New York Marekani. Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya teknolojia ya Astronomer Inc. ya nchini Marekani ameamua kujiuzulu baada ya kunaswa kwenye kamera akibusiana kwenye tamasha la muziki wa rock na mwanamke ambaye hakuwa mkewe.
Kufuatia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumatano, kigogo huyo anayeitwa Andy Byron ameamua kuachia ngazi ambapo bodi ya wakurugenzi imekubali huku Ofisa Mkuu wa Bidhaa Pete DeJoy akihudumu kama Ofisa Mtendaji Mkuu wa muda.
Kwa mujibu wa CNN, Reuters na DW, Byron alinaswa akiwa na Ofisa Mkuu wa rasilimali watu wa Astronomer, Kristin Cabot, kwenye kamera wakati wa tamasha la Coldplay Jumatano iliyopita huko Massachusetts.
Msemaji wa kampuni hiyo amesema wawili hao ndio walikuwa wafanyakazi pekee wa kampuni hiyo walionaswa kwenye kamera.
Pindi waliponaswa na kugundua kuwa walikuwa wakionyeshwa kwenye skrini kubwa ndani ya uwanja wa Gillette walipokuwa wakikumbatiana, Byron alijificha na Cabot alifunika uso wake kwa mikono.
Kampuni hiyo ya uendeshaji wa data, iliyoanzishwa mwaka 2018, imesema itaendelea na dhamira yake kushughulikia matatizo ya data na akili bandia. Pia imesema mwanzilishi mwenza na DeJoy, atahudumu kama ofisa Mtendaji mkuu wa muda.
Kwa sasa akaunti ya LinkedIn ya Byron haionekani tena hadharani na ameondolewa kwenye ukurasa wa uongozi wa kampuni kufuatia tangazo hilo, ambalo sasa linamtambua mwanzilishi mwenza DeJoy kama CEO.
Kwa upande mwingine video za tukio hilo zimepata mamilioni ya watazamaji kwenye TikTok na mitandao ya kijamii, zikisababisha ‘memes’
Hata hivyo, kulingana na utafiti wa magazeti maarufu kama vile New York Post na Daily Mail, Cabot, ambaye amewekwa likizo isiyo na kikomo wakati kampuni inafanya uchunguzi inaelezwa ameolewa.