Vigogo SADC kukutana Dar kujadili ulinzi, siasa na usalama

Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya masuala ya siasa, ulinzi na usalama (MCO).

Mkutano huo utafanyika kuanzia kesho Jumatatu Julai 21 hadi 25, 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

MCO ni miongoni mwa mikutano ya ngazi za juu ya SADC, ambayo hufanyika Julai kila mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu amani, siasa na usalama katika nchi za ukanda wa SADC.

Mkutano huo utawakutanisha wajumbe wapatao 300 wakiwemo mawaziri na maofisa waandamizi wanaoshughulikia masuala ya Mambo ya nje, ulinzi, mambo ya ndani na usalama wa umma kutoka nchi wanachama zote 16 za SADC.

Mkutano unatarajiwa kujadili hali ya ulinzi, siasa na usalama katika kanda, ikiwa ni pamoja na kutathmini utekelezaji na kupanga mikakati ya kushughulikia changamoto zilizopo.

Vilevile, utajadili uimarishaji wa mifumo ya kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro ikiwemo mifumo ya tahadhari ya mapema inayoweza kufuatilia na kufahamu viashiria vya hatari vya kisiasa, kiusalama, kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa leo Jumapili Julai 20, 205, mkutano huo unafanyika nchini kwa kuwa Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025.

“Itakumbukwa Agosti 18, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo. “Nafasi hii muhimu imeiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mstari wa mbele katika kusimamia masuala yanayohusu amani, usalama na uthabiti wa kikanda kwa mujibu wa Itifaki ya SADC ya siasa, ulinzi na usalama,” imeeleza taarifa hiyo.

Mkutano huo utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ambaye ni Mwenyekiti wa MCO.

Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu kitakachofanyika Julai 21 na 22, 2025 na kuongozwa na Balozi Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika kipindi cha uenyekiti wake, Tanzania imeendelea kuwa kinara na juhudi za kuimarisha amani na ushirikiano wa kisiasa ndani ya kanda ya SADC, hasa kupitia Misheni za Uangalizi wa Chaguzi za SADC (SEOMS) katika chaguzi kuu zilizofanyika kwenye nchi wanachama za Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia.

Misheni husika ziliongozwa na wakuu wake kutoka Tanzania walioteuliwa na Rais Samia kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa SADC Organ.

Aidha, Tanzania iliratibu na kuongoza mikutano kadhaa ya kimkakati ya ngazi ya juu ya Asasi hiyo, ikiwa ni pamoja na mikutano mitano maalumu ya wakuu wa nchi na Serikali wa SADC kati ya Novemba 2024 na Machi 2025, ambayo ilijadili masuala ya kulinda na kuendeleza amani na usalama wa kikanda.

Sambamba na hilo, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kihistoria wa pamoja wa kwanza wa wakuu wa nchi na Serikali wa jumuiya za SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Februari 8,2025, Dar es Salaam ambao uliitishwa mahususi kwa lengo la kujadili hatua jumuishi za kurejesha hali ya usalama Mashariki mwa DRC.

Mbali na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza nafasi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama kinara katika masuala ya amani na usalama katika ukanda huo, mkutano wa MCO unatoa fursa ya kuonesha urithi wa kitamaduni na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ambavyo vimeendelea kuongoza kikanda na kimataifa na kusababisha kushinda tuzo ya nchi yenye vivutio bora vya utalii duniani.