Songea_Ruvuma.
Katika kuhakikisha uchaguzi wa madiwani wa viti maalum unafanyika kwa haki, uwazi na amani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mjini kimewataka wagombea na wapiga kura kufuata taratibu za chama na kukubali matokeo yatakayotokana na mchakato huo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa kuwachagua madiwani wa viti maalum Mandwanga Omary Banda, amewahakikishia wanachama kuwa wote walioteuliwa kugombea ni wanachama halali na wenye sifa stahiki za uongozi.
Amewataka wagombea kuwa wavumilivu na kuepuka visasi baada ya matokeo, akisisitiza kuwa uchaguzi huo ni wa wazi na haki, na wajumbe wana uhuru wa kumchagua kiongozi wanayemuamini.
“Kila mmoja wenu ni bora, lakini ni wajumbe pekee ndiyo wenye jukumu la kuamua. Tukubaliane na matokeo bila chuki wala migawanyiko”.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Songea Mjini, Bi Bitrice Mchikoma, amesema kuwa wanachama 40 waliwasilisha nia ya kugombea, lakini baada ya mchakato wa ndani ya chama, majina 23 pekee ndiyo yaliyoidhinishwa kupigiwa kura.
Amebainisha kuwa fursa ya kupiga kura itatolewa kwa wajumbe pekee, na si kwa kila mwanachama. “Mchakato huu umezingatia taratibu za chama na leo, Julai 20, 2025, ndiyo siku ya uchaguzi,” alieleza.
Ameeleza kuwa zoezi la kuchukua fomu lilifanyika kati ya tarehe 28 Juni hadi 2 Julai, likifuatiwa na mchujo wa ndani ya chama hadi kufikia hatua ya leo ya kupiga kura.
Chama kimedhamiria kuhakikisha uchaguzi huo unaleta viongozi bora, waadilifu na watakaosimamia maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.