Wadau waonyesha njia kukabili uhaba wa ajira kwa wahitimu

Dar es Salaam. Uwekezaji katika sekta zinazotengeneza ajira nyingi ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau ili kuendana na ongezeko la wahitimu wa vyuo linaloshuhudiwa kila mwaka.

Vilevile wanapendekeza mabadiliko ya mtalaa vyuoni yaende sambamba na kutumia walimu waliobobea katika maeneo husika ili kuepuka kuwakaririsha wanafunzi vitu kwa nadharia badala ya vitendo.

Mapendekezo hayo yametolewa kutokana na takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) za mwaka 2024 kuonyesha idadi ya wahitimu wa vyuo imefikia 62,570 mwaka 2024 kutoka 48,621 mwaka 2020.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 28.68, wanaume wakiwa asilimia 51 ya wahitimu wote na wasichana asilimia 49.

Kati ya walioingia sokoni mwaka 2024, asilimia 68.54 walikuwa wahitimu wa shahada ya kwanza, huku asilimia 13.3 ni wa stashahada. Wahitimu wa shahada walikuwa 42,889, stashahada 8,328, astashahada (6,051), shahada ya uzamili (4,851), stashahada ya juu (84) na udaktari (367).

Kama ilivyo katika udahili wa wanafunzi, hata upande wa wahitimu kozi tano ndizo zinabeba asilimia 78.22 ya wahitimu wote.

Ripoti inaonyesha biashara ilitoa wahitimu 14,321, elimu (13,834), sayansi ya jamii (8,216), udaktari na afya (7,568) na sheria (5,008).

Mkurugenzi wa Taasisi ya Repoa, Dk Donald Mmari akizungumza na Mwananchi amesema uwekezaji wa kimkakati unaogusa sekta zenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia vijana wanaomaliza vyuo wasibaki mtaani.

Sekta hizo amesema ni zile ambazo zinaweza kuwa na uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu au nguvu kazi, ndiyo maana Dira 2050 umezitambua sekta hizo na kuzipa kipaumbele.

“Moja ya kigezo cha kuchagua sekta hizo ni kukuza ajira, ndiyo maana kuna kilimo, madini na viwanda ambazo zimewekewa mkazo,” amesema.

Ili kuhakikisha sekta hizo zinazalisha ajira zaidi kuendana na wahitimu wanaozalishwa na vyuo amesema ni vyema kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.

“Hii itasaidia kuwekeza katika viwanda, kilimo na madini ili ziweze kukuza fursa za ajira kwa sababu sekta ya umma haiwezi kuajiri kila mtu bali sekta binafsi ikiwezeshwa itasaidia,” amesema.

Suala la kutotengeneza ajira kulingana na mahitaji yaliyopo ni jambo ambalo Serikali ilikiri kujifunza katika utekelezaji wa Dira 2025.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo jambo hilo limepewa uzito katika Dira 2050.

Katika mkutano kati ya wahariri na Wizara ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari aliuliza ni kitu gani ambacho Serikali ilijifunza katika utekelezaji wa Dira 2025 wakati ikielekea utekelezaji wa Dira 2050.

Profesa Mkumbo akijibu alisema wakati wa utekelezaji wa Dira 2025 ukuaji wa uchumi ulikuwa kwa wastani wa asilimia 6.2 hadi asilimia 6.7 ambao mashirika ya kimataifa yameisifia lakini ukuaji huo haukuwa jumuishi vya kutosha kwa kiwango ambacho kilipangwa.

Hiyo ni kwa sababu kasi ya upunguzaji umasikini haukuwa ulivyotakiwa wala utengenezaji wa ajira haukuwa unavyotakiwa.

“Ndiyo maana umeona dhamira yetu kubwa kwenye Dira 2050 ni kujenga uchumi jumuishi, uchumi uwe imara ili ukuaji wake uendane na kuinua hali za maisha ya wananchi kwa kupunguza umasikini na kuongeza ajira,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Balozi Morwa kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) amesema kuna wakati wahitimu hukosa ajira kwa kigezo cha kutoajirika au kukosa sifa stahiki, hivyo lawama zinapaswa kuwaendea walimu, kwani wamekuwa wakifundisha vitu ambavyo hawaviishi.

“Hawaishi yale ambayo wanayafundisha, mtu huwezi kufundisha sheria na haujawahi kuwa mwanasheria ukatoa maarifa yanayotakiwa, utaishia kuwamezesha tu watoto uliyoyameza kutoka katika vitabu mbalimbali wakati huko kwenye soko la ajira kunahitaji vitendo,” amesema na kuongeza:

“Huwezi kumfundisha mtoto ujasiriamali wakati wewe humiliki hata kibanda, unamfundisha mtoto masuala ya benki wakati wewe hujawahi hata kufanya kazi benki unadhani akienda kwenye udahili atapita, haiwezekani.”

Amesema ni vyema mfumo huo ukaangaliwa upya ili kuhakikisha walimu wanaotumiwa vyuoni wanakuwa na maarifa stahiki kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi kuwa shindani katika soko la ajira.

Mitalaa ya vyuo vikuu iliyohuishwa inaanza kutumika katika mwaka mpya wa masomo 2025/26 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuangaliwa upya mfumo wa elimu ili utengeneze wanafunzi wenye ujuzi.

Kumekuwa na kilio kutoka kwa baadhi ya waajiri kwamba wahitimu wengi wa vyuo vikuu hawana uwezo wa kufanya kazi kutokana na kukosa stadi muhimu zinazohitajika kwenye soko la ajira.

Imekuwa ikielezwa kuwa vyuo haviwaandai vyema wahitimu kuingia moja kwa moja kwenye uzalishaji, hali inayowalazimu waajiri kuingia gharama ya kuwafundisha upya ili kuwaweka katika misingi inawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Kupitia Mradi wa wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) changamoto hiyo ilianza kufanyiwa kazo ambapo yamefanyika mapitio ya mitalaa kwa kuwahusisha waajiri, wazoefu katika nyanja mbalimbali za uzalishaji.