Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya Kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi.
Akifungua kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA katika ukumbi wa Madinat Al Bahr Zanzibar tarehe 19.07.2025 Dk. Mkuya amesema TRA imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo juhudi za makusanyo zinazofanywa na Watumishi wa TRA zinapaswa kupongezwa.
“Kwa hapa Zanzibar ipo miradi mingi ya miundombunu inatekelezwa, haya ni matokeo ya kodi na ninaunga mkono agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kutaka miradi inayotekelezwa kwa Kodi iwekewe mabango hilo litaongeza chachu ya ulipaji Kodi” Dkt. Mkuya
Amesema Mipango mingi inayowekwa na Serikali imekuwa ikiitegemea TRA katika mapato ya ndani maana yanatokana na makusanyo ya Kodi hivyo ni chanzo cha uhakika cha mapato na kuwataka Watumishi wa TRA kuto kufanya kazi kwa mazoea ili kuendelea kuvuka malengo ya makusanyo ambayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.
“Tunapokwenda kwenye mwaka mpya wa fedha mnapaswa kuwa na vyanzo vipya vya mapato kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii ambapo kazi nyingi za kiuchumi zinafanyika mtandaoni tunapaswa kuzifuata huko” amesema Mkuya.
Ametoa wito kwa Watumishi wa TRA kuendelea kuwa karibu na Walipakodi ili kuwezesha kuendeleza utamaduni wa kulipa Kodi kwa hiari.
Dk. Mkuya ameipongeza Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kwa kuendelea kutoa Elimu ya kodi kwa wananchi kwa njia mbalimbali ambazo zimewezesha kuongeza uelewa kwa Walipakodi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema katika mwaka mpya wa fedha 2025/2025 TRA imelenga kuongeza makusanyo ya Kodi kwa kuongeza wigo wa Kodi na siyo viwango vya Kodi.
Amesema katika mwaka mpya wa fedha 2025/2026 TRA imejipanga kuongeza wigo wa Kodi ili kufikia malengo ya makusanyo na kuleta usawa katika Kodi.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 TRA imejipanga kuendelea kuwezesha biashara na kuwawezesha Walipakodi wanaolipa Kodi vizuri waendelee kulipa, wanaoshindwa kulipa kuwawezesha kulipa na wale ambao hawataki kulipa Kodi kuwafanya walipe Kodi kwa mujibu wa sheria ili kuleta usawa katika Kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema kwa upande wa Zanzibar zipo shughuli nyingi za Utalii ambazo zina nafasi kubwa ya kuongeza makusanyo ya Kodi huku akitaja lengo jipya la makusanyo Zanzibar kuwa ni Sh. Bilioni 825.77 kutoka Sh. Bilioni 647 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 108 ya lengo la Sh. Bilioni 600.
Amewapongeza Watumishi wa TRA Zanzibar kwa juhudi wanaofanya katika kuongeza makusanyo ya Kodi, na kuwaeleza kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kuongeza wigo wa Kodi kwa kuwafanya watu ambao hawalipi Kodi nao waanze kulipa.
Kamishna Mkuu amewashukuru Walipakodi wa Zanzibar kwa kuendelea kuiamini TRA na kushirikiana nayo.
Awali akizungumza katika kikao hicho Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuiwezesha TRA Zanzibar kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.
= = = = = =