Kipato kidogo chatajwa kuongeza hatari maambukizi ya VVU kwa Vijana

Hai. Wakati Taifa likiendelea na jitihada za kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU), imeelezwa kuwa, uwezo wa kifedha wa watu wazima unaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazowaweka vijana katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti wa Masuala ya Uendelevu na Mambo ya Ubia (Afrika), Simon Shayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya GGM Kili Challenge 2025 yenye lengo la kuchangishaji fedha kuunga mkono juhudi za kitaifa za kupambana na VVU.

Kampeni hiyo iliyowakutanisha wapanda milima 49 na waendesha baskeri 17 kutoka ndani na nje Tanzania imedhaminiwa na Kampuni ya Dhahabu ya Geita Gold Mining kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), uliofanyika katika lango la Machame.

Shayo amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na mashirika hayo, kundi la vijana bado limeendelea kuwa hatarini, huku akitoa wito kwa wadau hasa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya VVU.

“Natoa wito maalumu kwa sisi kama waajiri hasa sekta binafsi kutupa jicho la pekee kwa vijana hasa waliopo shuleni, tunafahamu wakati maambukizi yanashuka kwa wengine,yanapanda kwa vijana,” amesema Shayo.

“Maana yake nini, tutakuwa na Taifa ambalo sio salama kwa siku zijazo na kazi hii ya kulinda vijana inapaswa kufanywa na kila mmoja wetu.

“Tunayo safari ndefu, kuna makundi ambayo pamoja na juhudi zote hizi yameendelea kuwa hatarini, wito wetu kwa wadau wote hasa sekta binafsi sio jukumu la Serikali ni jukumu letu wote,” amesema Shayo.

Pia, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano katika kipindi chote.

 ‘‘Tumeendelea na tutaendelea kusaidia maendeleo ya jamii katika sekta mbalimbali kupitia miradi ya afya, elimu na miundombinu.”

Kuhusu mapambano dhidi ya VVU, amesema mbali na kampeni ya Kili Challenge, GGML kwa kushirikiana na Tacaids imeanzisha vituo vya kutoa elimu na huduma mbalimbali katika maeneo ya mikusanyiko, ikiwamo Michungwani (Tanga) na Manyoni (Singida) ili kutoa elimu, ushauri na kinga.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Yasin Abbas amesema kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa mwaka 2022, kukithiri kwa VVU nchini kunaonesha wanawake wanaoongoza kuwa na maambukizi kwa asilimia 5.6, ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 3.0.

Aidha, amesema maambukizi hayo yanachangiwa na shughuli hatarishi kama migodini na uvuvi, madereva wa masafa marefu.

“Ushirikiano huu kati ya Serikali, GGML na wadau wengine wakiwamo wadhamini ni muhimu sana katika vita hii. Tunapojumuika kama hivi, tunaongeza kasi ya kutokomeza VVU, kuondoa unyanyapaa na kupunguza vifo,” amesema Abbas.

Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Miundombinu wa Mkoa, Jackson Masaka akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha jamii inapata huduma muhimu za kiafya na wanabaki salama.

“Kampeni hii ina mchango mkubwa katika kufikia malengo ya kitaifa ya kufikia sifuri 3, kutokuwa na maambukizi mapya ya   VVU, kutokuwa na unyanyapaa na ubaguzi wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na kutokuwa na vifo vitokanavyo na Ukimwi ifikapo mwaka 2030,” amesema.

“Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050 imeweka msisitizo kwenye maeneo mbalimbali ya kipaumbele, likiwamo la ustawi wa jamii. Kupitia kampeni hii, GGML inachangia juhudi za Serikali katika kudhibiti na kuzuia kuenea kwa janga hilo hapa nchini,” amesema Masaka.

Kampeni hiyo inaunga mkono malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikia sifuri tatu ifikapo mwaka 2030, ambazo ni kuzuia maambukizi mapya ya VVU, vifo vinavyotokana na Ukimwi na unyanyapaa.

Pia, utekelezaji wa dira unalenga kuongeza umri wa kuishi wa Watanzania kutoka wastani wa miaka 68 ya sasa hadi 75 kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.