Tunapofanya kitu chochote maishani, hatuna budi kufahamu dhahiri namna au mbinu bora ya kufanya kitu hicho.
Kwa kujua kufanya kitu hicho kiusahihi, ni wazi kwamba utafanikiwa na kwa kutojua kufanya kitu au jambo hilo, basi ni wazi kwamba utashindwa.
Yako mambo mengi sana maishani yana kanuni za kuyafanya, usipozijua kanuni hizo lazima ama ushindwe kuyafanya au uyafanye vibaya.
Katika kuyarahisisha maisha na kufanya mambo yetu yatuendee vema mara nyingine inatulazimu kubadili namna tunavyofikiri, kwa sababu yumkini ugumu tunaokutana nao unaletwa na misimamo au fikra zetu.
Mbinu moja ya muhimu sana katika kuyafikia mabadiliko ya kweli kwanza ni kubadili namna tunavyofikiri.
Ziendee fursa, usisubiri zikufuate
Huna haja ya kusubiri kuambiwa nini cha kufanya, waza, sugua kichwa, fikiria nini kinatakiwa kufanyika, wakati gani, na kwanini, kuwa mgunduzi na mvumbuzi, kamata fursa. Jifunze kubeba majukumu juu ya maisha yako wewe mwenyewe, usiwe mtu wa kutoa visingizio katika kila kitu.
Beba majukumu hata kama mara nyingine yanahusisha lawama. Kuwa dereva wa maisha yako wewe mwenyewe, kamwe usimkabidhi mtu mwingine funguo za kuyaendesha maisha yako. Hilo ni kosa kubwa sana.
Kama usipokuwa mvumbuzi, mgunduzi na unayeziendea fursa, basi unawaruhusu watu wengine kuweza kuyaendesha maisha yako.
Anza na mwisho akilini mwako
Kabla haujakianza kile unachotaka kukifanya, anza kwanza na kufikiria jinsi mwisho wake utakavyokuwa, usikurupuke na kuanza chochote kabla haujairuhusu akili yako kuwaza namna mwisho wa kile ukitakacho utakavyokuwa. Fahamu wapi unapotaka kwenda na wapi hiyo ndoto yako inakupeleka. Usiwaruhusu watu wengine au mtu mwingine aongoze ndoto yako. Najua wako washauri na waelekezaji, hii ni sawa, Upo ushauri na maelekezo utapaswa kufuata na mengine hayana maana kufuata, pamoja na kuelekezwa au kushauriwa bado inakupasa kushika usukani wa kuiendesha ndoto yako wewe mwenyewe.
Fahamu kila ambacho kinatakiwa katika kuyafanikisha maisha yako. Kabla hujaendelea na ndoto za kuwa mjasiriamali, waziri, au mfanyabiashara mkubwa, kwanza jitazame na ujione kama mmoja wa hao.
Kumbuka kuwa jinsi ujionavyo nafsini mwako ndivyo ulivyo. Wakati unapojitahidi kufikiri na kutazama mwisho wa kile unachotaka kukifanya, pia fikiria juu ya malengo yako. Rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy aliwahi kusema: “Jitihada pamoja na hamasa havitoshi pasipo lengo na mwelekeo”.
Weka vitu vya kwanza viwe vya kwanza
Jifunze kuvipa kipaumbele vitu unavyovifanya, usifanye tu kwa sababu hauna budi kufanya, weka akili yako na nishati zako zote katika kile unachokifanya.
Wakati unaangalia nini cha kufanya, anza na vile ambavyo ni vya lazima na vyenye umuhimu kabla ya kuviendea vile visivyo vya lazima na vyenye umuhimu mdogo, ila tusije kuvifanya vitu vingine kuwa vya lazima kwa sisi wenyewe kuwa wavivu.
Haina haja ya kulundika majukumu mengi ili uje uyafanye kwa kuzima moto, hii sio tabia nzuri na haina ufanisi kabisa. Fahamu tofauti iliyopo baina ya mambo ya haraka na mambo muhimu. Jifunze kuwa mwangalifu sana ili kupunguza uharaka wa mambo.
Viko baadhi ya vitu ambavyo ni muhimu na vinahitaji uharaka. Viko vingine vinahitaji uharaka lakini sio vya muhimu sana. Viko ambavyo sio vya haraka lakini ni muhimu na pia vingine sio vya haraka na sio vya muhimu.
Waza katika dhana ya “wote tushinde/ wote tufanikiwe”
Usiwe mbinafsi, hakuna mafanikio ya kweli kwenye ubinafsi; hakikisha kila unachokifanya hakikunufaishi wewe peke yako bali kinawanufaisha na wengine pia.
Kwa kufanya hivyo wewe pia utanufaika na kufanikiwa. Kamwe usiwe na mtazamo wa “kama haitoninufaisha mimi basi mwingine yeyote asinufaike” na “kama sifanikiwi mimi basi hakuna mwingine kufanikiwa”.
Najua kabisa kwamba ushindani upo, na ushindani ni mzuri lakini sio katika kila kitu tunaweka au kuendekeza ushindani. Mama Theresa aliwahi kusema: “Mafanikio ya kweli sio yale yanayogusa maisha ya mtu peke yake bali ni yale yanayogusa maisha ya watu wengine pia”.