:::::::
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation itafanya kambi maalum ya huduma za uchunguzi na matibabu ya ubingwa bobezi bila malipo kwa wakazi wa mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kuanzia Julai 21 hadi 27, 2025.
Kwa wakazi wa mkoa wa Tanga kambi hiyo itafanyika Chuo cha Ualimu Korogwe Julai 21 hadi 23 na Kilimanjaro itafanyika soko la Memorial lililopo Manispaa ya Moshi, Julai 25 hadi 27, 2025.
Huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya macho, afya ya kinywa na meno, magonjwa ya akina mama na afya ya uzazi, magonjwa ya ngozi, magonjwa ya afya ya akili, sukari na homoni pamoja na saratani ikiwemo tezi dume.
Aidha, kambi hiyo itatumika kama jukwaa la kutoa elimu kwa wakazi wa mikoa hiyo na maeneo ya jirani namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tishio na kugharimu fedha nyingi kwa wananchi walio wengi.
Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila imekuwa na utaratibu wa kufanya huduma mkoba kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi ambapo kwa siku za karibuni ilitoa huduma mkoani Dodoma katika Wiki ya Utumishi wa Umma na wananchi zaidi ya 2000 walinufaika na huduma mbalimbali za Ubingwa Bobezi.