DEREVA Waleed Nahdi ametoa onyo kwa wapinzani wake, baada ya kushinda mbio fupi za magari za Mount Uluguru Auto Sprint zilizochezwa mwishoni mwa juma, mjini Morogoro.
Akiendesha gari aina ya Subaru Impreza N11, Nahdi aliibuka mshindi baada ya kuwashinda kasi madereva wote akitumia dakika 4:23:25.
“Kwangu, mbio hizi ni maandalizi kwa ajili ya ubingwa wa Taifa zitakazofanyika Morogoro Agosti na za ubingwa wa Afrika zitakazofanyika pia mkoani Morogoro Septemba mwaka huu. Naamini nitafanya vizuri pia katika mashindano yote mawili,” alisema Nahdi.
Mshindi wa pili alikuwa ni Marey Al Kithri aliyetumia dakika 4:33:29 akitumia Subaru Impreza N10.
Pia kulikuwepo na washindi kwa madereva walioendesha magari yasiyo maalum kwa mashindano (Street car) na Ahmed Balhabou aliyetumia dakika 4:35:28 aliibuka mshindi.
Mwenyekiti wa Klabu ya Mount Uluguru waandaaji wa mashindano, Gwakisa Mahigi aliwashukuru wadhamini na wadau wa mchezo huo kwa kufanikisha mashindano hayo.
Kulikuwa na madereva 10 kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro katika raundi hii, kwa mujibu wa Mahigi.
“Mashindano haya ya mbio fupi ni maadalizi ya raundi ya tatu ya mbio za magari ubingwa wa Taifa yatakayonyika mkoani Morogoro katikati ya mwezi wa Agosti.
Raundi ya tatu ubingwa wa taifa inatua mkoani Morogoro baada ya Iringa na Dar es Salaam kuandaa raundi mbili za awali.