Sirro afunguka hali ya usalama Kigoma

Dodoma. Siku chache baada ya tukio la utekaji wa magari na uporaji kutokea Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi linaendesha operesheni mkoa mzima kuwabaini wahusika kisha kuwafikisha mahakamani.

Tukio hilo lilitokea Julai 13, 2025 katika eneo la Kibaoni karibu na kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo Kibondo ambapo majambazi wakiwa na silaha, waliwapora na kuwajeruhi abiria walipokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kwenda jijini Mwanza.

Akizungumzia kuhusu hali ilivyo leo Jumamosi Julai 19, 2025, Sirro ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu amesema taarifa alizonazo ni kuwa operesheni zinaendelea katika mkoa huo katika kuhakikisha kuwa wanawatia mbaroni.

“Askari wetu wako wengi Kigoma sasa maeneo yote na wala si Wilaya ya Kibondo tu ni mkoa mzima wanafanya operesheni kuhakikisha hao waliofanya tukio hilo kwa kushtukiza, wanakamatwa na kupelekwa mahakamani,” amesema.

Mapema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisema yuko porini kikazi na atalizungumzia baadaye

“Bado niko vijijini huku, baadaye labda nitatoa taarifa kamili lakini ni kweli kuna gari la Adventure na Kluger yalitekwa na majambazi wanaoaminika kwamba walikuwa na silaha, wakapora na vitu lakini polisi wa Nduta waliwahi wakazuia ile hali,” alisema Makungu na kuongeza kuwa, hakuna mtu aliyepigwa risasi wala aliyeuawa.

Aliwataka wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa vyombo vya dola vimeimarisha doria saa 24.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Sita, Balozi Sirro amesema Mkoa wa Kigoma kwa ujumla umekuwa mtulivu licha ya kuwa na matukio machache ya uvunjifu wa amani.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kupitia vitengo vyake limeendelea na majukumu yake ya kubaini uhalifu na wahalifu na kuwakamata, kukusanya taarifa za kiintelijensia, kukusanya taarifa za uhalifu na wahalifu na kupeleleza kesi,” amesema.

Amesema makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni mwaka 2024 ni 1,653 ukilinganisha na 1,531 ya kipindi cha Julai 2024 hadi Juni 2025.

Amesema idadi hiyo inafanya upungufu wa makosa 122 sawa na asilimia 7.3.

“Upungufu huu ni matokeo ya juhudi endelevu zinazofanywa katika kupambana na uhalifu na wahalifu kwa kuimarisha doria na misako, kutoa elimu ya polisi jamii kwa wananchi, kupelekea wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,” amesema.

Balozi Sirro amesema idadi ya makosa dhidi ya maadili ya jamii kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Juni, 2024 ilikuwa ni 645 ukilinganisha na kipindi cha Julai 2024 hadi Juni, 2025 ambapo yameripotiwa 702.

Amesema idadi hiyo inafanya uwepo wa ongezeko la makosa 57 ni sawa na asilimia 8.86.

Kwa upande wa makosa ya Usalama Barabarani, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 ajali 67 za usalama barabarani ziliripotiwa ikilinganisha na 53 zilizoripotiwa kipindi kama hicho kwa Julai 2024 hadi Juni, 2025, sawa na upungufu wa matukio 14 (asilimia 20).

Bandari za Ujiji na Kibirizi

Ujenzi wa bandari za Ujiji na Kibirizi Mkoani Kigoma umefikia asilimia 98 huku ikielezwa kukabiliwa na changamoto ya bandari kujaa maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema mradi hiyo inatekelezwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation (CR15G) huku wa Ujiji ukigharimu Sh8 bilioni na Kibirizi Sh16.5 bilioni.

Amesema miradi yote imekamilika kwa asilimia 98 lakini inakabiliwa na changamoto ya bandari kujaa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu miradi ya kimkakati, Balozi Sirro amesema wanaendelea na ukamilishaji wa ukarabati wa Meli ya MT Sangara ambayo inatumika kubeba shehena ya mafuta lita 410,000 katika Ziwa Tanganyika ambao umefikia asilimia 99.

“Meli hii ni kiunganishi na tegemeo kwa shehena ya mafuta yanayosafirishwa kuelekea Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi,” amesema.

Pia wataendelea na utekelezaji wa ukarabati wa Meli kongwe ya Mv Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo ambao umefikia asilimia 15.

Amesema meli hiyo inatarajiwa kutoa huduma ya usafiri kwa abiria na mizigo kwa wakazi waishio katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Pia amesema meli hiyo inatarajiwa kuongeza utalii kwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaofika nchini kutokana na historia yake na kwa kuzingatia meli hii ni sehemu ya urithi wa Taifa.

“Kuendelea na ukarabati wa Meli ya Mv Mwongozo yenye uwezo wa kubeba abiria 800 na tani 80 za mizigo. Mzabuni wa kufanya ukarabati ameshapatikana ambaye ni Kampuni ya Songoro Marine ya Mwanza,” amesema.

Amesema kwa sasa taratibu za maandalizi ya mkataba zinaendelea.

Balozi Sirro amesema kuendelea na ujenzi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Kakonko kwa gharama ya Sh351.4 milioni ambapo ujenzi umefikia asilimia 85.