Siku ya kulia, kucheka CCM

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeingia katika hatua ya mchujo wa mwisho wa majina ya watia nia ya kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani, ambapo leo Jumamosi Julai 19, 2025, ndoto za baadhi ya wagombea zitafikia tamati huku wengine wakipiga hatua kuelekea kwenye kinyang’anyiro kikuu.

Ni siku ya maamuzi, ambapo Kamati Kuu, inatarajiwa kuweka hadharani majina matatu ya kila nafasi yatakayopigiwa kura za maoni, hatua ambayo kwa wengi ni chanzo cha kilio, na kwa wachache ni kicheko cha ushindi wa awali.

Kikao cha kamati kuu kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, kinafanyika baada ya kukamilika kwa kikao cha sekretarieti kilichoanza Julai 14, kikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Kwa sababu ya kikao hicho cha sekretarieti, baadhi ya wajumbe akiwemo Dk Nchimbi, hawakuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 jijini Dodoma Julai 17.

Sekretarieti ilikuwa na jukumu la kuchambua majina ya watiania waliopendekezwa na kamati za siasa za kata, wilaya na mikoa na kupendekeza kwa kamati kuu, nani na nani warudishwe kwa wajumbe.

Katika baadhi ya majimbo, watiania waliojitosa wanafikia 20 hadi 30, wakiwania kuingia tatu bora kabla ya kupigiwa kura za maoni kupata mmoja wa kugombea.

Miongoni mwa walojitosa kwenye kinyang’anyiro hicho ni wabunge wanaomaliza muda wao, mawaziri wa zamani kwenye serikali za awamu ya nne iliyokuwa chini ya Jakaya Kikwete na awamu ya hayati John Magufuli.

Mchuano ni mkali kwa baadhi ya majimbo ambako kuna majina ya vigogo wanaochuana endapo kamati kuu itawarejesha kwenye kura za maoni.

Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu, wameiambia Mwananchi kuwa majina ya makada watatu kwenye kila jimbo na kata, yatajulikana baada ya kukamilika kikao cha kamati kuu na yatasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mchujo huo utateua makada watatu kwenye kila jimbo, sawa takriban waombaji 800 kati ya 4,109 waliotia nia katika majimbo 272 Tanzania Bara na Zanzibar.

Pia watia nia 30,000 wa udiwani wanasubiri hatima yao kwenye kata 3,960 ambako majina takriban 11,880 yanatarajiwa kurejeshwa mikononi mwa wajumbe.

Wasiwasi unaongezeka kutokana na tetesi zinazoendelea katika mitandao ya kijamii, zikidai baadhi ya wanasiasa wakongwe wametemwa, suala ambalo Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amelifafanua akisema “hakuna aliyekatwa”.

Ukiacha tetesi za kukatwa, yapo madai ya baadhi ya wagombea kucheza rafu kushinikiza ushindi, kama ilivyowahi kuelezwa na Khamis Mbeto, katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar.

Mbeto alisema wapo watia nia wanaochafuana, wengine wanaandaa wagombea vivuli akionya kuwa vikao hivyo vya juu, pamoja na mambo mengine vitayapitia yote hayo.

Hayo yakiendelea, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mikoa mbalimbali nayo imekaa mguu sawa kuhakikisha inadhibiti na kuwatia nguvuni watia nia wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Miongoni mwa maeneo ambayo Takukuru inayaangazia ni mawakala wa fedha mitandaoni, ambao wanaelezwa wanatumiwa na wanasiasa kufikisha fedha kwa wajumbe, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za uchaguzi.

Kupitishwa kwa majina hayo, kunafungua pazia la kuanza kwa mchakamchaka wa watia nia hao kupita kila kata kukutana na wajumbe kuomba kura za maoni.

Njia watakazopita watia nia wa ubunge, ndizo hizo hizo watakazopita wa udiwani kwa kuwa wote watapigiwa kura kwenye mikutano mikuu ya jimbo/kata inayoundwa na wenyeviti, makatibu na wajumbe wa kamati za utekelezaji na siasa za CCM za matawi na kata.

Kipindi hicho kitakuwa na joto la aina yake kisiasa hasa ukizingatia baadhi ya watia nia majina yao hayataakuwa yamekurudi, hivyo kuwepo uwezekano wa watakaokubaliana na uamuzi wa vikao vya juu, na watakaopinga kwa njia mbalimbali.

Kwa kawaida, kipindi hicho pamoja na kufuatilia mienendo ya watia nia, chama hicho pia aghalabu hukitumia kutibu majeraha na kuepusha mpasuko unaoweza kusababishwa na hasira ya baadhi ya makada kukatwa wakati wa mchakato.

Akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wajumbe wa kamati kuu ya CCM, amesema kwa utaratibu wao, majina hayo yanasomwa hadharani mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho.

“Yanasomwa na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii, kisha yatawasilishwa kwa mamlaka za chini za chama kwa ajili ya kuwapokea watia nia sambamba na ratiba ya kwenda kujitambulisha kata kwa kata ianze,” amesema.

Amesema watia nia hao watakaowekwa hadharani, ndio watakaopigiwa kura za maoni na mmoja kati yao, atapitishwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya ama ya ubunge, uwakilishi au udiwani, kulingana na alivyoomba.

Mjumbe mwingine wa kikao hicho (jina pia linahifadhiwa), amesema ni viongozi ndio watakaoamua utaratibu wa kuyaweka hadharani majina ya watiania hao, lakini kwa muda uliobaki bila shaka yatasomwa baada ya kikao.

“Ratiba imewekwa wazi na muda ni mchache sana, sioni kama kutakuwa na delay (ucheleweshaji), pale yatakapopatikana yatatajwa na mwenezi, taratibu nyingine zitafuata,” ameeleza.

Alipoulizwa iwapo ni vitu gani vinavyozingatiwa wakati wa kupitisha majina hayo matatu, amesema ni miiko ya uanachama, kukubalika ndani na nje ya chama, historia nzuri, maadili na mapendekezo ya vikao vya chini.

“Inawezekana vikao vya kata, wilaya na mikoa havijakupendekeza, lakini sekretarieti ilikuona unafaa kwa sifa, unashangaa jina lako linakwenda kamati kuu na linapita. Kwa hiyo ni mchezo usiotabirika,” amesema.

Mmoja wa watiania wa ubunge kutoka mkoa wa Arusha anasema: “Kwa kweli presha inapanda, inashuka. Kwa sababu sijui kama jina langu litarudi. Hapa tunazidisha maombi tu hasa ikizingatiwa mchakato umekuwa wenye usiri sana,” amesema mtia nia huyo ambaye anadai kwenye kamati za siasa za wilaya na mkoa alipenya.

Mwingine ambaye anagombea ubunge kutoka moja ya jimbo la Mkoa wa Mwanza amesema kwa taarifa za vyanzo vyake jina lake lilipita vizuri kamati ya siasa wilaya, lakini mkoa halikuwa vizuri.

“Sasa hapa, sijui huko juu waliniona, ndio nasikilizia hapa. Unajua chama kikubwa hiki, kinapokea taarifa mbalimbali na zingine tulichafuana tu, sasa chama kinapekua faili lako nje, ndani. Kwa kweli wacha siku ifike tujua nani ni nani,” anasema mtia nia huyo ambaye anapigania kurudi tena bungeni.

Wakati mambo yakiwa hivyo, Januari 18-19, 2025 katika mkutano mkuu wa CCM, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengi aligusia mchakato wa kuwapata wagombea akitaka haki itendeke.

“Anayefaa aambiwe anafaa, asiyefaa aambiwe huyu ana kasoro mbili, tatu kwamba hatufai kwa huko mbele tunapokwenda. Tukitoa mwanya, tukapitisha kwa wanaposema na mimi niwemo tuwaweke kando, hakuna kuoneana aibu au haya,” alisema Rais Samia.

Aidha, Aprili 24, 2025 akiwa jijini Dodoma katika Wilaya ya Kongwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Stephen Wasira aliahidi chama hicho kupeleka kwenye uchaguzi wagombea kwa kuwasikiliza wananchi ili wapate mtu anayekubalika na wote.

“CCM safari hii hatutaki kujichosha, hatutaki kubeba mizigo kama umepakia kwenye mkokoteni halafu unasukuma, hatutaki. Mnasema mtu fulani mitano tena, je anakubalika lakini uamuzi wa mwisho ni wajumbe,” alisema Wasira.

Alisema chama hicho kinahitaji kushinda uchaguzi kwa kishindo na ili kifanikiwe ni lazima kipate makada wanaokubalika kwa wananchi hata akisimama wote wanasema mwenzao.