Moto jengo la Tanesco ulivyodhibitiwa

Lindi. Jengo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco ) Mkoa wa Lindi limeungua moto leo huku chanzo chake bado hakijajulika.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa kazi ya kuzima moto huo, Mrakibu Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Lindi, Joseph Mwasabeja amesema walipokea taarifa za tukio hilo saa 3:32 asubuhi.

“Tulipigiwa simu saa 3:30 na kufika eneo la tukio ndani ya dakika chache. Tulikuta moto umeshika kasi kubwa na tukashindwa kuingia kupitia mlangoni, hivyo tukalazimika kutumia dirisha ili kuweza kuuzima,” amesema Mwasabeja.

Amesema walifanya kazi ya kuuzima moto huo hadi saa 5:00 asubuhi na juhudi kubwa zilifanywa kuhakikisha unazimwa kabla ya kusambaa zaidi.


Hata hivyo, amebainisha kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea ili kubaini ulipoanzia.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi, Theodory Hall amesema walipatiwa taarifa za moto huo 3:20 asubuhi, ambapo ulianzia katika moja ya vyumba vya ofisi vinavyotumika kuhifadhi nyaraka.

“Baada ya kupata taarifa, tuliwasiliana haraka na Jeshi la Zimamoto ambao walifika kwa wakati na kuanza shughuli ya kuzima moto huo,” amesema Hall na kuongeza, “Kwa sasa tupo katika hatua ya kufanya tathmini ya uharibifu wa mali na kuendelea na uchunguzi wa chanzo.”


Naye Elizabeth John, mmoja wa mashuhuda waliokuwepo karibu na eneo hilo, amesema ya saa 3:00 asubuhi aliona moshi mwingi ukitoka kwenye jengo hilo na waliposogea waliona chumba kimoja kikiwaka moto.

Hakuna taarifa za majeruhi zilizotolewa, lakini mamlaka zimetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.