Riyadh. Mtoto wa mfalme wa Saudi Arabia aitwaye Al-Waleed bin Khaled bin Talal Al Saud, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kuwa katika hali ya kupoteza fahamu (coma) kwa miaka 20.
Kitalaamu Coma ni hali ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu. Inaweza kuwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jeraha la kichwa, kiharusi, uvimbe wa ubongo, au ulevi wa madawa ya kulevya au pombe.
Familia ya mwana huyo aliyejulikana kama “Mwanamfalme aliyelala” imethibitisha kifo chake hapo jana Jumamosi ya Julai 19, 2025. Vyombo mbalimbali vya habari duniani vimeripoti.
“Kwa nyoyo zilizojaa imani katika amri na hatima ya Mwenyezi Mungu, na kwa huzuni na masikitiko makubwa, tunamwombolezea mwanetu mpendwa Mwanamfalme Al-Waleed bin Khaled bin Talal bin Abdulaziz Al Saud, Mwenyezi Mungu amrehemu, ambaye ameaga dunia kuelekea rehema za Mwenyezi Mungu leo,” baba yake Mwanamfalme Khaled bin Talal bin Abdulaziz amechapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Mwanamfalme Al-Waleed aliingia kwenye hali ya coma mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 15 kufuatia ajali mbaya ya gari huko London.
Mwana huyo alienda kusoma katika taasisi ya kijeshi ya Uingereza huko London. Masomo yake yalikatizwa kabisa na ajali hiyo mbaya.
Alivuja sana damu kwenye ubongo na alirudishwa Saudi Arabia, ambapo alilazwa katika Hospitali ya King Abdulaziz Medical City huko Riyadh.
Licha ya kupata matibabu kutoka kwa wataalamu nchini Marekani na Hispania, mwanamfalme hakuwahi kurudia fahamu zake kikamilifu. Kwa karibu miaka 20, alibaki katika hali hiyo, akitegemea mashine ya kupumulia.
Mwanamfalme Al-Waleed, alizaliwa Aprili 1990, alikuwa mtoto mkubwa wa Mwanamfalme Khaled bin Talal.
Sherehe za kidini za kumuenzi Mwanamfalme Al-Waleed zitafanyika katika Msikiti wa Imam Turki bin Abdullah huko Riyadh, kulingana na News.com.au.
Ikumbukwe Baba yake, Mwanamfalme Al-Waleed, hakuwahi kukata tamaa kwamba mwanawe siku moja angepona kikamilifu. Aliendelea kupigania uzima wa mwanaye huyo hadi alipofariki hapo jana.