Wanariadha 4,000 kuchuana Mwanza kusaka Sh1 bilioni, RT yabariki

JUMLA na wakimbiaji 4,000 wanatarajiwa kushindana katika mbio za hisani za Bugando Health Marathon msimu wa pili zenye lengo la kukusanya Sh1 bilioni za kusaidia wagonjwa wa saratani wasiomudu gharama za matibabu.

‎Idadi hiyo ya wakimbiaji ni ongezeko la wanariadha 2,000 waliochuana kwenye mbio za msimu uliopita.

‎Bugando Health Marathon itafanyika Agosti 3, 2025 huku wanariadha katika makundi mbalimbali wakishindana katika Kilometa 2.5, 5, 10 na 21, ambapo washindi wa kwanza hadi wa tano watapata zawadi mbalimbali.

‎Akizungumza leo Jumamosi Julai 19, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa vifaa na njia zitakazotumika kukimbilia, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi amewahakikishia wanariadha kuwa msimu wa pili wa mbio za Bugando zimekidhi vigezo vyote na washindi watapata zawadi zao kwa wakati.

‎Amewapongeza waandaji wa mbio hizo kwani zinawasaidia wanariadha kujiweka fiti na kuwa na maandalizi wakati wote, huku akiwahamasisha wakimbiaji wa Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanatoa ushindani kwa wenzao wa Arusha ambao mara nyingi wamekuwa washindi.

‎”Natoa wito kwa wakimbiaji wote wajisajili kwa wingi kwa sababu mbio zetu zimekidhi vigezo vyote, kazi ni kwa wenyeji kubakiza ushindi nyumbani na kuacha mazoea ya washindi kutoka Arusha,” amesema Isangi.

‎Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Billy Kinyaha amesema wameanzisha kampeni hiyo kusaidia kuokoa maisha ya watu wa Kanda ya Ziwa, ambapo kwa kiingilio cha Sh35,000 mkimbiaji atachangia kupatikana Sh1 bilioni.

“Mwitikio ni mzuri watu wanaendelea kujisajili, mwaka jana tulifanikiwa kuweka hamasa na wananchi wakaona umuhimu wa kuchangia matibabu kwa wagonjwa wasiojiweza,” amesema Kinyaha.

‎Kaimu Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Bahati Wajanga amesema mbali na matarajio ya kukusanya fedha kutoka kwa wakimbiaji 4,000 watakaosajiliwa, Watanzania wengine wana nafasi ya kuchangia kuanzia Sh1,000 ili kupata Sh1 bilioni ya matumaini.

‎”Kwa wastani mgonjwa wa Saratani anahitaji Sh10 milioni kwa kipindi cha matibabu yake, gharama hii ni kubwa kwa Watanzania hali inayosababisha wagonjwa wengi kukatisha matibabu,” amesema Dk Wajanga.

‎Naye, Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala akizindua jezi zitakazotumika kwenye mbio hizo, ameipongeza Bugando kwa kuandaa mbio hizo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wasio na uwezo, huku akichangia Sh500,000.

‎”Natoa wito kujisajili sisi wenyewe, marafiki na jamaa zetu na watu wote wenye mapenzi mema tushiriki sote kutoa hamasa ili tukio letu hili lifanikiwe, tuwaunge mkono Bugando kwani wanachokifanya hapa ni kwa maslahi ya Watanzania wote,” amesema Salala.