Dar/mikoani. Uchaguzi wa kuwapata madiwani wa viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mikoa mbalimbali nchini unaendelea.
Wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, jumla ya wajumbe 1,300 wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Bukoba Vijijini, wanaendelea kupiga kura kuwachagua madiwani tisa wa viti maalumu, kati ya wagombea 33 walioteuliwa kuwania nafasi hizo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Julai 20, 2025, msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Bukoba Vijijini, Jesca Ndyamkama amesema kazi hiyo inaendelea kwa utulivu na amani katika maeneo yote ya uchaguzi.
“Tuna tarafa nne ambazo kila moja ina idadi maalumu ya madiwani wanaotakiwa kupigiwa kura. Tulitarajia kuwa na wajumbe 1,460, lakini hadi sasa waliojitokeza kushiriki ni 1,300 na uchaguzi unaendelea hadi saa 12 jioni hii,” amesema Ndyamkama.
Ameongeza kuwa wingi wa wajumbe waliojitokeza kushiriki umewashangaza, kwa sababu hawakutarajia idadi hiyo kubwa.
Amesema mkutano wa aina hiyo haujawahi kufanyika kwa ukubwa kama huo wilayani humo.
Ndyamkama amewahimiza wagombea ambao hawatapata nafasi kuwa na moyo wa subira na kuendelea kuwa na imani na CCM akisisitiza kuwa matokeo ya leo si ya mwisho.
“Uamuzi rasmi wa mwisho utafanyika katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025,” amesema katibu huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, Erasto Sima amesema vyombo vya usalama vinaendelea kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika hatua zote za uchaguzi huo katika maeneo yote ya wilaya.
Nako wilayani Mbeya, mchakato wa kuwapata madiwani hao umefikia hatua ya kupiga kura huku wagombea wakisubiri hatima yao.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulipaswa kuanza asubuhi lakini umeanza saa sita mchana kutokana na uwingi wa wagombea waliokuwa wanajinadi.
“Kwa sasa kazi inayoendelea ni upigaji kura kwa ngazi za tarafa ambazo zimegawanywa sehemu mbili, Sisimba na Iyunga,” amesema.
Zaidi ya wapiga kura 1,500 wanashiriki kupiga kura za kuwapata viongozi hao ambao ni 12, watano watatoka Tarafa ya Sisimba na saba kutoka Iyunga.
Mkoani Songwe, jumla ya watia nia 88 wa udiwani viti maalumu wanaendelea kujinadi.
Huku baadhi ya wanachama wakiwa wamekusanyika kwenye kumbi za ofisi za chama wakisubiri matokeo ambayo yataamua hatima ya baadhi ya wagombea, ambao wameahidi kuwasimamia wanawake katika miradi mbalimbali sambamba na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri.
(Imeandikwa na Ananias Khalula (Bukoba), Sadam Saddick (Mbeya) na Denis Sinkonde (Songwe)