London / Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeshinda tuzo tatu za kimataifa na kutajwa na jarida la kifedha la kimataifa la Euromoney kama Benki Bora Tanzania.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo, iliyohudhuriwa na wabobezi wa huduma za kibenki zaidi ya 500, ilifanyika Julai 17, 2025, jijini London, Uingereza, na CRDB kuibuka kidedea katika vipengele vitatu.
Vipengele hivyo ni pamoja na Benki Bora Tanzania, Benki Bora kwa Masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), na Benki Bora kwa Biashara Ndogo na za Kati (SME).
Tuzo hizo tatu zimekuja ikiwa ni miezi miwili imepita tangu CRDB kutambuliwa na jarida hilo kama Benki Bora kwa huduma za benki zinazofuata misingi ya Kiislamu nchini Tanzania, wakati wa utoaji wa Tuzo za Euromoney Islamic Finance zilizofanyika Dubai, Mei 20, 2025.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya benki hiyo, tuzo hizo zinakwenda kuwaongezea chachu ya kuendelea kusimamia kusudi lao la kuboresha maisha na kuleta mabadiliko chanya ya kudumu.

“Heshima hii ya tuzo kutoka Euromoney inadhihirisha dhamira ya msingi ya benki yetu ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo kwa watu binafsi, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla, kukuza maendeleo jumuishi, uwajibikaji wa kifedha, na maendeleo endelevu,” amesema Mwambapa.
Pia amesema zinaonesha mtazamo mpana na wa kimkakati wa CRDB katika utoaji wa huduma za kifedha, unaolenga kuleta mageuzi kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha, kukuza biashara endelevu na kuwawezesha wananchi katika masoko yanayohudumiwa.
Vilevile, amesema inaonesha juhudi za benki katika kubuni na kutoa huduma mahsusi kwa biashara ndogo na za kati, ambazo ndizo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, ubunifu, mageuzi ya kidijitali, na upanuzi wa huduma za fedha kikanda.
“Tuzo hizi pia ni za kipekee kwa sababu zinakuja wakati benki inaadhimisha miaka 30 ya uwepo wake sokoni, ikisheherekea mchango wake katika kuimarisha masuala ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania tangu mwaka 1996.
“Tunashukuru kupokea tuzo hizi wakati tunapoendelea kusimamia vipaumbele vyetu vya kukuza na kulinda biashara yetu, huku tukileta athari chanya katika jamii na kujiandaa kwa ajili ya siku za usoni.
“Tuzo hizi ni alama ya imani ya wateja na wanahisa wetu kwetu, uongozi wenye maono wa bodi na menejimenti, pamoja na kujituma kwa kila mfanyakazi,” amesema ofisa huyo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, benki hiyo pia ilijishindia tuzo ya dhahabu ya Kimataifa ya Uwekezaji katika Jamii (International CSR Awards 2025) kupitia mbio zake za kimataifa za CRDB Bank International Marathon.
Tuzo hiyo ya hadhi ya juu ilitolewa na CSR Society, shirika huru la kimataifa linalotambua na kuenzi mashirika yenye juhudi za uwajibikaji wa kijamii duniani kote, lenye makao makuu yake nchini Uingereza.
Mwaka huu, Benki ya CRDB ilikuwa miongoni mwa washiriki 300 walioshindana kutoka nchi mbalimbali duniani na kushinda tuzo hiyo kwa kuonesha ubunifu mkubwa katika uwezeshaji wa kijamii katika nyanja tofauti.
Akiiwakilisha Benki ya CRDB na kupokea tuzo na cheti cha ushindi, Ofisa Uwekezaji wa Jamii, Natalia Tuwano, alisema tuzo hiyo inaipa Benki ya CRDB heshima na hadhi ya juu katika kuiwezesha jamii.
Kutokana na tuzo hiyo, Benki ya CRDB sasa inaweza kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Green World Awards mwakani.