Baa, gesti mitaani zinavyovuruga maadili

Dar/Mikoani. Kwa muda mrefu, kumekuwapo mjadala kuhusu kuporomoka kwa maadili, hususan ya vijana nchini, hali inayochangiwa na kuwapo mwingiliano wa mambo katika mazingira ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

Miongoni mwa hayo ni mabadiliko ya kijamii, ikiwamo mifumo ya malezi, ambayo wazazi wengi hivi sasa ni kama hawana muda wa kuwa karibu na watoto wao kutokana na majukumu ya kikazi.

Si hivyo tu, kuna ukuaji holela wa miji. Katika maeneo mengi mijini, kumekuwa na ujenzi holela usiozingatia mipango miji, hali inayosababisha kuwepo kwa mchanganyiko wa makazi na biashara zisizo rafiki kwa maadili, kama vile baa, vilabu vya usiku, nyumba za kulala wageni na maduka ya pombe ambayo yapo karibu na shule, nyumba za makazi na hata za ibada.

Baa nyingi hufanya kazi hadi usiku wa manane au alfajiri, huku kukiwa na muziki, unywaji pombe, na mara nyingine vitendo visivyo na staha vikifanyika hadharani.

Nyumba za kulala wageni, na hasa zile zisizodhibitiwa, hutumika vibaya kama maeneo ya kukutania kimapenzi, jambo linalowavutia vijana kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi, ngono zembe na hata ukahaba.

Kupitia maeneo hayo, baadhi ya vijana hupoteza dira na mwelekeo wa maisha yao, hawapati fursa ya kujifunza nidhamu, adabu, heshima na maadili kutoka kwa watu wazima au taasisi za malezi kama vile familia, shule na dini.

Mazingira hayo huchochea tabia za utumiaji wa dawa za kulevya, uhalifu kama vile wizi, na ushawishi wa kuingia kwenye makundi hatarishi ya kihalifu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika ripoti hii maalumu umebaini chanzo cha uwepo wa ujenzi holela ni kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa sheria, ikiwamo utoaji wa vibali vya ujenzi.

Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 inatoa mwongozo wa matumizi ya ardhi na kanuni za maendeleo ya miji, ikilenga kuhakikisha mipango ya maendeleo ya miji inafanyika kwa mpangilio mzuri na inazingatia usalama, afya na ustawi wa umma.

Sheria hii inazungumzia ujenzi wa maeneo ya biashara kama baa na nyumba za kulala wageni, ikielekeza majengo hayo yasijengwe maeneo yanayoweza kuathiri jamii, utulivu na ukuaji wa watoto.

Hata hivyo, hali ni tofauti kama anavyoeleza Levina Kimario, mkazi wa Tabata, mkoani Dar es Salaam, anayesema: “Hali ni mbaya siku hizi, umepanga nyumba mbele kuna fremu, wanaanza na duka la kawaida, baada ya siku mbili wanaanza kuuza pombe. Kukiwa na walevi, lugha zao hazifai kwa watoto.”

Amesema biashara hiyo huondoa utulivu kutokana na muziki unaopigwa hadi usiku wa manane bila kujali eneo hilo ni la makazi ya watu.

Si baa pekee, amesema: “Imekuwa ni kawaida kuona nyumba ikikarabatiwa, baadaye unaona tangazo ni nyumba ya kulala wageni. Unabaki unajiuliza, hivi mamlaka zinaona mambo haya? Mbona kama ziko kimya?”

Kauli ya Levina inaakisi hali ilivyo katika miji na majiji mbalimbali nchini, ambako ujenzi wa baa na nyumba za kulala wageni kwenye maeneo ya makazi ya watu na jirani na majengo ya shule limekuwa kama jambo la kawaida.

Awadhi Mzenga, mkazi wa Mabibo, mkoani Dar es Salaam, amesema mamlaka hazisimamii ipasavyo utekelezaji wa sheria, hivyo kutoa mwanya wa uwepo wa ujenzi holela.

“Tutalalamika kuwepo kwa gesti na baa, lakini kuna mamlaka zinazosimamia kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa. Inamaanisha hadi jengo linamalizika, hakuna viongozi wanaojua?” amehoji.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno, amekiri kuhusu kuwapo kwa upungufu katika usimamizi wa sheria katika utoaji wa vibali vya ujenzi.

Amesema kuna haja ya kufanya ufuatiliaji ili waliojenga kinyume cha sheria, hatua stahiki zichukuliwe.

Aliyekuwa diwani wa Manzese, Eliam Manumbu, amewashutumu watendaji wa manispaa kwa kutofanya kazi kwa umakini, akieleza iwapo wangefanya kwa ufanisi na weledi, isingekuwa rahisi kuona majengo ya baa au nyumba za kulala wageni zikiwa jirani na shule.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, ameomba apewe muda wa kufuatilia suala hilo. “Tunaomba tufuatilie suala hili na tutarudi kwako,” amesema Mabelya alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Mtazamo wa wazazi, walimu

Jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Mtaa wa California, Fadhili Nassoro amesema: “Katika mtaa wangu, kuna baadhi ya baa inapofika usiku huwa wanafungua muziki ambao huwaathiri wakazi. Kuna watu wana presha, kisukari, ambao hawahitaji kelele bali utulivu wa akili na mwili. Tunaomba wafunge soundproof (vifaa kuzuia sauti kutoka nje).”

Amesema baadhi ya nyumba za kulala wageni zimejengwa jirani na shule, jambo linalochochea wanafunzi kuiga matendo na maisha yanayoendelea katika maeneo hayo, hivyo Serikali iliangalie suala hilo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya, Masunga Kea, amezungumzia kuhusu nyumba za kulala wageni, akieleza baadhi zimekuwa sehemu za watu kufanya ukahaba.

“Maeneo kama Nyegezi kona kuna wadada wanaojiuza. Ukiangalia maeneo hayo yapo karibu na makazi ya watu, inaleta taswira mbaya. Licha ya kwamba tumejaribu kufanya operesheni na msako kuwakamata na kuwapeleka kituoni, baada ya muda unawaona tena. Tunaomba Serikali itusaidie katika hilo,” amesema.

Judith Wambura maarufu Mama Warioba, mkazi wa Mtaa wa Mabatini, aliyepanga jirani na nyumba ya kulala wageni, amesema matendo yanayoendelea usiku na mchana yanatia aibu na yanamtatiza katika malezi ya watoto wake.

“Mazingira kama haya kwetu ni kero, inatupa changamoto ya kulea watoto. Yanawafanya kuamini hayo ni maisha ya kawaida.

“Kuna haja ya kuwa na maeneo tofauti kati ya yale ya makazi ya watu na nyumba za wageni ili kuepusha mkanganyiko na kuwezesha watoto kupata malezi stahiki,” amesema.

Yohana Paul, mkazi wa Mtaa wa 14 Kambarage, mjini Geita, amesema uwepo wa nyumba za kulala wageni na baa kwenye makazi ya watu, jirani na shule au nyumba za ibada, kunatokana na changamoto za mipango miji, hali inayochangia mmomonyoko wa maadili hasa kwa watoto na vijana.

Amesema mamlaka za Serikali za mitaa zinapaswa kuwajibika kusimamia, kupanga na kuratibu mchakato mzima wa ujenzi wa nyumba za kulala wageni ili kuepusha mmonyoko wa maadili.

Kwa upande wake, Nasra Ismail, mkazi wa Katoro mkoani Geita, amesema: “Vitendo na tabia mbaya hasa kwa watoto ni kutokana na yale wanayoyaona.”

Ameshauri halmashauri kupanga maeneo rasmi, badala ya watu kujenga kiholela na matokeo yake kusababisha maadili kuporomoka.

Mwalimu Mkuu katika moja ya shule mkoani Dar es Salaam amesema: “Tunapata tabu wakati mwingine kwenye ufundishaji. Watoto wanaweza kuona tukio nje ya baa, wanakuja kusimuliana. Wapo wanaotoka nje kwenda kuangalia.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Mpakani, Dar es Salaam, Msafiri Mwajuma, amehusisha ujenzi holela na uzembe wa halmashauri, ambazo hutoa vibali vya ujenzi bila kufuatilia kwa kina maeneo yanayoombewa vibali hivyo.

“Hata inapotokea wakapelekewa malalamiko, wanasema haina madhara kwa kueleza umbali uliopo baina ya majengo hayo na shule,” amesema Msafiri.

Akizungumzia kuhusu baa, Maenda Mhando, mkazi wa Tabata, amesema: “Siku hizi kila duka linalouza pombe linaweka viti na kupiga muziki. Ni usumbufu. Unajiuliza, hawa wamepewa leseni ya kufanya kazi kama baa inayoruhusu watu kukaa, au wanatakiwa kuuza watu wakanywee sehemu nyingine?”

Amesema kutokana na muziki unaopigwa, watoto hushindwa kujisomea kwa utulivu.

Biashara ya vileo inatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Vileo ya Mwaka 1968 na marekebisho yaliyofanywa mwaka 2004. Inatoa miongozo kuhusu aina za leseni, imeweka katazo kwa mtu anayefanya biashara ya pombe kinyume cha matakwa ya leseni, huku ikiainisha muda wa uuzaji, maeneo yanayoruhusiwa na masharti mengine muhimu.

Sheria inatamka adhabu kwa wanaoikiuka, ikiwamo kufutiwa leseni, faini au kufungiwa biashara.

Kelele na sheria ya mazingira

Kuhusu kelele kutoka baa na kumbi za starehe, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekuwa likifanya msako na kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.

Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, Kifungu 106(5) kinaeleza: “Si ruhusa kwa mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kelele kuzidi kiwango kilichoainishwa au kitakachobainishwa kuhusiana na upigaji kelele.”

Kifungu cha (6) kinasema: “Litakuwa ni kosa kwa mtu yeyote kumwaga uchafu au kupiga kelele bila kuzingatia njia iliyobainishwa kuwa ni bora katika kanuni zinazoweza kutungwa na waziri.”

Waziri mwenye dhamana ya mazingira kupitia Kifungu cha 230(2)(s) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 ya mwaka 2015, alitunga Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Viwango vya Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015 (Tangazo la Serikali Na. 32 la mwaka 2015).

Kanuni zinabainisha viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makazi, biashara, viwanda na hospitali. Kwa mfano, maeneo ya makazi yanaruhusiwa kuwa na kelele za hadi decibel 55 mchana na 45 usiku.

Wanaokiuka viwango hivi wanakabiliwa na adhabu mbalimbali, ikiwamo faini kuanzia Sh5 milioni hadi Sh10 milioni, kufungiwa biashara na hatua za kisheria kama vile kufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji katika Jiji la Dar es Salaam, Maduhu Ilanga, amesema udhaifu wa usimamizi na ukiukwaji wa sheria na taratibu za upangaji miji unachangia kuzorotesha matumizi ya ardhi yaliyopangwa kwa mujibu wa sheria.

“Halmashauri zote, iwe ni za majiji, manispaa, wilaya au miji midogo, kisheria ni mamlaka za upangaji. Zinapaswa kupanga matumizi ya ardhi kwa kuzingatia sheria zilizopo ili kuwapo mpangilio bora wa miji,” amesema.

Kwa mujibu wa Ilanga, sheria zimeweka bayana majukumu ya halmashauri katika upangaji wa matumizi ya ardhi. Sheria hizo ni Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982, Sheria ya Mipango Miji Sura 355 ya mwaka 2007 na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.

“Ardhi ya jiji imegawanyika katika mafungu makuu matatu, kuna ardhi ya jumla, ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi. Ardhi ya jumla ndiyo inayosimamiwa na halmashauri, ambazo zinapaswa kutenga maeneo ya makazi, huduma kama vile shule, hospitali, maeneo ya viwanda, makaburi na mengineyo kulingana na mahitaji,” amesema.

Amesema matumizi ya ardhi yanapaswa kuzingatia yanayoendana, kwani yapo yasiyoendana kama vile shule haiwezi kuwa karibu na ama kiwanda au nyumba ya kulala wageni, huku msikiti ukiwa kando ya baa au klabu ya usiku.

“Hata kama lodge ni sehemu ya makazi maalumu, matumizi yake hayapaswi kuingiliana na makazi ya kawaida ya familia au huduma nyeti kama shule na hospitali. Ndiyo maana sheria imeelekeza kila matumizi ya ardhi yatengwe kwenye maeneo yanayofanana,” amesema.

Amesema kuna watu hujenga nyumba kwa lengo la kuishi, lakini baadaye huibadilisha kimyakimya kuwa ya kulala wageni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Hii ni changamoto ya usimamizi dhaifu. Ujenzi wa gesti kwenye maeneo ya makazi bila kufuata taratibu ni uvunjaji wa sheria. Si kwamba sheria haipo, bali utekelezaji wake ndiyo umekuwa tatizo,” amesema.

Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 imeweka wazi kuwa matumizi ya ardhi yanapaswa kuidhinishwa kwa mujibu wa mpango wa matumizi ya ardhi, na hairuhusiwi kubadilishwa bila kibali cha mamlaka husika.