Dar es Salaam. Zaidi ya Watanzania 500 wamenufaika na mafunzo ya ufundi na utawala nchini Japan kuanzia miaka ya 1980 mpaka sasa.
Mafunzo hayo yametolewa kupitia Taasisi ya Japan iitwayo Association for Overseas Technical Cooperation and Sustainable Partnerships (AOTS), ambayo inafadhiliwa na Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan (Meti). AOTS ni taasisi yenye lengo la kuboresha ufanisi wa kiufundi na kiviwanda katika nchi zinazoendelea.
Taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Organization for Technical Enhancement and Industrial Development (Otide) ni mshirika wa AOTS nchini Tanzania. Otide, pamoja na majukumu mengine, inawasaidia Watanzania kushiriki katika mafunzo haya kwa kuwapeleka nchini Japan, ambapo wanapata ujuzi muhimu wa kuboresha sekta za kiufundi na kiviwanda.
Naibu Katibu Mkuu wa Otide Tanzania, Godwin Mmbaga, amesema hayo jijini Dar es Salaam Julai 18, 2025 alipozungumza wakati wa ziara ya Meya wa Jiji la Nangai, nchini Japan, Shigeharu Uchia, aliyoifanya kwenye viwanda mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuhitimisha kwenye kiwanda cha Superdoll Trailers Manufacture Ltd.
Mmbaga amesema Watanzania walionufaika ni kutoka taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi.
Akizungumzia kuhusu ziara ya Meya wa Jiji la Nangai nchini, Mmbaga amesema ziara hiyo imetokana na ujio wa viongozi wa jiji hilo mwaka 2023, na baada ya kutembelea vyuo vya VETA waligundua kuwa vinahitaji walimu wake kuongezewa ujuzi wa mbinu za kufundisha, ili kutoa vijana wenye uwezo mkubwa zaidi kiutendaji na waweze kukidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa.
“Kuna gepu la uwezo wa kiutendaji kwa wanafunzi wanaohitimu VETA, hivyo meya amekuja na msafara wa wadau wa ufundi kutoka Japan kwa lengo la kutathmini hali hiyo, wakati mradi mkubwa wa Serikali ya Japan unaoendeshwa na JICA hapa nchini wa kuwajengea uwezo walimu wa VETA ukiwa kwenye hatua za awali,” amesema.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Nangai, Uchia, amesema utekelezaji wa mradi huo utakuza ubora wa uzalishaji nchini, utachochea ongezeko la ajira kwa vijana wahitimu wa VETA hapa nchini na wengine watafaidika kwa kupata ajira nchini Japan.
Amesema Japan kwa sasa ina nafasi nyingi za ajira, lakini kuna idadi ndogo ya vijana wanaoweza kuajiriwa huku idadi ya wazee wastaafu ikiwa kubwa kuliko vijana. Jiji la Nagai nchini Japan lina urafiki na Jiji la Dodoma, Tanzania.