BEKI wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ sio tu kumaliza mkataba wake kikosini hapo, pia ameiaga rasmi akionyesha hataendelea na Wekundu hao, huku watani zao wa jadi, Yanga wakitajwa kumalizana naye.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Tshabalala ambaye alikuwa nahodha wa Simba, ameandika: “Takribani miaka 11 ya furaha, huzuni, shangwe, vifijo, nderemo na masikitiko ndani ya mbuga.
“Kwa uaminifu mkubwa, weledi wa kiwango cha juu, kuvuja jasho kupigania nembo ya klabu ndio ulikuwa msingi na malengo.
“Wahenga walisema kila lenye mwanzo, halikosi mwisho na leo nawaaga rasmi, haya ni maamuzi yaliyolenga maendeleo yangu binafsi, maslahi yangu binafsi na weledi wangu uliotukuka.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, benchi la ufundi na watendaji wote wa klabu ya Simba kwa kipindi chote cha kuhudumu ndani ya klabu.
“Kipekee niwashukuru mashabiki kwa kuwa nami kipindi chote, kama mnavyonipenda na mimi nawapenda pia na nina imani mtaendelea kuniunga mkono.
“Nawashukuru wasimamizi wangu wakiongozwa na Carlos kwa ushirikiano mkubwa wa kipindi chote.”
Hatua huyo ya kuaga kwa Tshabalala ni kama inawasha taa ya kijani kwa Yanga ambayo imekuwa ikiipigia hesabu saini ya beki huyo wa kushoto huku ikielezwa ameshapewa mkataba wa miaka miwili.
Tshabalala amehudumu ndani ya Simba kwa takribani miaka 11 ambapo alitua kikosini hapo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.
Katika kipindi cha miaka 11 ndani ya Simba, Tshabalala amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya kikosi hicho kwa kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Pia ameshinda makombe ya FA na Ngao ya Jamii.
Tshabalala pia amechangia Simba kufanya vizuri michuano ya CAF huku timu hiyo ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita 2024-2025 na kupoteza mbele ya RS Berkane. Kabla ya hapo, imeishia robo fainali za CAF mara tano kuanzia 2018.