LICHA ya nguvu ya ziada iliyotumiwa na mabosi wa Simba kumshawishi beki na nahodha aliyemaliza mkataba wake ndani ya kikosi hicho, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kumshawishi abaki, lakini imeshindikana kufuatia mwenyewe kuaga jioni ya jana Julai 19, 2025.
Baada ya uwepo wa taarifa za Tshabalala kusaini mkataba wa miaka miwili na Yanga, uongozi wa klabu hiyo ulikaa kikao mchana wa Julai 18, 2025 na baba mzazi wa staa huyo Hussein Mohamed pamoja na Heri Chibakasa maarufu Heri Mzozo ili kuona unamshawishi vipi kutoondoka.
Mtoa taarifa amebainisha kwamba, sababu za uongozi wa Simba ukiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ kukaa kikao hicho na familia ya Tshabalala sambamba na Mzozo, ni kutokana na mchezaji huyo kwa mara ya kwanza wakati anatua Msimbazi mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar, Mzozo ambaye ni kiongozi mkongwe wa timu ya Friends Rangers, alihusika kwa kiasi kikubwa kwani ndiye aliyemlea kisoka.
“Try Again alihitaji kukutana na baba yake Tshabalala na Mzozo ili kulimaliza jambo hilo kwa amani na kumpa mchezaji heshima anayostahili kwa kuitumikia Simba kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Tshabalala na Simba hawana tatizo kabisa, changamoto inakuja mchezaji anapowaambia viongozi ishu yake ya kuongeza mkataba iwe chini ya msimamizi wake Carlos Mastermind ambaye anaonekana haelewani na mmoja wa kigogo wa timu hiyo.
“Carlos hakulipwa pesa zake wakati wa mkataba ulioisha wa Tshabalala, jambo ambalo linawafanya wasiwe na maelewano mazuri katika kutaka kuongeza mkataba mpya, ndiyo maana Simba ilihitaji mazungumzo na Mzozo ambaye bado anamuongoza Tshabalala katika masuala mbalimbali ya mpira wa miguu.”
Mtoa taarifa huyo aliendelea kwa kusema: “Kikao kilifanyika lakini hakukuwa na mabadiliko, mpaka sasa asilimia 80 Tshabalala anakwenda Yanga.”
Hivi karibuni, Mwanaspoti liliandika kuhusiana na Yanga kumtumia mkataba Tshabalala akiwa na timu ya Taifa Stars, iliyoweka kambi nchini Misri kujiandaa na michuano ya CHAN pia Simba ilifanya hivyo ila sharti lake aliwataka warudi kwa meneja wake Carlos.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, naye hivi karibuni alinukuliwa na Mwanaspoti akisema mazungumzo ya uongozi wa klabu hiyo na Tshabalala kuhusu mkataba mpya yalifanyika kabla ya aliokuwa nao haujamalizika, lakini hawakufikia kwenye makubaliano.
“Tukisema tunaachana na Tshabalala pia ni kwa maslahi ya Simba na mchezaji mwenyewe na lazima wanasimba wakubali hilo kwamba unakuja na unaweza kuondoka, hakuna mtu angetamani kuona nahodha wa timu anaondoka, muda ukishaamua umeamua,” alisema Ally ambaye alisisitiza beki huyo aliyedumu Simba kwa miaka 11, ni mchezaji huru na walitamani kuendelea naye.