Dodoma. Uwanja wa ndege wa jijini Arusha ulioko eneo la Kisongo, utaanza kutoa huduma za kuruka na kutua ndege saa 24, Desemba mwaka huu.
Mbali na hilo, Sh5.93 bilioni zimetumika katika kuwalipa fidia wananchi 187 watakaopisha ujenzi wa Uwanja cha ndege Ziwa Manyara.
Hayo yamesemwa leo Jumapili, Julai 20, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi alipokuwa akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwenye mkoa wake.
Amesema kufuatia ongezeko la watalii nchini, uliochagizwa na Filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa huo umepokea Sh103 bilioni kwa ajili ya uboreshaji wa viwanja vya ndege viwili.
Juni 27,2025 Rais Samia akihutubia bunge jijini Dodoma, alisema ongezeko ni kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii milioni 2.41 mwaka 2025 huku kwa watalii wa ndani wakiongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 3.218.
Amevitaja viwanja hivyo ni Arusha na Ziwa Manyara na kuwa fedha hizo zimefanya maboresho ili kuvipa hadhi na kuongeza idadi ya abiria kufuatia idadi ya miruko.
“Kuboresha eneo la maegesho ya magari Sh640 milioni na Sh2.8 bilioni zimetumika kujenga jengo la kisasa la abiria pamoja na kuongeza barabara za kurukia ndege,” amesema.
Kihongosi amesema ujenzi umekamilika na umeanza kutoa huduma kwa abiria.
Amesema uwanja huu wa ndege ni wa pili kwa miruko ya ndege Tanzania na watatu kwa idadi ya abiria ikifuatia Uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro na Julius Nyerere wa jijini Dar es Salaam.
Amesema pia Serikali imetoa Sh11 bilioni kwa ajili ya kutengeneza mindombinu ya taa za kuongozea ndege.
Amesema matengenezo hayo yakikamilika utaanza kufanya kazi kwa saa 24 na kupokea ndege za kimataifa.
Aidha, Kihongosi amesema Sh88.53 bilioni zimetumika kuboresha Uwanja wa ndege Ziwa Manyara.
“Mradi ambao utasaidia kufikia malengo ya utalii katika ukanda wa Kaskazini ukiwemo Mkoa wa Arusha,” amesema.
Aidha, Kihongosi amesema kupitia Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro Mkoa unatekeleza Mradi wa ujenzi wa jengo la Makumbusho ya Jiolojia ya Kisasa (Ngorongoro – Lengai Unesco Global Geopark).
Amesema jengo hilo limejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, kwa gharama Sh25 bilioni.
“Jengo hilo ni maktaba ya inayoonyesha mandhari ya vituo vyote vinavyopatikana ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro Crater pamoja na jamii zote zilizowahi kuishi ndani ya bonde hilo la Ngorongoro,” amesema.
Amesema lengo ni kulinda na kutangaza urithi wa jiolojia na utamaduni ndani ya hifadhi na kuongeza maudhui ya kielimu kupitia muundo wa makumbusho yenye taarifa za kisayansi.
Lengo lingine ni kuboresha huduma na muda wa kukaa wageni na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kuhusu ujenzi wa barabara, Kihongosi amesema kuwa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Uwanja ndege wa Arusha hadi mjini unaendelea lengo likiwa ni kupunguza msongamano kwenye jiji hilo.
Pia amesema mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara kutoka Arusha kwenda Wilayani Kongwa mkoani Dodoma umeshasainiwa.
Mmoja wa wakazi wa Arusha kwa Mrombo, Doreen Aloyce amesema uwepo wa uwanja hicho utaleta fursa kwa wafanyabiashara wanaofuta bidhaa nje ya nchi na ndani ambapo badala ya kutumia siku nzima kwenda Dar es Salaam, sasa watatumia saa chache.
“Mfano wafanyabiashara ya maua wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenda Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) kusafirisha mazao hayo, lakini kukamilika kwa uboreshaji wa uwanja wa Arusha utapunguza gharama kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Pia amesema uboreshaji huo, utarahisisha usafiri kwa watalii wanaokwenda kutembelea vivutio mbalimbali katika mikoa ya Arusha na Manyara.