Dar es Salaam. Kukosekana kwa maarifa stahiki kwa madereva wa bodaboda, ndiyo sababu iliyotajwa kuchochea makosa ya usalama barabarani kwa madereva wa vyombo hivyo na usafiri na hatimaye kusababisha ajali.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Chang’ombe wilayani Temeke, Reverent Nkyami amesema baadhi ya bodaboda wanajifunza mtaani siku mbili na kuingia barabarani, hatua iliyosababisha matukio ya ajali za barabarani na vifo.
Kauli ya mkuu huyo wa usalama barabarani, inasadifu takwimu zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, zinazoeleza ajali za bodaboda zimepoteza uhai wa wananchi 1,113 kati ya mwaka 2022 hadi 2024, sawa na wastani wa vifo 46 kila mwezi.
Naibu waziri wa wizara hiyo, Daniel Sillo amesema kati ya idadi hiyo ya waliofariki kwa usafiri huo, madereva ni 759, abiria 283 na wananchi wanaotembea kwa miguu kandokando ya barabara na wanaovuka na kugongwa ni 71.
Nkyami ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Jumapili Julai 20, 2025 wakati wa kongamano la madereva wa bodaboda wilayani Temeke, lililoambatana na uzinduzi wa kilainishi cha Caltex kinachotumika kwenye usafiri huo.
Amesema madereva hao wa bodaboda wanatakiwa kujifunza kwa kina sheria za usalama barabarani na kupata maarifa sahihi ya matumizi ya barabara.
Ameeleza ukosefu wa elimu rasmi na mafunzo ya usalama barabarani umechangia madereva wengi wa pikipiki kuendesha kiholela bila kuzingatia sheria, hali inayochochea ongezeko la ajali na vifo barabarani.
“Kumekuwa na tabia ya kujifunza siku mbili tu mitaani, kesho mtu anaingia barabarani bila uelewa wa sheria. Mbaya zaidi anapakia abiria zaidi ya uwezo ‘mishikaki’ hana stadi ya kuendesha kwa usalama na mwisho wa siku anagongwa au anasababisha vifo,” amesema Nkyami.
Ameongeza jeshi hilo limeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa waendesha vyombo vya moto na kufanya operesheni mbalimbali, zenye lengo la kuongeza uelewa kwa madereva na kupunguza ajali barabarani.
“Asilimia kubwa ya ajali zinahusisha pikipiki, iwe ni dhidi ya waenda kwa miguu, magari au hata pikipiki kwa pikipiki. Hivyo tumejikita katika kutoa elimu zaidi kwa bodaboda ili kukomesha hali hiyo,” amesema.
Mkuu wa kitengo cha vilainishi kutoka Kampuni ya Karimjee Value Chain Limited, Anam Mwemutsi amesema wameanzisha bidhaa hiyo kuepuka uchakachuaji.
“Tumeleta kilainishi chenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 5,000 bila kubadilishwa, tofauti na sasa ambapo wengi hubadilisha kila baada ya wiki moja. Hii itapunguza gharama na kuongeza ufanisi wa vyombo vya usafiri,” amesema.
Msemaji Msaidizi wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Msisiri amesema ni kiu yao kukomesha ajali za barabara na juhudi mbalimbali zinafanywa kufanikisha hilo.