Dar es Salaam. Kuna kisa kimoja kilitokea huko Mombasa Kenya. Bwana mmoja alikuwa na mkewe pamoja na watoto. Huyu bwana alikuwa akitafuta riziki zake kwa kuongoza watalii kwenye pwani ya Mombasa.
Siku moja, alimpata mzungu mwanaume aliyetokea kuzoeana naye. Huyu mzungu, kila akija, humwambia amtafutie wanawake wa kufanya nao ngono kwa malipo aliyoona manono kwake.
Mara ya kwanza, huyu bwana alimtafutia mteja wake wanawake na kumalizana naye. Kwa vile ni watu waliokuwa wanaishi eneo moja, yule mteja alikwenda kumshukuru yule baba kwa kumtafutia mteja aliyemlipa vizuri.
Hivyo, alimkatia pesa nzuri sana kutokana na ukuwadi wake. Yule baba alishangaa kugundua kuwa kumbe yule mteja wake alikuwa akiwalipa pesa nono wanawake aliokuwa akiwachukua.
Mara ya pili, yule mzungu alirejea baada ya miaka kama miwili hivi na akamtaka, kama kawaida yake amtafutie mwanamke wa kutumia naye kwa wakati ule ambao alikaa Mombasa.
Hivyo, kwa kujua namna yule bwana anavyotoa dau kubwa, aliona kwanini riziki kwenda mbali wakati mkewe angeweza kutumika na kuingiza hicho kipato kinono?
Kwa tamaa ya kupata asijue anaweza kupatikana na kujuta, alimshauri mkewe akubali. Kwenda kutumia naye na akakubali lakini akiwa anashangaa mantiki gani ya muwe kufanya hivyo.
Mwanzoni, alidhani mumewe alikuwa anamtega kuona kama alikuwa mwaminifu. Hata hivyo, alipotaka mumewe amhakikishie kuwa si mtego, yule mama alikubaliana na mumewe kwa shingo upande asiamini kuwa mumewe hakuwa akimthamini kiasi hicho kiasi cha kumgeuza kifaa cha kutafutia riziki.
Pamoja na kukubali ushauri wa mumewe, mke aliona kama anadhalilishwa na kuamua kuondoka na yule mzungu. Hivyo, pamoja na kukubali kwenda, alipanga namna ya kumkomesha mumewe aliyemuona kama alikuwa akimchukulia kama kifaa kisicho na thamani ya pekee kiasi cha kumkodisha kama gari au nyumba tena kwa malipo ya fedha.
Kwa kujua thamani yake, yule mama, hakuona uzuri wa kwenda kufanya umalaya ili kupata fedha tena kwa kushauriwa na mumewe. Hivyo, aliamua ama aachane na yule mume au amridhishe yule mzungu lau ampe mtaji aanze maisha yake aondokane na aibu na utumwa huu.
Kweli, kila aombaye hupewa. Yule mzungu alitokea kumpenda yule mama kiasi cha kutamani amuoe kama angekuwa tayari. Na bahati mbaya, yule bwana hakumwambia kuwa yule mama alikuwa mkewe.
Hivyo, baada ya kunogewa na kuridhika, yule mzungu alimuuliza yule mama kama alikuwa ameolewa au kwenye uhusiano. Mama alimwambia kuwa alifiwa na mumewe miezi michache iliyopita na aliamua kumkubalia kutumia naye kwa sababu yule bwana aliyemtafuta alisema alikuwa ni mtu muaminifu sana.
Mzungu kusikia hivyo, alizidi kupenda. Alimuomba amuoe lau aweze kuachana na mateso yaliyosababishwa na kifo cha mumewe.
Kwa kujua, kuwa yule bwana angeweza kutibua dili, alimuomba waondoke kwenda kutumia Zanzibar, na huko wapange namna ya kwenda kufunga ndoa Ulaya.
Mambo yalipangwa yakapangika. Wawili walienda zao Zanzibar kustarehe na baadaye kuelekea Ulaya tayari kuwa mke na mume. Kwa kuhofia mumewe angeweza kutibua dili, alimuomba waondoke kimya kimya kwa sababu yule bwana, yaani mumewe, aliyemkuwadia yule mzungu alikuwa akitaka wagawane fedha nusu kwa nusu kwa kuwa bila yeye asingepata mteja.
Mzungu kusikia vile alichukia na kumuona mume wa yule mama hakuwa mwaminifu na alikuwa mwenye tamaa kwa vile alikuwa akimlipa fedha ya kutosha kumkuwadia. Hivyo, alikubaliana na pendekezo hili kirahisi.
Yule Bwana alishangaa maana, alitegemea mkewe angerejea asubuhi. Alipoona harejei, alijiaminisha kuwa alikuwa amepewa dau kubwa la kutumika kwa zaidi ya siku moja. Hivyo, hakuwa na shaka mkewe angerejea na kibunda cha kutosha asijue kuwa kumbe asingemuona tena maisha yake yote.
Vitu hata viwe na thamani gani, unaweza kuuza, kukodisha hata kugawa lakini si mtu. Je hapa tunajifunza nini? Ungekuwa wewe ungefanyaje? Je uamuzi wa yule mama kuondoka maisha yote ilikuwa ni uamuzi mzuri au mbaya?
Somo kubwa ni kwamba mwenza wako ana thamani kuliko kitu chochote. Hivyo, hata uwe na shida au changamoto kiasi gani, acha kumtumia kama kitu. Hata kufikiria tu ni dhambi isiyo na msamaha.