Bwana Yesu asifiwe wapendwa katika Kristo, leo tumepewa ujumbe unaosema Neema ya Mungu hutupa nguvu ya kushinda majaribu ya maisha. Katika dunia hii tunayoishi, kila mmoja wetu anakumbana na changamoto, vishawishi, na majaribu ya kila namna. Lakini ashukuriwe Mungu kwa sababu hakutuacha yatima; ametupa neema yake neema ambayo siyo tu ya wokovu bali pia ya kutushika, kutuongoza na kutupa nguvu ya kushinda.
Neema ni zawadi ya Mungu isiyostahiliwa:
Biblia inasema katika Waefeso 2:8-9: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
Hii inatuonesha kuwa neema ni zawadi hatuipati kwa sababu ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu. Hii ni neema ileile inayotuwezesha kusimama wakati wa dhiki, matatizo na kupata nguvu mpya ya kusimama.
Neema hutupa nguvu ya kushinda majaribu:
Katika 2 Wakorintho 12:9, Paulo anasema: “Lakini aliniambia, Neema yangu yakutosha; kwa maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.”
Paulo alikuwa na “mwiba” katika mwili wake jambo lililomsumbua sana, lakini Mungu alimwambia kuwa neema yake inamtosha. Hii inatufundisha kuwa hata sisi tunapopitia majaribu, hatuachwi peke yetu neema ya Mungu inatufunika, kututia moyo na kutuimarisha.
Tuchukue mfano wa mtu anayepambana kuacha pombe. Kwa miaka mingi, amekuwa akijaribu kuacha lakini kila mara anarudi tena. Lakini siku moja, anasikia mahubiri juu ya neema ya Mungu na anamua kumkabidhi Kristo maisha yake.
Haikuwa rahisi, lakini alipoanza kusoma Neno la Mungu, kuomba, na kushirikiana na Wakristo wengine katika ibada, alianza kuona mabadiliko. Aliweza kusema hili hapana lifike mwisho katika mazingira hayo utaonakwamba si kwa nguvu zake binafsi, bali kwa nguvu ya neema ya Mungu iliyokuwa ikifanya kazi ndani yake imemsaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine nzuri inayomsaidia kuimarisha ushirika wake na Mungu.
Mfano mwingine ni kijana anayeishi katika mazingira ya dhambi shuleni au kazini, kila upande kuna vishawishi. Lakini kwa kuwa ameamua kutembea na Mungu, anapojaribiwa, anakumbuka Neno la Mungu na huomba msaada. Anaposhinda, si kwa sababu yeye ni jasiri kuliko wengine, bali kwa sababu neema ya Mungu inampa ujasiri na nguvu ya kusema hapana dhambi sasa basi nataka kuwa chombo maalumu kwa ajili ya kazi ya Mungu. Siyo hivyo tu, tumesikia shuhuda nyingi watu waliokuwa wamezama katika uovu wezi, majambazi wakiacha dhambi hiyo na kutubu na kumrudia Muumba. Hayo yote yanapotokea yatupasa kutambua sio kwa nguvu zao bali ni neema tu ya Mungu inatenda kazi yake.
Tunaitikiaje Neema ya Mungu?
Katika Tito 2:11-12, Biblia inasema: “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa, nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa katika ulimwengu huu wa sasa.”
Neema haimaanishi kuishi tu kwa jinsi tunavyotaka; bali ni nguvu ya kuishi kwa kumpendeza Mungu. Inatufundisha kusema hapana kwa dhambi zote na ndiyo kwa mambo ya haki.
Neema na ushindi wa milele
Mwisho wa yote, neema ya Mungu ndiyo itakayotupeleka mbinguni. Kwa maisha haya tunayoishi, neema inatusaidia kila siku.
Warumi 5:20, Biblia inasema: “…lakini dhambi ilipozidi, neema ilizidi sana.”
Hii inatupa tumaini haijalishi majaribu ni makubwa kiasi gani, haijalishi dhambi ilitufunga kwa muda gani neema ya Mungu ni kuu zaidi. Tunaweza kuinuka tena, kuendelea mbele, na kushinda.
Wapendwa, majaribu ni sehemu ya maisha ya kila Mkristo. Lakini hatuko peke yetu. Neema ya Mungu ipo inatufundisha, inatufariji, inatufanya tusimame. Tukikumbatia neema hii, tutaweza kushinda kila jaribu.
Tusimsahau Yesu Kristo ambaye ni mfano mkuu alijaribiwa kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Na sasa, kwa kupitia kwake, neema hiyo imejaa na inapatikana kwa kila mmoja wetu.
Hebu tusimame imara katika imani, tukiitegemea neema ya Mungu kila siku. Tusiichukulie neema kwa kawaida, bali tuiheshimu, tuiamini, na tuiishi. Maana kwa neema, tumeokoka. Na kwa neema, tutashinda.
Mtu wa Mungu uliyepata nafasi leo hii kusoma ujumbe huu yamkini kuna mambo mengi yanakuzonga unatamani kuacha lakini hujui namna ya kutoka, iwe ni kusema uongo, iwe na kusengenya, iwe na udokozi ifike mwisho leo amua kusema ‘hapana’ na Mungu ingia ndani yangu nisaidie niishi maisha ya kukupendeza.
Nguvu za Mungu zinazofanya kazi kila mahali siku zote daima na milele zitakuhamisha kutoka hatua moja kwenda viwango vya juu.
Siku zote tamani kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili mwisho tuweze kuurithi ufalme wa Mungu tukiwa washindi.
Tuombe kwa ajili yako msomaji wetu, Mungu tunakushukuru kwa nafasi nyingine tena uliyotupa siku ya leo kuzungumza nawe kupitia nafasi hii ya Mahubiri gazetini, nguvu za Mungu zikawe nawe kila mahali ukimtanguliza kwa kila jambo na kumwamini katika yeye pekee.
Hatuna Mungu mwingine anayetupa nguvu za kushinda zaidi yako Mungu wa majeshi, kila mmoja wetu anapolianza juma akafanikiwe na kubarikiwa katika kazi za mikono yake. Amen