Simba yafuata kiungo Mali | Mwanaspoti

KATIKA kuimarisha eneo la kiungo, Simba imeanza harakati mapema za kulijenga eneo hilo ambalo tayari kuna nyota wanne wameshaondoka baada ya msimu wa 2024-2025 kumalizika.

Katika hilo, klabu hiyo haijakubali unyonge, kwani mabosi wa Simba wako kwenye mazungumzo na Stade Malien ya Mali, ikimtaka Lassine Kouma.

Kouma ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, Simba inapambana kunasa saini yake kwenda kuboresha eneo hilo kwa ajili ya msimu ujao.

Hata hivyo, Simba italazimika kumalizana na klabu yake kwanza kutokana na kiungo huyo bado ana mkataba wa miaka miwili na Stade Mallien ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Mali.

Msimu uliomalizika, Kouma amehusika kwenye jumla ya mabao 16, akifunga saba na kuasisti mara tisa akihesabika kuwa kiungo aliyefanya vizuri nchini humo.

“Tumetafutwa na klabu ya Simba, wanamtaka Kouma, tunaendelea na mazungumzo nao, hawataki taarifa zao zisambae, kwahiyo siwezi kukwambia zaidi,” amesema bosi mmoja wa idara ya ufundi ndani ya Stade Malien

Endapo mazungumzo hayo yataendelea vizuri, kuna uwezekano Simba ikamtuma mmoja wa mabosi wake kwenda kumalizana na klabu yake.

Katika kuboresha kikosi, Simba tayari imeshatema wachezaji nane, wakiwemo viungo wanne ambao ni Fabrice Ngoma aliyemaliza mkataba, Augustine Okejepha na Debora Mavambo waliofikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Omary Omary aliyepelekwa Mashukaa kwa mkopo. Wengine ni mabeki watatu Valentine Nouma na Kelvin Kijili waliofikia makubaliano ya pande mbili na Hussein Kazi aliyemaliza mkataba. Pia kipa Aishi Manula aliyemaliza mkataba.