WASHINDI 2200 WA AWAMU YA KWANZA KAMPENI YA ‘’MIAMALA NI FURSA ’’ YA BANK OF AFRICA TANZANIA WAZAWADIWA

Na Mwandishi Wetu Michuzi Tv

WATEJA 20 wa Bank of Africa Tanzania, wamefanikiwa kujinyakulia ushindi wa shilingi 50,000 kila mmoja wao kupitia kampeni ya kupata huduma za kibenki kwa njia ya kijidigitali inayojulikana kama “Miamala ni Fursa, iliyozinduliwa mwezi uliopita.

Kampeni hii ya miezi mitatu iliyoanza Juni 4, 2025 imelenga kuhamasisha wateja wa benki kutumia huduma za kidigitali kupata huduma mbalimbali za kibenki, ambapo wanazawadiwa kutokana na mihamala wanayoifanya ikiwa ni moja ya dhamira ya benki kukuza matumizi ya huduma za kidigitali na ujumuishaji wananchi katika huduma za kifedha nchini kote.

Akizungumzia maendeleo ya kampeni hiyo Afisa Mkuu wa Huduma za Kidigitali Lameck Mushi alisema,” “Tumefurahi kuona wateja wetu wengi wamejitokeza kushiriki. “Miamala ni Fursa” tayari inaendelea kuwawezesha wateja wetu kufurahia huduma zetu za kidigitali na kurahisisha maisha yao ya kila siku, wateja wanajishindia zawadi kupitia kufanya miamala ikiwemo ya kulipia huduma mbalimbali pia tumepunguza makato ya kutumia huduma zetu za kidigitali kwa asilimia 50% ili kuwapatia unafuu wetu wote na kuona urahisi wa kuzitumia kufanya mihamala”.

Kila wiki, wateja watano wenye bahati ambao watafanya miamala ya kutoa fedha benki kwa njia ya kidigitali na kufanya mhamala wa kulipia huduma watakuwa katika nafasi ya kuingia katika droo ya kumpata mshindi.

Mwisho wa kampeni, ambayo inaendelea hadi Septemba 2025, mshindi mmoja wa zawadi kubwa ataweza kujishindia kiasi cha shilingi milioni 5.

Asupya Nalingigwa, Mkuu wa kitengo cha huduma za Rejareja, alisisitiza: “Lengo letu ni kufanya huduma za kibenki kupatikana kwa urahisi , kuzawadia wateja wetu na kuwa karibu na wateja popote pale wanapokuwa iwe sehemu za mijini ama vijijini wakifanya miamala kwa njia ya kidigitali watakuwa na nafasi ya kushiriki na kushinda”,

Ili kuhakikisha ushiriki kwa wateja wengi, Bank of Africa, imewapanga wafanyakazi wake katika matawi yote kote nchini kuwapa wateja mwongozo wa kutumia huduma zake za kidigitali na kutatua changamoto zozote wanazopata katika matumizi ya huduma hizo.

Naye, Nandi Mwiyombella, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, ameongeza: “Kampeni hii mbali ya kuwazawadia wateja pia ni wezeshi kwa kuwa kuhamasisha matumizi ya kidigitali kupata huduma za kibenki tunasaidia Watanzania wengi kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha.”

Zawadi za kujishindia bado zipo na washindi wapya watakuwa wanatangazwa kila wiki, Bank of Africa – Tanzania, inawaalika wateja wote kufanya mihamala kidigitali, kushinda, na kupata uzoefu wa urahisi wa kupata huduma za kibenki mikononi mwao.

Wateja walioibuka washindi katika awamu hii ya kwanza ni Hussein Ally Massomo, Saidi Mohamedi MpateJoseph Jackson Malugu, Jeroen Jochem Metselaar,Pascazia Kokushubila Bash,Elibariki Fanuel Mkireri,Majaliwa Maingu Mayengela,Simon Alphonce Sabasaba,Angel Josephat Nationota na David Mutumba Hamli.

Wengine ni Daruni E.A Transport Co, Hussein Jafari Yogopeni, Monica Alex Bugomola, Andrew Joseph, Alfred Raphael Bavuma, Justice Valence, Omega Elias Mmbando, Allan Juma Wastara, Mpoint Office Solution na Ramadhani Yasin Namakweto.