapokutana kwa mara ya kwanza au unapomwelezea mtoto Ridhiwani Asheri.
Kwa wiki sasa mtoto huyu amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania baada ya kipande cha video yake kusambaa ikimuonyesha akiwa ametengeneza mji kwa kutumia miti, vipande vya makopo ya plastiki, mbao na vitu vingine ambavyo unaweza kusema ni mabaki au uchafu.
Ila kwa ustadi mkubwa mabaki hayo yameonyesha taswira ya mji, tena wa kisasa. Kwenye eneo pembeni mwa nyumba yao chini ya miti, ndipo Ridhiwan amejenga miji yake iliyopangiliwa vizuri, ikionyesha madaraja, majengo marefu na madogo, barabara za juu na chini. Pia inaonyesha uwepo wa viwanja, shule na masoko. Katika eneo hilo kuna miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Morogoro na mingine.

Ubunifu wa mtoto Ridhiwani Asheri alioufanya wa kutengeneza miji na barabata kwa kutumia vipande vya miti na mabaki ya plastiki.
Video hiyo iliwashangaza wengi, baadhi wakihoji kipaji na ubunifu wa mtoto Ridhawan na kuanza kuuliza mahali anapopatikana.
Hata hivyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alishachukua hatua kuhakikisha Ridhiwan anafikiwa kwa haraka na kusaidiwa kutimiza ndoto yake ya kuwa mtaalamu wa mipango miji.
Hatua ya kwanza ambayo Ulega ameichukua ni kuwatuma maofisa wa Wizara ya Ujenzi kumtembelea Ridhiwan na kuzungumza na wazazi wake.
Mwananchi pia lilifunga safari kwenda Mtaa wa Sakosi uliopo Mji Mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, ndani ya nyumba ndogo yenye uzio wa miti, kukiwa na migomba michache.
Hii ni nyumba ya Martin Asheri na Vumilia Ndagala. Wawili hawa ndio wazazi wa Ridhiwan ambaye amejipambanua kwa kuonyesha kipaji kikubwa.
Neno la kwanza la Ridhiwan mwenye miaka 13 baada ya kukutana na mwandishi wa Mwananchi, Hebel Chidawali na maofisa wa Wizara ya Ujenzi baada ya salamu lilikuwa:
“Yaani natamani niwe msomi na mtu mkubwa ili nijenge barabara nzuri zitakazopunguza ajali, lakini natamani niwe na uwezo wa kuwaambia wasijenge barabara wakati mvua zinanyesha.”
Katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani anakoishi kijana huyu, yalionyesha namna alivyo na uwezo mkubwa, hasa katika kujibu maswali kwa kile anachokiamini na kukisimamia.

Mtoto Ridhiwani Asheri akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa Mwananchi.
Kwa umri ni kijana mdogo, umbo lake pia halisadifu umri huo kwani anaonekana ni wa miaka chini ya anayotaja kuwa nayo, lakini akili yake inamuinua na kuhisi huenda ana mingi zaidi ya hapo.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Mwananchi na Ridhiwan.
Swali: Ridhiwan hiki ulichokifanya hapa ni kitu gani?
Jibu: Hapa nimetengeneza barabara za mijini na vijijini, nimejenga madaraja makubwa na madogo ambayo yanasaidia maji yasiharibu barabara na kusababisha ajali.
Swali: Nani alikufundisha kazi hii?
Jibu: Huwa naangalia kwenye video wanapotoa taarifa za habari, sasa nikiamka asubuhi nami nawaza kama ningejenga hivyo au zaidi maana kuna maeneo naona wamejenga madaraja madogo halafu maji ni mengi.
Swali: Kuangalia kwenye runinga pekee halafu unakuja kuchora chini au unatazama ukiwa na kalamu na karatasi?
Jibu: Hapana, huwa naangalia halafu natamani sana, sijawahi kuwa na kalamu wala karatasi, hivyo nikija hapa nabuni kwangu kuwe kuzuri zaidi.
Huku akionyesha namna alivyopanga kazi yake na jinsi anavyotamani iwe, anaonyesha matamanio ya ujenzi wa madaraja yanayotakiwa kupeleka maji kwenye maeneo ya mabonde akitaka maji hayo pia yatumike kufuga samaki na vijana kuogelea.
Swali: Baada ya maelezo yako, unaweza kunionyesha jinsi miji yako ilivyopangwa?
Jibu: Ndiyo, hii barabara imetoka Dar es Salaam kupitia Morogoro kuja Dodoma, huku Dar nimeweka soko la Kariakoo na Mtaa wa Msimbazi, unaona watu wengi hapa.
Kingine nimeweka Mtaa Sumbawanga, Uwanja wa Mkapa na hapa pembeni kuna uwanja mdogo wa michezo huwa nausikia lakini hapa niliweka taa wakazivunja watoto.
Swali: Humu umeweka vigari vidogo vya kuchezea je, huwa unavipata wapi?
Jibu: Mimi nikipata Sh50O au Sh1,000 kutoka kwa mama sinunui kitu kingine zaidi ya gari, humu sichezei ila nimeweka mfano wa jinsi zinavyotakiwa kupishana zikiwa barabarani.
Swali: Je, kuna faida gani unapata kwa kazi hii?
Jibu: Napata faida ya kufurahia nikiwa peke yangu lakini inanisaidia, mama akiniachia mji hapa nakuwa sisinzii maana muda wote inabidi nifanye kazi zangu hapahapa.
Swali: Zipi changamoto kwenye kazi yako?
Jibu: Changamoto ndiyo nini (anaelezwa) zipo nyingi, kwanza mama huwa anabomoa kazi zangu na wakati mwingine watoto wanaiba vigari vyangu ila sikati tamaa na pengine nakosa pesa za kununua simenti (saruji) ya kujengea inabidi niende kuomba kwa wanaojenga majumba.
Swali: Mbali na kazi hii unapenda nini kingine?
Jibu: Napenda mpira na huwa naangalia wanapocheza timu kubwa (hata hivyo anasema hana ushabiki wa timu).
Swali: Vipi kuhusu shule?
Jibu: Sisomi maana nilifeli darasa la nne sasa namwambia mama anihamishe hataki mimi wananirudisha nianze kusoma na wadogo zangu sipendi.
Vumilia mama mzazi wa Ridhiwan anamtaja kuwa mwenye kipaji ambacho walianza kukigundua akiwa na miaka minne tu.

Mtoto Ridhiwani Asheri akionyesha moja ya ubunifu wake alioufanya wa kutengeneza miji na barabata kwa kutumia vipande vya miti na mabaki ya plastiki.
“Shida ya huyu ni kigugumizi ndiyo maana hata kwenye kujifunza wanachelewa kumuelewa mapema, lakini hizi kazi zake humwambii kitu na kwa namna yoyote akimaliza kazi aliyotumwa lazima umkute hapo,” anasema.
Anasema Ridhiwan ni mtoto wake wa sita na ndiye wa mwisho.
Anae leza kuhusu maisha yake akisema yana upekee ukilinganisha na wenzake, huku akiwa na ndugu zake huwa mkimya zaidi lakini akipanga hoja inakuwa na mashiko.
Vumilia anasema hakuna mtu amewahi kumuona akimwelekeza kufanya jambo lolote kwenye michoro yake na wakati mwingine anachoshuhudia ni jinsi anavyokusanya makopo na vifuniko vya chupa za maji na soda kisha anaumba umbo la namna yoyote ambalo kwake analiona kuwa na faida, lakini pengine anakaa mbali kidogo akilitazama huwa analibomoa na kuumba vinginevyo.
“Mwanzoni nilikuwa navunja haya madude yake, lakini ulifika wakati nikaona yana faida kwani sipati kazi kumtafuta zaidi ya kumkuta akipanga vitu vyake na hata mimi nimeanza kuona ajabu maana nikikaa naye jioni anasimulia mambo hayohayo licha ya kaka na dada zake kutokumuunga mkono,” anasema.
Kwa mujibu wa mama huyo, zaidi ya mara mbili kijana wake akiwa mdogo wa miaka 10 kulikuwa na ujenzi wa barabara jirani na eneo la Kibaigwa alikwenda huko akiwa anawatazama wajenzi kwa muda mrefu hadi watu wakaanza kuhisi amechanganyikiwa na wakamrudisha nyumbani. Hata hivyo anasema siku iliyofuata alianza kujenga daraja kama alilolikuta ingawa yeye alijenga likiwa na midomo mitatu na siyo miwili kama walivyojenga wao.
Akizungumzia masomo, anakiri Ridhiwan angepaswa kuwa darasa la sita lakini alishindwa kwenye mtihani wa darasa la nne na aliporudishwa kuanza na watu wa chini yake aliamua kugoma kwa madai hawezai kuendelea kusoma na wadogo zake, akaomba abadilishiwe shule jambo lililowashinda wanafamilia kutokana na uwezo mdogo walionao.
Amesema iwapo atajitokeza mtu wa kumwendeleza itakuwa nafuu kwake, Kati ya watoto wake yupo mmoja aliyefaulu kidato cha nne akapangiwa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini lakini alisoma muhula mmoja kisha wakashindwa kumlipia hivyo hakuendelea na masomo.
Hata hivyo, anatoa angalizo katika kujifunza kwa kijana wake, waangalie kigugumizi alichonacho kwani wakimwendea haraka hawawezi kumtambua kuhusu uwezo wake.
Yona Mlilima ndiye alimuanika Ridhiwan kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuona kitu alichotengeneza hakikuwa cha kawaida licha ya kuwa alikwenda nyumbani kwao kwa lengo la kusikia kilio cha mama mzazi wa kijana alipotaka aende gereji.
“Huyu mama yake ni ndugu yangu, alikuja akaniomba nimchukue mwanaye ili niwe nashinda naye gereji ambako mimi nafanya kazi, kweli nilimwambia kijana ni mdogo anatakiwa akasome kwanza ndipo nikaona nije kujua kwa nini amechagua kuja kwenye machuma,” anasema.
Yona anasema alipofika hapo akakutana na kitu ambacho hakutarajia kwa umri wa kijana kama huyo, ndipo akapiga picha na kuirusha kwenye mitandano ya kijamii, huku akijua kama ingeweza kuwafikia watu wengi zaidi.
Akizungumza baada ya kujionea hali halisi nyumbani kwa kina Ridhiwan, Katibu wa Waziri, Mhandisi Aman Mdekha, amesema baada ya Waziri Ulega kuona video hiyo aliwaagiza kufika nyumbani kwa kijana huyo.
Amesema Julai 18, 2025 walianza safari kwenda Kibaigwa kukutana na familia yake kwa ajili ya kuzungumza na wazazi wake kuona njia sahihi ya kutimiza ndoto ya mtoto huyo.
“Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ndiye alianza kuona video ya huyu mtoto mitandaoni, akaelekeza atafutwe baada ya kushangazwa na kuvutiwa na ubunifu wake. Tumetekeleza hilo na tumeshazungumza. Hatua zaidi zitafuata baada ya kupata maelekezo mengine kutoka kwa Waziri,” amesema.