Siri nyuma ya mchujo wa CCM kusogezwa

Dodoma/Dar. Mambo ni mengi na muda ni mfupi kwenye ulingo wa siasa za Tanzania kwa sasa. Ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) presha kwa makada waliotia nia kuwania uteuzi wa kugombea uwakilishi na ubunge imeendelea kupanda na kushuka.

Julai 19, 2025 CCM imetangaza kuahirisha kikao cha uteuzi wa wagombea hao ikieleza watiania waliojitokeza ni wengi.

Hata hivyo, baadhi ya wabobezi wa masuala ya siasa waliozungumza na Mwananchi, wamesema huenda ahirisho hilo liko ni nje ya sababu zilizotajwa, hata kama na zenyewe zinachangia.

Wamesema upo uwezekano likawa linatokana na kauli za wazi na minyukano ya ndani kwa ndani ya makada wa chama hicho.

Habari za ndani zinadai mchuano wa makundi yenye nguvu ndani ya CCM umepamba moto, kila upande ukipambana watiania wanaotoka makundi hayo wapitishwe kwenda kupigiwa kura za maoni na wajumbe.

Pia zinatajwa kauli za makada kama Askofu Josephat Gwajima na Hamphrey Polepole kuwa huenda zimechangia ahirisho hilo.

Wakati hayo yakiendelea, CCM imetangaza kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Julai 26 kikitanguliwa na Kamati Kuu, ambayo hata hivyo, hakikutaja sababu za kuitishwa kwa kikao hicho.

Mbali hilo, CCM kupitia kwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla imetangaza kusogeza mbele tarehe ya mchujo wa watiania wa ubunge, uwakilishi na udiwani hadi Julai 28, Kamati Kuu itakapoketi kwa ajili hiyo.

Kwa upande mwingine, wabobezi wa masuala ya kisiasa wameunga mkono sababu zilizotolewa na CCM kuhusu idadi kubwa ya watiania waliojitokeza, wakieleza kunahitajika muda na umakini wa kuchakata majina kwa ajili ya kupata wagombea watatu watakaokwenda kupigiwa kura za maoni na wajumbe, ili kukwepa malalamiko na mpasuko.

Hayo yakitikisa, Makalla ameeleza sababu za kuahirishwa kwa vikao vya uteuzi ni kutokamilika kwa mchakato wa uchujaji wa makada waliotia nia.

Kutokana na hilo, amesema hatima ya makada watakaouteuliwa kwenda kupigiwa kura kuwania udiwani, ubunge na uwakilishi kupitia CCM, itajulikana Julai 28, 2025.

Tofauti na kinachozungumzwe kwenye ulingo wa siasa ndani ya chama hicho, Makalla amesema mchakato wa uchaguzi unaendelea vizuri na kwamba, maandalizi ya vikao vya mwisho vya uteuzi wa wagombea vinaendelea.

“Ile Kamati Kuu ambayo ilikuwa iteue wagombea leo (Julai 19) haitafanyika na badala yake uteuzi wa mwisho utafanyika Julai 28, 2025 na vikao vyote vitafanyika jijini Dodoma,” amesema.

Kwa mujibu wa Makalla, makada wengi wa CCM wakiwamo watiania walitarajia Kamati Kuu ingefanya kikao na uteuzi wa mwisho kwa walioomba nafasi mbalimbali ili kwenda kura za maoni.

Amewataka watiania watulie wakati mchakato ukiendelea, akisema wagombea ni wengi, hivyo kazi ya uchambuzi ni kubwa akiahidi itafanyika kwa umakini mkubwa.

“Niliona simu nyingi juu ya kuahirishwa kwa vikao, sasa hii ndiyo taarifa rasmi kwamba wabunge, madiwani, watiania wote idadi ni kubwa. Watu wamegombea wengi kazi ni kubwa. Tunataka tuendelee kuifanya kwa umakini na kutulia vizuri,” amesema na kuongeza:

“Sababu sisi ndio tuliotoa ratiba na huu ni mchakato ndani ya CCM, ninyi ni mashahidi nafasi tu za madiwani kuna zaidi ya watu 27,000 (walioomba), ubunge zaidi ya watu 10,000 ni watu wengi.”

Makalla amesema ni lazima kupitia wasifu wa watiania wote walioomba nafasi za kugombea kabla ya uamuzi kufanyika.

Kuhusu baadhi ya watu kudaiwa kushinikiza uteuzi, Makalla amesema CCM ina taratibu zake na zinafahamika kwa wanachama wote, hivyo ni lazima zifuatwe.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mpaka sasa hakuna mtu aliyekatwa au kufyekwa hadi Julai 28, 2025 ambayo itatoka taarifa ya mwisho ya uteuzi wa wagombea.

Kuhusu mchakato wa Madiwani wa Viti Maalumu kwa ngazi ya udiwani nchi nzima, Makalla amesema CCM imeridhia majina ya walioomba kuendelea na mchakato wa kuomba ridhaa kwa wajumbe na kupigiwa kura.

Mchakato wa kura za maoni kwa madiwani hao umepangwa kufanyika Julai 20, 2025 katika maeneo yote nchini.

Makalla amesema hayo wakati kukiwa na tetesi kwenye mitandao ya kijamii, zikidai baadhi ya wanasiasa wakongwe wametemwa kuanzia kwenye mapendekezo ngazi za wilaya na mikoa.

Ukiacha tetesi hiyo, yapo madai ya baadhi ya wagombea kucheza michezo michafu kushinikiza ushindi, kama ilivyowahi kuelezwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto.

Mbeto aliweka wazi kuwa, wapo watiania wanaochafuana, wengine wanaandaa wagombea vivuli na kwamba vikao hivyo vya juu, pamoja na mambo mengine vitayapitia yote hayo.

Hata hivyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika mikoa mbalimbali imekaa mguu sawa kuhakikisha inadhibiti vitendo vya rushwa.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamekuwa na maoni tofauti kuhusu sababu za vikao vya mchujo wa wagombea udiwani, ubunge na uwakilishi kusogezwa mbele, wakiwataja makada wa chama hicho, Polepole na Gwajima huenda wakawa nyuma ya ahirisho hilo kutokana na kauli zao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema “isingewezekana CCM Taifa kuchuja majina yote ya watiania katika majimbo 272 katika kipindi walichotenga kwa sababu orodha ni ndefu, lakini jambo la pili mkanganyiko ulioanza kujitokeza kwa baadhi ya vigogo kutopendekezwa katika tatu bora kuanzia ngazi ya chini,” amesema na kuongeza:

“Hali hii inadaiwa ilishaanza kuleta dalili za mpasuko na sintofahamu ndani ya chama, ndiyo Makalla alijitokeza akasema hakuna mchujo uliofanyika hadi CCM Taifa itoe taarifa. Sasa ukiongeza na haya mavuguvugu ya makada maarufu kina Polepole na Askofu Gwajima waliotoa kauli ya kutoridhika na yanayoendelea… inaleta sintofahamu kidogo.”

Dk Kristomus amefafanua kuwa ingetokea leo (Jumamosi Julai 19) CCM wangetangaza majina matatu, wakati vuguvugu la Polepole halijapoa waliokatwa wangepata nguvu ya kusema jambo lolote.

Amesema CCM wametumia busara kusogeza mbele mchakato huo ili joto lililoanzishwa na Polepole lipoe kwanza na kupata nafasi nzuri ya kujipanga.

“Likishapoa na kusahaulika katika vichwa vya makada, baadaye CCM watakuwa na nafasi nzuri kuendeleza mchakato huu, tofauti na hivi sasa wangetangaza tu leo, kuna wale makada maarufu ambao inasemekana wangeachwa ingeleta shida na wangeamua kuungana na Polepole kutoa matamko,” amesema.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Ramadhani Manyeko ameungana na Dk Kristomus akisema kulikuwa na malalamiko mengi ya wagombea ambayo hayakuwahi kuwekwa wazi, wakidai kulikuwa na ukiukwaji wa miiko na kanuni katika mchakato huo wa ngazi za chini.

“Nadhani CCM wamejipa muda wa kuondoa kasoro ili wagombea watakaoteuliwa kusiwe na malalamiko mengi kama chaguzi za nyuma zilizopita. Kuanzia ngazi ya chini kulikuwa na malalamiko na madai ya kuwashughulikia wabunge au wagombea wakongwe, sasa kauli za Polepole na mwenzake zimechangia suala hili kupelekwa mbele,” amesema.

Amesema kauli ya Polepole huenda imechangia ahirisho la vikao hivyo ndio maana viongozi wakuu wa CCM wamekaa na kutafakari kusogeza mbele mchakato ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.

“Unajua wanakwenda katika uchaguzi ambao unahitaji umoja na mshikamano, sasa kama hakuna umoja kutasababisha mpasuko, jambo ambalo si tabia ya CCM kwa namna inavyotambulika. Nadhani wamejipa muda kujipanga ili mchakato ukimalizika chama kibaki kuwa salama,” amesema.

Kwa upande wake Dk Richard Mbunda, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema si vibaya kusogeza muda mbele, akieleza mwaka 2020 kila aliyetia nia alikuwa na haki ya kupigiwa kura, jambo lililolamikiwa, lakini hivi sasa CCM imekuja na taratibu mpya.

“Mchakato wa sasa ni mrefu kwa sababu watiania ni wengi, wanawapa kazi kubwa CCM. Hata hivyo, hatua ya kusogeza mbele mchakato si kwamba kuna shida, labda kama wangesema wanataka kubadili mfumo,” amesema na kuongeza:

“Hata mwaka 2020 walitaka kufanya hivihivi, watu watie nia halafu majina matatu yanarudi kwa ajili ya kura za maoni, lakini wakaona kazi itakuwa kubwa wakaamuru wagombea wote wapigiwe kura.”