Ndoto ya Asheri aliyetengeneza mchoro wa barabara, madaraja yaanza kutimia

Dar es Salaam. Safari ya kijana, Ridhiwani Asheri kutimiza ndoto yake imeanza kuiva, baada ya kutua jijini Dar es Salaam kukutana na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega katika ofisi ndogo za wizara hiyo, zilizopo Barabara ya Sam Nujoma jijini hapa.

Asheri aliyeambatana na mama na mjomba wake, walifika Dar es Salaam jana Jumamosi Julai 19, 2024 kwa mwaliko wa Waziri Ulega ambaye alitumia takriban saa mbili kuwatembeza katika miradi ya kimkakati iliyokamilika na inayoendelea kujengwa ikiwamo daraja la Kijazi wilayani Ubungo.

Maeneo mengine aliyotembelea leo Jumapili Julai 20,2025 Asheri ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mwendokasi ya Tegeta, daraja la Tanzanite, Stesheni ya SGR, daraja la Kigamboni na Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa.


Kwa mujibu wa Asheri, maeneo aliyoyatembelea ilikuwa ndoto yake kubwa aliyoitamani kufika, kwa sababu awali aliishia kuyaangalia kwenye picha na video kupitia taarifa za habari, huku akitumia nafasi hiyo kufanya ubunifu wa kuyatengeneza.

Asheri mwenye kipaji na ubunifu, amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania baada ya kipande cha video yake kusambaa ikimuonyesha akiwa ametengeneza mji, barabara, majengo na madaraja kutumia miti, vipande vya makopo ya plastiki, mbao na vitu vingine ambavyo unaweza kusema ni mabaki au uchafu.


Kwa ustadi mkubwa mabaki hayo yameonyesha taswira ya mji, tena wa kisasa. Kwenye eneo pembeni mwa nyumba anayoishi chini ya miti, ndipo Asheri amejenga miji yake iliyopangiliwa vizuri, ikionyesha madaraja, majengo marefu na madogo, barabara za juu na chini.

Video hiyo iliwashangaza wengi, baadhi wakihoji kipaji na ubunifu wa mtoto Asheri na kuanza kuuliza mahali anapopatikana.

Baada ya kuonekana katika mitandao ya kijamii, Waziri Ulega alituma timu ya wataalamu wa wizara hiyo waliokwenda nyumbani kwa Asheri Mtaa wa Sakosi uliopo Mji Mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, mkoani Dodoma kwa lengo la kufanya mazungumzo naye.

Alivyoingia ofisini kwa Ulega

Baada ya kushuka kwenye gari, Asheri pamoja na mama yake, Vumilia Ndagala walielekea moja kwa moja ofisi ya Ulega na kuketi sehemu maalumu kwa ajili ya kumsubiria waziri huyo.

Akiwa ameketi kumsubiri Waziri Ulega katika ghorofa ya 12, Asheri alionekana kushangazwa namna Jiji la Dar es Salaam linavyoonekana kwa juu akitumia muda huo kuwauliza maswali baadhi ya maofisa wa wizara hiyo.


Asheri alisikika akisema: “Natamani kuona madaraja makubwa ya Dar es Salaam, uwanja wa mpira wa miguu, barabara za mwendokasi natamani, naamini nitapelekwa kuyaona…”

Baada ya kusubiri kwa dakika kadhaa hatimaye Waziri Ulega akawasili ofisini hapo huku akionekana kuwa na shauku na bashasha ya kumuona kijana huyo, ambaye kwa siku kadhaa alivuma katika mitandao ya kijamii kutokana na kipaji na ubunifu wake.

Katika maelezo yake, Waziri Ulega amesema baada ya kuona video fupi ya Asheri katika mitandao ya kijamii ilimvutia akisema alikuwa akipata simu na ujumbe mbalimbali kutoka kwa wadau waliovutiwa na kipaji cha kijana huyo.

Wakati Ulega akieleza hayo, mama Asheri alionekana mwenye furaha huku mwanaye akiwa kimya katika hali ya utulivu akimsikiliza kwa makini kiongozi huyo.

“Baada ya timu ya wataalamu kuja nyumbani wamenikabidhi ripoti na nimefanya uamuzi mje Dar es Salaam ili kwanza kutimiza ndoto za Asheri. Pili, Asheri aone kwa macho kile alichokuwa akikusudia kukifanya na kipo Dar es Salaam.

“Lakini pia Asheri aone kwa macho yake yale anayoshuhudia katika luninga. Wataalamu wangu wamenipa mrejesho na nimeshawasiliana na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda kwa sababu suala lake lipo kielimu na inatakiwa kuendeleza ndoto zake,” amesema Ulega.

Waziri Ulega amewahakikishia wazazi wa Asheri, kuwa Serikali itahakikisha ndoto, matamanio na ubunifu wa kijana hayatapotea ili kuwa chachu kwa vijana wengine.

 “Tumefurahishwa sana na ubunifu wa Asheri, tunamtakiwa kila la heri na tunawatia moyo wazazi wengine vijiji wasiviache vipaji vya watoto. Tutamfikisha mahali pazuri kuhusu elimu ya Asheri, hatutaki kumfikisha mahali ambapo tutakwama au kugonga ukuta, tunataka akienda mahali pawe sahihi ili kutimiza ndoto zake.

“Lengo letu si kufanya ubabaishaji bali tufanye jambo la uhakika kwa ajili ya Asheri, kijana huyu tutamtunza na kufuatilia mienendo yake kazi hii itafanywa na wizara, bodi ya usajili wa wahandisi,” amesisitiza.

Katika mazungumzo hayo, Asheri alikabidhiwa fedha taslimu kwa ajili ya maandalizi ya mahali atakapopelekwa kwa kuendelezwa kielimu, kipaji na ubunifu wake.

Alichokisema mama, mjomba

“Hakuwahi kufika Dar es Salaam, alikuwa anaangalia majengo kwenye luninga kisha anachora, mwishoni akawa mbobezi wa ile kazi. Tunashukuru akiendeleza atakuwa msaada kwa Taifa Mungu akubariki sana,” amesema Ndagala.

Naye mjombe wake, Yona Albert amesema ilikuwa kama mzaha lakini Mungu ana makusudio yake kuhusu hatua aliyoifikia Asheri.


“Nilipofika nyumbani sikuwa na lengo la kuchukua video ile, lakini ni Mungu ikatokea nikachukua, tunashukuru kwa ushirikiano wenu kuanzia Dodoma, hadi sasa tupo Dar es Salaam.

“Vile vitu alivyokuwa akibuni na kuvitengeneza anavishuhudia kwa macho sasa hivi. Zile ndoto alizokuwa anaota sasa anazishuhudia vizuri bila kuhadithiwa,” amesema.

Safari ya matembezi yaanza

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho kifupi safari ya matembezi ikaanza ambapo daraja la Kijazi, ndicho kilikuwa kituo cha kwanza kisha wakaelekea eneo la Mwenge kuangalia ujenzi wa barabara ya mwendokasi.

Msafara huo ulielekea hadi daraja Tanzanite lililojengwa juu ya bahari, ambapo katika matembezi hayo Asheri alionekana mtu mwenye shauku ya kutaka kujua jambo fulani au kupata ufafanuzi kutokana kwa waziri, na kiongozi huyo alimpa ushirikiano wa kutosha kwa kile alichokihitaji.

Baada ya kumaliza eneo la Tanzanite msafara ulielekea Stesheni ya SGR kisha kumalizikia Uwanja wa Benjamin Mkapa na daraja la Kigamboni.